Raila Amolo Odinga
Raila mwenye umri wa miaka 68 wa chama cha ODM ingawa kwa sasa anagombea urais kwa muungano wa CORD, ameamua kushirikiana na makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, ambaye pia alikuwa hasimu wake miezi miwili tu kabla ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Aliondoka kutoka chama cha ODM na kuunda chama chake ODM-Kenya na hata kuitikia uteuzi wake kama makamu wa rais wa serikali ya Rais Mwai Kibaki.
Kama hayati babake, Jaramogi Oginga Odinga, Raila ambaye ni waziri mkuu wa kwanza wa Kenya, kwa miaka minane aliishi kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 hadi 1991 kwa harakati zake za kupigania mageuzi wakati wa muhula wa pili wa utawala wa rais Daniel arap Moi.
Kufuatia kuundwa kwa katiba mpya, mwezi Agosti, mwaka 2010, amekuwa akisema kwenye kampeini zake kuwa nia yake ni kuleta mageuzi ya kisiasa.
Raila ni mwanasiasa anayesifika sana kwa ushawishi wake kisiasa na ambaye amekuwa katika msitari wa mbele kuunda vyama vya miungano na wanasiasa ambao ni mahasimu wake.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 1997 ambapo Raila alishikilia nafasi ya tatu, kufuatia kuundwa kwa muungano wa chama chake (NDP) na chama cha rais wa zamani Daniel moi (KANU), aliteuliwa kama waziri wa kawi katika serikali ya muhula wa mwisho wa Moi.
Mwaka 2002, baada ya Moi kumuunga mkono uhuru Kenyatta, kama mrithi wake, Raila na maafisa wengine wa KANU ikiwemo Kalonzo Musyoka na wafuasi wengine, walipinga ungwaji mkono wa Kenyatta kugombea Urais. Waliungana na kiongozi wa upinzani Mwai Kibakina na kuunda muungano wa National Rainbow Coalition (Narc) ambao baadaye ulishinda uchaguzi wa mwaka 2002.
Wakati Kibaki alipomfuta kazi na washirika wake, aliunda chama cha ODM ambacho kilipiga kura ya La dhidi ya rasimu ya katiba mpya. Aliongoza kampeini mwaka 2007 na kwa shingo upande kukubali ushindi wa rais Kibaki
Katika uchaguzi uliokumbwa na utata , ghasia na mauaji. Lakini hatimaye alilazimika kujiunga na Kibaki katika serikali ya Muungano.
Disemba mwaka 2012, Raila alilazimika kupiga moyo konde na kurudiana na Kalonzo Musyoka chini ya muungano wa CORD, kwani daima husema katika siasa, hakuna maadui wa kudumu.
Raila anaamini kuwa wakenya wanastahili kuhudumiwa vyema zaidi kuliko ahadi wanazopewa na kwamba chini ya utawala wake, Raila anaahidi kuleta mageuzi na kuhakikisha uongozi bora. Anaahidi kuwa serikali yake itaekeza katika viwanda vya kisasa , mabohari pamoja na vituo vya teknolojia ya mawasiliano katika maeneo ya kuvulia, ushirikiano na sekta ya kibinafsi ili kuimarisha kilimo.
Comments