POLISI TARAFA WATAKIWA KUTUMIA PIKIPIKI KWA MATUMIZI YALIYOKUSUDIWA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Magesa
Stanslaus Mulongo amewataka Wakaguzi wa Polisi wa Tarafa kuzitumia
pikipiki walizokabidhiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa tena kwa hekima
kubwa na si vinginevyo.
Hayo aliyasema jana katika hafla
iliyofanyika katika uwanja wa gwaride uliopo kwenye kambi mojawapo
iliyopo mjini hapa ambapo jumla ya pikipiki 12 zilikabidhiwa kwa Wakuu
wa Polisi wa wilaya za Mkoa huu ambao walipokea kwa niaba ya Wakaguzi
hao.
Aliendelea kuwataka Wakaguzi hao
kutumia vyombo hivyo vya usafiri kwa kuwahi katika maeneo yenye matatizo
ya kiuhalifu na pia kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo
mbalimbali hali ambayo itasaidia kuzuia uhalifu.
Pia aliwaomba Watendaji wa Kata na
Tarafa kuwapokea Wakaguzi hao kwa mikono miwili ili kurahisisha
utendaji wa kazi za ulinzi katika maeneo yao.
“Wapokeeni hao wenzetu, wasaidieni
kwani nyinyi mnajua mazingira vizuri hali ambayo itasaidia kupunguza
uhalifu”. Alisisitiza Mh. Mulongo.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus
Sabas, alisema kwamba pikipiki hizo zitawasaidia Wakaguzi hao kuwa
karibu na wananchi kwa kutembelea kwenye maeneo mbalimbali ya Tarafa
zao.
Kamanda Sabas alimalizia kwa
kusema kwamba, sababu za kutolewa kwa pikipiki hizo ni kusaidia
kupunguza uhalifu katika maeneo yao hali ambayo itasaidia jamii kukaa
kwa usalama.
Jeshi la Polisi nchini lilitoa
pikipiki hizo kwa Makamanda wa mikoa yote hapa nchini tarehe 11/01/2013
katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo huku Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam Naibu Kamishna Suleimani Kova akipokea
pikipiki hizo kwa niaba ya Makamanda hao.
Comments