TAMKO LA SERIKALI KUHUSU UHAMAJI KUTOKA MFUMO WA UTANGAZAJI WA ANALOJIA KWENDA DIJITALI



Mabadiliko katika mfumo wa utangazaji kutoka mfumo wa analojia kwenda katika mfumo wa dijitali ni utaratibu ambao unaendelea ulimwenguni kote. Mabadiliko haya yanatokana na makubaliano ya nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa lenye dhamana ya masuala ya mawasiliano yaani International Telecommucations Union yaliyofanyika mwaka 2005 huko Geneva, Uswisi. Makubaliano ya nchi wanachama ni kuzima kabisa matangazo katika mfumo wa analojia na kutumia mfumo wa utangazaji wa dijitali ifikapo tarehe 17 Juni 2015.

Ili kuhakikisha mabadiliko haya yanafanyika kwa ufanisi, tija na pia kutoa muda wa kutosha wa kutekeleza mabadiliko haya, mwaka 2005 Serikali ilianza mchakato wa uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda dijitali ambao ulihusisha wadau wote, wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari na vituo vya utangazaji wa televisheni, hatua kwa hatua, hadi kuridhia ratiba nzima ya uzimaji wa mitambo ya analojia. Kwa kifupi mchakato wa uhamaji ulipitia hatua zifuatazo:
Mwaka 2005:   Waraka wa kwanza wa mashauriano (consultative document) kuhusu umuhimu na faida za kuhama kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda dijitali ulitayarishwa na kusambazwa kwa wadau wote;
Mwaka 2006:   Waraka wa pili wa mashauriano na mapendekezo ya muundo wa leseni kwenye mfumo wa utangazaji wa teknolojia ya dijitali ulitayarishwa na kusambazwa kwa wadau wote;
Mwaka 2007:   Kamati ya kiufundi inayoshughulikia uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda dijitali iliundwa;
Mwaka 2007:   Mkutano mkuu uliojumuisha vituo vyote vya utangazaji nchini ulifanyika Bagamoyo kupitisha maazimio ya mfumo wa leseni za utangazaji utakaotumika kwenye mfumo wa dijitali;
Mwaka 2010:   Kampuni tatu (3) zilipewa leseni za ujenzi wa miundombinu ya utangazaji ya dijitali. Kampuni tatu zilizopewa leseni za kusambaza matangazo ya dijitali ni Agape Associates Limited, Basic Transmission Limited, na Star Media (T) Limited. Kampuni hizo zilipewa leseni baada ya kuthibitisha kuwa zina uwezo wa kujenga miundombinu ya kurushia matangazo katika mfumo wa dijitali;
Mwaka 2010:   Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mabadiliko ya Utangazaji toka mfumo wa analojia kwenda dijitali iliundwa. Kamati hii hukutana kila baada ya miezi mitatu kutathmini maendeleo ya ubadilishaji wa mfumo wa utangazaji;
Mwaka 2011:   Kampeni ya Kitaifa ya kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya mfumo wa utangazaji ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya urushaji wa matangazo katika mfumo wa dijitali unaendana na ratiba ya uhamiaji katika mfumo wa matangazo kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali, taarifa za mara kwa mara zimekuwa zikiletwa na wajenzi wa miundombinu hiyo katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na kujadiliwa na Kamati mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uhamaji katika mfumo wa utangazaji wa dijitali. Taarifa hizo zimekuwa zikionyesha kuwa ujenzi wa miundombinu unaendelea vizuri na kwamba ratiba ya uzimaji wa mitambo ya analojia nchini itakwenda kama ilivyokubalika na wadau wa utangazaji.
