KATIBU MKUU EAC KUWA MGENI RASMI SIKU VYOMBO VYA HABARI DUNIANI



Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Dk. Richard Sezibera, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya vyombo vya habari duniani, ambapo kwa Afrika Mashariki, yatafanyika Arusha.

Maadhimisho hayo ya siku tatu, moja ya mada zinazotarajiwa kujadiliwa ni kutafuta usalama wa waandishi wa habari ukanda huo, baada ya siku za karibuni kuwepo hali tete ya mazingira ya kufanyia kazi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi hayo, Tumaini Mwailenge, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa) Tanzania, amesema maadhimisho hayo yatafanyika Mei 3 hadi 5 mwaka huu.

Aliyasema hayo leo Dar es Salaam wakati wa mkutano baina ya kamati ya maandalizi hayo na wanahabari ambapo aliongeza kuwa mada nyingine itakayojadiliwa katika maadhimisho hayo ni pamoja kuhamasisha wamiliki wa vyombo vya habari kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi sanjari na kuwalipa mishahara kwa wakati.

Alifafanua kuwa hayo yametokana na  kuwepo na matukio kadhaa ya vitisho ikiwemo Septemba 2  mwaka jana kuuawa kwa mwanahabari Daudi Mwangosi na mapema mwaka huu kuuawa kwa mwandishi mwingine, Issa Mbumba mkoani Kigoma katika mazingira ya utata.

Hali kadhalika kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa kung'olewa meno, jicho na kucha Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006, Absalom Kibanda ambapo yanadaiwa kufanywa na Watanzania wenyewe.

Alitanabaisha kuwa pia kutazinduliwa mfuko maalumu wa kuwasaidia wanahabari punde watakapokuwa wakikutwa na maafa utakaoitwa Mwangosi Fund.

Mwailenge aliongeza pia siku hiyo mke wa Mwangosi atapewa kiasi cha fedha ambazo zitamsaidia kuanzisha biashara sanjari na uzinduzi wa machapisho ya Misa.

"Majadiliano mazito siku hiyo yatahusu haki na uhuru wa vyombo vya habari,"alisema Mwailenge.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfuko wa Vyombo vya  Habari Tanzania (TMF), Ernest Sungura, alisema uhuru wa vyombo vya habari bila umoja ni kazi bure, lakini alisifu umoja ulioanza kuonekana sasa hasa wakati wa maandalizi ya siku hiyo muhimu vya wanahabari.

Hata hivyo alikiri kuwepo hali tete kwa wanahabari nchini hasa za uchunguzi.

Alisema TMF haina maana kuwepo nchini iwapo mazingira ya kufanyia kazi si salama sanjari na wanahabari kufanya kazi katika mazingira ya kutolipwa mishahara yao kwa wakati.

Alisema maadhimisho hayo yatasaidia mapambazuko kwa wanahabari katika mazingira yao ya kufanyia kazi na malipo yao kutokana na wamiliki wa vyombo vya habari nao kushiriki katika siku hiyo.

Meneja Maadili na Upatanishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Allan Lawa, alitoa mwito kwa wanahabari kutoa taarifa kwa baraza hilo iwapo watakumbana na matukio ya uvunjifu wa haki zao.

Alisema taarifa za manyanyaso zinazotolewa na wanahabari zitasaidia kupatikana takwimu za matukio hayo na hivyo kuyatafutia ufumbuzi.

Pia alitoa mwito kwa wadau ambao walitakiwa kusaini Azimio la Dar es Salaam wafanye hivyo kabla ya kwenda Arusha.

Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi, Deus Kibamba alisema kituo hicho kinaona wanahabari ni askari wa kulinda na kupigania haki za watu.

Kibamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Kataba (Jukata), alisema wao hawajaanza sasa kupigania mambo ya wanahabari  pia sheria ya haki ya kupata habari  ambayo haiwahusu wanahabari pekee.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT),  Henry Muhanika, alisema usalama unawahusu wanahabari na wamiliki pia.

Alisema wao wapo katika mkakati wa kuandaa mazingira mazuri ya kufanyia kazi wanahabari nchini sanjari na maslahi yao.


   


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.