JK ASAMEHE ZAIDI YA WAFUNGWA 4000

Rais Jakaya Kikwete akikagua gwaride la heshima wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano yaliyofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam

 Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya Watanzania katika maadhimisho ya miaka 49 ya muungano yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na baadaye kusamehe wafungwa 4,180.
Idadi kubwa ya watanzania walishiriki katika maadhimisho hayo hayo ambayo yalianza saa 2:30 asubuhi na kupambwa na gwaride rasmi lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na kupendezeshwa na halaiki ya wanafunzi 2,695 kutoka Tanzania Bara na Visiwani waliofanya maonyesho mbalimbali ya kuashiria maadhimisho ya muungano.
Viongozi mbalimbali wakiwamo wastaafu kutoka Tanzania Bara na Visiwani walishiriki kwenye maadhimisho hayo ikiwa ni ishara ya kuuenzi na kuulinda muungano huo.
Viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilali, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad na Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd.
Wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Baada ya viongozi kuketi katika nafasi zao, gwaride rasmi lenye gadi kumi lilipita na kutoa heshima zao mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya hapo vijana wa halaiki walionyesha maumbo mbalimbali kuashiria maendeleo yaliyopatikana nchini kwa muda wa miaka 49 tokea taifa la Tanzania liundwe rasmi kabla ya Wanahalaiki kujipanga na kuonyesha taswira mbalimbali na kuimba wimbo wa kuhamasisha kudumisha muungano.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa upinzani hawakuweza kushiriki kwenye maonyesho hayo.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa shughuli za maadhimisho hayo, mjumbe wa Kamati Kuu Chadema ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema kuwa, Watanzania wanapaswa kujivunia Muungano walionao kwa sababu umedumu kwa miaka 49, akieleza kuwa ni nadra sana kuona nchi za Afrika au Ulaya kuendeleza muungano wenye umri mkubwa kama huu wa Tanganyika na Zanzibar, hivyo basi wanapaswa kuuenzi na kuulinda kuendeleza amani iliyopo.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,180 waliokuwa wakitumikia vifungo vyao katika magereza mbalimbali hapa nchini katika kuadhimisha miaka 49 ya muungano.
Wafungwa waliosamehewa ni wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano, ambapo mpaka siku ya msamaha yaani April 26, watakuwa wameshatumikia robo ya vifungo vyao, wafungwa wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na kansa ambao wamethibitishwa na jopo la madaktari.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.