Kufuatia uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya mfumo wa utangazaji kutoka katika mfumo wa analojia na kwenda katika mfumo wa dijitali uliofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali, kwa kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, iliandaa Mkakati Maalum wa Mawasiliano ambao ulilenga katika kuhamasisha wananchi kuhusu uhamaji katika mfumo wa utangazaji wa dijitali. Njia mbalimbali zimetumika katika kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya mfumo wa utangazaji ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara sehemu mbalimbali, kutoa vipeperushi na matangazo katika magazeti, redio na televisheni, kufanya majadiliano katika televisheni na redio ambayo yalihusisha pia maswali kutoka kwa wadau mbalimbali, kuweka taarifa katika tovuti kuhusu masuala mbalimbali ya uhamaji katika mfumo wa utangazaji.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa uhamasishaji na elimu kwa umma imetolewa kwa kiasi kikubwa na wananchi wamehamasika sana katika kuingia katika mfumo wa utangazaji wa dijitali kutoka ule wa analojia. Hii ni kutokana na wananchi wengi kujitokeza kununua vingamuzi (visimbuzi) kwa wingi katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ambayo matangazo katika mfumo wa analojia yalitarajiwa kuzimwa. Aidha, hapakuwa na mapendekezo yoyote kutoka kwa wajenzi wa miundombinu ya urushaji wa matangazo ya dijitali kuwa watashindwa kujenga miundombinu hiyo kwa wakati ifikapo tarehe 31 Desemba 2012, siku ambayo ilikuwa imekubalika kuzima mitambo ya utangazaji ya mfumo wa analojia na kuanza kutumia mfumo wa dijitali. Tarehe 31 Desemba 2012, Serikali ilianza kuzima matangazo hayo kwa awamu ili kubaini na kushughulikia changamoto mbalimbali ambazo zingeweza kujitokeza katika mabadiliko hayo.
Uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa analojia kwenda katika mfumo wa utangazaji wa dijitali ilianza kutekelezwa tarehe 31 Desemba 2012 kwa kuzima mitambo 14 ya televisheni inayotumia utangazaji wa mfumo wa analojia katika jiji la Dar es Salaam ambapo wananchi wengi walinunua vingamuzi ili waweze kujiunga na mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali. Kadhalika, uzimaji wa mitambo ya analojia kwenye miji ya Dodoma na Tanga ulifanyika tarehe 31 Januari 2013. Uzimaji wa mitambo ya analojia kwa jiji la Mwanza ulifanyika tarehe 28 Februari 2013. Uzimaji wa mitambo kwa miji ya Arusha na Moshi umefanywa tarehe 31 Machi 2013. Kwa ujumla wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kujiunga na mfumo huu mpya wa utangazaji na hakuna matatizo yaliyojitokeza zaidi ya changamoto kadhaa ambazo zimeendelea kupatiwa ufumbuzi.
Ikumbukwe kuwa uzimaji wa urushaji wa matangazo katika mfumo wa analojia na kuanza kutumika kwa mfumo wa dijitali umefanywa mahali ambapo kuna mawimbi (signal) ya televisheni ya dijitali tu. Pale ambapo hakuna mawimbi ya televisheni ya dijitali, matangazo ya televisheni yameendelea kurushwa katika mfumo wa analojia hadi wakati ambapo mawimbi ya televisheni ya dijitali yatakapofikia mahali hapo. Hivyo, kwa mfano katika Jiji la Mwanza ambapo urushaji wa matangazo katika mfumo wa dijitali ulisitishwa tarehe 28 Februari 2013, maeneo yaliyoguswa na usitishaji wa matangazo hayo ni Mwanza City, Sengerema, Ukerewe na Kisesa. Sehemu nyingine zote za Mkoa wa Mwanza bado zinaendelea kupokea matangazo ya televisheni katika mfumo uliokuwepo hapo awali. Vivyo hivyo, uzimaji wa matangazo katika Jiji la Tanga umegusa maeneo ya Jiji la Tanga, Muheza, Mkanyageni, Nguvu Mali, Mabokweni na Mkinga. Maeneo mengine kama vile Lushoto, Korogwe, Handeni yanaendelea kupokea matangazo katika mfumo uliokuwa unatumika hapo awali. Hivyo, katika maeneo ambayo hakuna uzimaji wa mitambo ya analojia umefanywa, wananchi wanaendelea kupata matangazo ya televisheni kwa kutumia mfumo uliokuwepo hapo awali.
Serikali inapenda kuwakumbusha wananchi kuwa katika maeneo ambayo tayari kuna matanagzo ya televisheni katika mfumo wa dijitali, watumiaji wa televisheni wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanapata matangazo ya televisheni zote zenye leseni za kitaifa bila gharama yoyote ile ya ziada mbali na gharama ya kununua kingamuzi (kisimbuzi) ambacho kinawezesha kuona matangazo katika mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali. Stesheni hizo ni TBC1, ITV, Star TV, Channel 10, na East African TV. Endapo matangazo ya televisheni ya vituo hivyo hayapatikani, wananchi wawasiliane mara moja na wato huduma za vingamuzi ili kuwasaidia kupatia ufumbuzi.
