NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII, DK SEIF RASHID AKIFUNGUA KONGAMANO LA 8 LA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA NA WANAHABARI MTWARA
HOTUBA YA MHE. DKT.
SEIF S. RASHID (MB.),
NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII KATIKA KONGAMANO LA NANE LA BIMA YA AFYA LA WANAHABARI, KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA ELIMU MTWARA TAREHE
21 - 22 FEBRUARI, 2013
·
Mheshimiwa
Hawa Abdulrahman Ghasia, Waziri - Ofisi
ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
·
Mheshimiwa
Aggrey Deaisile Mwamri - Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa,
·
Mheshimiwa
Abass Kandoro - Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa,
·
Mheshimiwa
Joseph Simbakalia - Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
·
Mwakilishi
wa Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya
· Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya za Mikoa ya Mtwara na Lindi,
· Wakurugenzi wa Halmashauri za Mikoa ya Mtwara na Lindi,
· Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya
– Mikoa ya Mtwara na Lindi,
· Bwana Emanuel Humba, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,
· Waratibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii wa
mikoa ya Mtwara na Lindi,
· Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali,
· Wageni Waalikwa,
· Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Afya njema siku ya leo na kutuwezesha kukusanyika
hapa. Vile vile, naushukuru Uongozi wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika Kongamano hili
muhimu kwa Ustawi wa Sekta ya Afya. Kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, napenda niwakaribishe wote na kuwatakia heri ya mwaka mpya, 2013. Pia niwashukuru wenyeji wetu kwa mapokezi na
maandalizi mazuri ya kongamano hili ambalo nimeambiwa ni la nane. Hongereni sana.
Ndugu Washiriki,
Kama ilivyoelezwa
katika taarifa ya utangulizi na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya, Lengo Kuu la Kongamano hili ni kupata taarifa za utafiti
uliofanywa na wanahabari katika halmashauri 26 mbalimbali hapa nchini,katika
Utafiti huo kulikuwa na changamoto na mafanikio yaliyojitokeza, ni matarajio
yangu kuwa mtajadili taarifa hiyo kwa umakini na kuupatia ufumbuzi wa pamoja wa
changamoto zilizojitokeza. Aidha, ni matumaini yangu kuwa mafanikio yaliyopatikana
katika uchangiaji ngazi za halmashauri mtayapa kipaumbele na kuyatangaza. Katika kutoa habari za mafanikio kwa wananchi
ni vema tuwafahamishe juu ya hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya
kutolea huduma za afya, uimarishaji wa miundombinu, motisha zinazotolewa kwa watoa
huduma ngazi ya Halmashauri, haya ni
mambo ambayo kwa ujumla wake yatawapa moyo zaidi wananchi na watendaji kwa
kuona kuwa mambo haya yanawezekana.
Nawaombeni mjadiliane kwa uhuru na uwazi na ukizingatia kuwa watendaji
wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao wapo
pamoja nasi, watakuwa na jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali
yanayohusu uendeshaji wa Mfuko. Masuala
ya kisera yatatolewa ufafanuzi na Wawakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Ndugu Washiriki,
Ili kuhakikisha kuwa
fedha zinazochangwa na wananchi kwa
lengo la kuboresha huduma za afya nchini zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,
Serikali ilitoa muongozo wa matumizi ya fedha za uchangiaji mwaka 1997 ambao
ulielekeza kipaumbele cha fedha za uchangia kiwe ununuzi wa dawa hasa katika
ngazi ya Halmashauri. Katika kusisitiza
umuhimu wa suala hili serikali iliagiza kuwa fedha zitokanazo na Mfuko wa Afya
ya jamii (CHF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Fedha za Papo kwa Papo, Fedha
za Tele kwa Tele, ilielekezwa kuwa asilimia 67 ya fedha hizo zitumike kwa ajili
ya kununulia dawa.
Wizara yangu na
Serikali kwa ujumla tunatarajia kuwa utafiti wenu utatoa picha halisi ya hali
ilivyo katika Halmashauri zetu. Hususan, matumizi ya fedha zitokanazo na
michango ya mifuko ya jamii. Vile vile, matokeo ya utafiti huu yatatusaidia
sana kubaini kasoro na mapungufu na hata ushauri wa wananchi kuhusu namna bora
zaidi ya kuimarisha utendaji wa sekta ya afya.
Vile vile, nauagiza uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
kuwasilisha taarifa ya utafiti na majumuisho ya kongamano Wizarani kwa
utekelezaji.
Ndugu Washiriki,
Kongamano hili leo
linatimiza miaka nane ambacho ni kielelezo tosha cha umuhimu wa kuwashirikisha
wanahabari katika masuala yanayohusu sekta ya afya pamoja na shughuli mbalimbali
zinazotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Kauli Mbiu ya Kongamano ya mwaka huu inasema “Matumizi
Sahihi ya Fedha za Uchangiaji Katika Halmashauri ili kuboresha huduma katika
vituo vya matibabu”. Binafsi napenda kuupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya kwa kuona umuhimu wa kuwashirikisha wana hahari katika kufuatilia
changamoto za utoaji wa huduma zenu ili baada ya Kongamano wapate taarifa za
kina kuhusu hali ilivyo kwenye Halmashauri zetu ambapo kuna wanachama wa Mfuko
wa Afya ya Jamii.
Ndugu Washiriki,
Naomba niwakumbushe wanahabari
kupitia vyombo vyenu vya habari kuwa, mnao wajibu mkubwa kutoa elimu kwa umma
juu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), kitu ambacho kitawasaidia
wao kupata matibabu ya uhakika na kupitia michango yao itatuwezesha kununua
dawa za ziada. Naomba wanahabari msisubiri kongamano kama hili, lakini kila
mnapoona inawezekana tumieni kalamu zenu na ujuzi wenu wa kufuatilia mambo ili
muisaidie Serikali kubaini changamoto zinazowakwaza wananchi katika kujiunga na
Mifuko ya Afya ya Jamii na mifumo mingine ya uchangiaji wa huduma.
Ndugu Washiriki,
Baada ya kusema hayo machache, naomba niwashukuru tena kwa
kunikaribisha kushiriki nanyi katika kongamano hili. Hivyo natamka kuwa
Kongamano la Nane la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Wanahabari limefunguliwa
rasmi.
Comments