LEMA AKAMATWA NA POLISI USIKU WA MANANE NYUMBANI KWAKE


Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) akiwa Kituo cha Polisi hivi karibun.

Arusha. Maofisa wa Jeshi la Polisi, waliokuwa na mbwa, mabomu ya machozi na silaha nyingine za moto, usiku wa kuamkia jana waliruka ukuta na kuingia katika eneo la makazi ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambako walizingira nyumba yake kwa zaidi ya saa nne.
Operesheni ya kutiwa mbaroni Lema iliogozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Gillel Muroto ambaye alifuatana na askari zaidi ya 25 waliokuwa na silaha hizo.
Walifika nyumbani kwa Lema saa 5:00 usiku lakini walilazimika kusubiri hadi saa 9:10 walipomkamata Mbunge huyo baada ya yeye mwenyewe kujisalimisha. Habari zinasema Lema aliyekuwa akihojiwa na polisi hadi jana jioni, alinyimwa dhamana kwa maelezo kwamba “anaweza kuhatarisha amani”.
Mashuhuda waliokuwa karibu na anakoishi Lema, eneo la Njiro Mwisho wa Lami, walisema polisi hao walifika wakiwa kwenye magari manne na kwamba ili kuchunguza ndani ya uzio wa nyumba yake, walipanda juu ya mabega ya wenzao huku wakielekeza mitutu ya bunduki tayari kukabiliana na lolote ambalo lingejitokeza.
Baada ya kuchungulia baadhi yao walitumbukia ndani ya uzio na kwenda kusimama mbele ya milango na madirisha ya nyumba ya Lema na huku nyuma wengine walipanda tena kwenye mabega ya wenzao kuendelea kuweka ulinzi kwa walioingia ndani.
Askari hao wanadaiwa kwamba waliwataka walinzi wa nyumba hiyo iliyopo karibu na Chuo cha Ufundi Veta, kuwafungulia mlango, lakini walinzi hao walikataa hivyo kuzua mabishano makali.
Kutokana na mabishano hayo, Lema aliyekuwa ndani amelala alishtuka na kuanza kufuatilia na kubaini kuwapo kwa polisi nje ya nyumba yake hiyo. Mke wa Lema, Neema alimpigia simu Katibu wa Wilaya wa Chadema, Aman Golugwa kumwarifu kuhusu uwepo wa watu walioruka ukuta.
Golugwa jana alithibitisha kupokea simu ya mke wa Lema na kwamba alipopata taarifa hizo alimwarifu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Arusha, Camillius Wambura ambaye baadaye alimuahidi kwamba angefuatilia suala hilo.
“Baadaye alithibitisha kuwapo kwa polisi waliotumwa kwa ajili ya kumkamata Lema lakini akasema amewapa maelekezo ya kufuata taratibu za kawaida,”alisema Golugwa na kuongeza:“Baada ya hapo, wale askari waliokuwa wameruka ukuta walitoka nje ya uzio”.
Habari zinasema wakati baadhi ya askari wanaruka ukuta, wengine walibaki nje wakizingira uzio wa nyumba ya Lema huku wakiwazuia viongozi wa Chadema waliokuwa eneo hilo kusogea.
Kukamatwa kwa Lema katika mtindo wa aina yake kumefanywa saa chache tangu alipotoa kauli ya kukataa kujisalimisha polisi, kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo. Mulongo aliagiza Lema akamatwe kwa tuhuma kwamba alichochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Katika vurugu hizo, wanafunzi hao walimzomea Mulongo na kurushia mawe msafara wake wakati alipokwenda kusikiliza malalamiko yao yaliyotokana na kuuawa kwa mwanafunzi mwenzao, Henry Kago (22) ambaye alichomwa kisu na watu wasiofahamika wakati anatoka kujisomea saa 4:00 usiku.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA