RAIS KIKWETE AWEKA SAHIHI MPANGO WA UMOJA WA MATAIFA LEO


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa hafla hiyo maalumu iliyofanyika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari 24, 2013.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo Februari 24, 2013 ameungana na Wakuu wenzake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kutia saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mhe. Rais Kikwete alisema mara baada ya utiwaji saini wa Mpango huo kwamba: “Hii ni siku kubwa na ya kihistoria kwa watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jirani zake na Ukanda wote wa Maziwa Makuu. Ni siku ya kukumbukwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Afrika, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Jumuiya yote ya Kimataifa.
Watu wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu sana. Wanastahili kupumua sasa. Wanastahili kuishi maisha bora; maisha ambayo usalama wao umehakikishiwa na kuthibitishwa; maisha ambayo yatawafanya waendeshe maisha yao kwa kufanya mambo ya maana zaidi katika kuboresha maisha yao ya kila siku.
Saini tulizotia kwa Mpango huo leo ni kielelezo cha dhati na ahadi ya utekelezwaji wa yale yanayotarajiwa na watu wa Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu kwa ajili ya Amani, Usalama na Ushirikiano.
Kwa niaba ya Serikali na Watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naahidi kwamba sisi tutatekeleza kwa dhati yale yote yanayotarajiwa kwa upande wetu”, alisema.
Mpango huo umetiwa saini na viongozi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Uganda, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kongo (Brazaville), Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki-moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma, pamoja na wenyeviti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) wametia saini Mpango huo kama mashahidi na wadhamini.
Mpango huo una nia ya kuchangia juhudi ambazo zimefanywa na ICGLR na SADC katika kutafuta amani Mashariki ya Kongo na ukanda wote wa Maziwa Makuu kwa ujumla.
Mpango huo pia umetilia maanani mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya mashauriano kati ya wakuu wa nchi za ICGLR na SADCna Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mapendekezo ya mpango huo ni pamoja na kuboresha sekta ya Ulinzi na usalama, hususan jeshi la polisi, Kuimarisha mamlaka ya nchi hasa mashariki ya Kongo; na kuendeleza ajenda kuhusu maelewano, kuvumiliana na kudumisha demokrasia nchini humo.
Vile vile, nchi za Kanda zimetakiwa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi jirani, kututoa msaada wowote wa vikundi vya waasi, kuheshimu utawala na maeneo ya nchi jirani na kuimarisha mahusiano ya Kanda.
Hali kadhalika, Jumuiya ya Kimataifa imetakiwa kuisaidia DRC na Kanda yote ya Maziwa Makuu kwa ujumla katika utekelezaji wa miradi muhimu pamoja na mkataba wa Amani, Usalama na Maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aidha, Mpango huo unapendekeza kuwepo kwa chombo cha usimamizi (Oversight Mechanism) ambacho kitaundwa na viongozi wote wa nchi 11 pamoja na Umoja wa Mataifa, SADC na ICGLR.
Mwisho”
Imetolewa na:
Muhidin Issa Michuzi,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Addis Ababa,
ETHIOPIA.
24 Februari, 2013

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*