WANANCHI KUANZA KUOMBA UJUMBE MABARAZA YA KATIBA MACHI 8


Na Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa mwongozo wa jinsi ya kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba yatakayoendeshwa na Tume na kujadili rasimu ya Katiba kuanzia mwezi Juni mwaka huu na kuwataka wananchi wanaopenda kuwa wajumbe kuwasilisha majina yao kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji au Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa Sheha kwa Zanzibar kati ya tarehe 08 hadi 20 mwezi Machi mwaka huu (2013).
Kutolewa kwa mwongozo huu kunafuatia kuchapishwa kwa rasimu yake mwanzoni mwa mwezi huu ili kupokea maoni ya wadau mbalimbali kabla ya kuuboresha. Wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia na vyama vya siasa vilitoa maoni yao.
Kwa mujibu wa mwongozo huo ambao umechapishwa katika magazeti mbalimbali ya leo (Feb. 27, 2013), baada ya kuwasilisha majina yao, orodha ya majina yote itawekwa kwenye maeneo ya wazi na mbao za matangazo katika Ofisi za Vijiji au Mitaa kwa Tanzania Bara na maeneo ya wazi kwenye Shehia kwa Zanzibar kati ya tarehe 22 hadi 28 Machi mwaka huu.
“Kwa Tanzania Bara, Vikao vya Vijiji au Mitaa vya kuwachagua kwa kuwapigia kura za siri wananchi wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba vifanyike kati ya tarehe 30 Machi 2013 hadi 03 Aprili, 2013,” inasomeka sehemu ya 7 ya mwongozo huo ambao pia unapatikana katika tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz).
Kwa upande wa Tanzania Bara, mwongozo huo unaongeza, kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata cha kuwachagua wajumbe wanne kutoka miongoni mwa Wananchi waliopigiwa kura na Mikutano Mikuu ya Vijiji au Mitaa kitafanyika kati ya tarehe 05 mwezi Aprili 2013 hadi 09 Aprili mwaka huu (2013).
“Kwa Tanzania Bara, majina ya Wajumbe wanne waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika kati ya tarehe 13 Aprili, 2013 hadi 17 Aprili, 2013,” imeongeza sehemu ya mwongozo huo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mwongozo huo, mchakato huo wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kwa mkoa wa Dar es Salaam umepangiwa tarehe tofauti.
“Kwa mkoa wa Dar es Salaam, Vikao vya Mitaa vya kuwapigia kura ya kuwapendekeza wajumbe wanane wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike kati ya tarehe 30 Machi, 2013 hadi 03 Aprili, 2013,” inasomeka sehemu ya mwongozo huo na kuongeza:
“Vikao Maalum vya Kamati za Maendeleo za Kata vya kuwachagua wajumbe wanane kutoka miongoni mwa wananchi waliopigiwa kura na Mikutano Mikuu ya Mitaa vifanyike kati ya tarehe 05 Aprili, 2013 hadi 09 Aprili, 2013,” imefafanua Tume katika mwongozo wake.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, Majina ya Wajumbe wanane waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, yatapaswa kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika kati ya tarehe 13 Aprili 2013 hadi 17 Aprili, 2013.
 Kuhusu Zanzibar
Kuhusu Zanzibar, Tume kupitia mwongozo wake, imeagiza kuwa Vikao vya Shehia vya kuwachagua kwa kuwapigia kura za siri Wananchi watatu kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike kati ya tarehe 30 mwezi ujao (Machi, 2013) hadi mwezi tarehe 03 Aprili mwaka huu (2013). 
“Majina ya Wajumbe watatu, waliochaguliwa na Mikutano ya Shehia, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri ya Mji au Wilaya ilipo Shehia hiyo kati ya tarehe 13 Aprili 2013 hadi 17 Aprili, 2013,” imesema Tume kupitia mwongozo huo na kufafanua zaidi:
“Majina ya watu wote waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, pamoja na majina ya Madiwani wote wa Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika yawasilishwe kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kutumia Fomu maalum iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa madhumuni hayo kwa njia ya nakala tete (soft Copy) na nakala mango (hard copy) kati ya tarehe 25 Aprili 2013 hadi 30 Aprili, 2013,” imefafanua Tume.
Mabaraza ya Katiba yatakayoundwa kwa mujibu wa mwongozo huo yataendeshwa katika kila wilaya na halmashauri ya Mji na Manispaa kuanzia mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu. Katika mikutano hiyo ya mabaraza, Tume itawasilisha rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja zitakazojitokeza. Baada ya mikutano ya Mabaraza ya Katiba, Tume itawasilisha rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*