Serikali inatumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza wananchi kwa kuitikia vyema wito wa kuhamia katika mfumo wa utangazaji wa dijitali katika maeneo yote yaliyohusika na uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa analojia. Aidha, Serikali inavishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha umma kuhusu mabadiliko haya ya mfumo wa utangazaji. Serikali itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kwa kutumia njia mbalimbali, ili Tanzania iwe imekamilisha uhamiaji katika mfumo mpya wa utangazaji kabla ya tarehe 17 Juni 2015.
Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, Serikali imeshuhudia kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari na hasa wa utangazaji kupitia vyombo vya habari wanavyovimiliki, wakiilaumu na kuishutumu Serikali kuhusu uamuzi halali wa Serikali wa kuhamia katika mfumo wa dijitali. Kauli hizo zilizotolewa kwa nguvu kupitia mikutano ya waandishi wa habari na pia kuhusisha mijadala katika baadhi ya redio na televisheni zina nia ya kufifisha mchakato wa uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa dijitali.
Kauli hizi sio za kweli, zinapotosha ukweli na hali halisi na pia zinalenga kuchochea wananchi kutokubaliana na maamuzi haya ya Serikali na pia kutounga mkono juhudi za Serikali ilizokwishafanya katika kutekeleza azma ya uhamaji kutoka utangazaji wa mfumo wa analojia kwenda dijitali. Kauli hizo si tu zimewachanganya wananchi wanaoendelea kuhamia katika mfumo mpya utangazaji wa dijitali, bali pia zimetia hofu vyombo vya fedha ambavyo vimekuwa vikitoa mikopo kwa wajenzi wa miundombinu ya urushaji wa matangazo katika mfumo wa dijitali. Madhara ya kauli hizo ni kuwapotosha wananchi kuhusu suala zima la uhamiaji katika mfumo wa utangazaji wa dijitali na pia kukwamisha juhudi za Serikali kuhakikisha zoezi la kuhamia dijitali linafanikiwa kabla ya kufikia ukomo wa matangazo ya analojia tarehe 17 Juni 2015.
Serikali inapenda kuwafahamisha wananchi kwa mara nyingine tena, Serikali ilifikia maamuzi ya kuhamia dijitali kwa kuzingatia maslahi ya taifa wananchi msikubali kupotoshwa kwa ajili ya maslahi binafsi. Upotoshaji huu unaweza kusababisha wananchi kukosa taarifa muhimu ikiwa ni pamoja na kupata taarifa mbalimbali za maendeleo au matukio ya ndani na nje ya nchi; kufuatilia mijadala bungeni na pia kufuatilia mchakato wa kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, upotoshaji unaofanywa unaweza kusababisha hasara kubwa kwa wananchi ambao wataendelea kununua televisheni zinazotumia mfumo wa analojia. Vile vile, upotoshaji huo utachelewesha wananchi kutumia huduma nyingine nyingi zinazoendana na teknolojia ya utangazaji ya dijitali ikiwa ni pamoja na huduma za Intaneti, huduma za kifedha, ununuzi wa vitu kwa njia ya mtandao na kupata chaneli nyingine za ziada.
Baadhi ya wamiliki hao wa vyombo vya habari wanatambua wazi kuwa walikuwa na fursa kwa zaidi ya miaka 7 kuwasilisha maoni au malalamiko yao kwa vyombo husika ili kama kuna changamoto katika uhamiaji huo ziweze kufanyiwa kazi, badala ya kutumia muda mwingi wa matangazo katika vyombo vyao vya habari kupotosha umma kuhusu dhana nzima na mchakato wa uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda dijitali. Kwa kuwa upotoshaji huu unaongozwa na wamiliki wa vyombo vya habari ambavyo kwa namna moja au nyingine vinahusika na ujenzi wa miundombinu ya urushaji wa matangazo katika mfumo wa dijitali, Serikali iko tayari kushirikiana na wadau hao katika kutatua changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa uhamiaji katika mfumo wa utangazaji unaendelea kama ilivyopangwa badala ya kutumia muda mwingi kuupotosha umma.
Ikumbukwe kuwa mabadiliko haya hayaepukiki, hivyo basi wadau wote kwa pamoja hawana budi kushirikiana katika mchakato mzima kama ilivyokubalika kupitia vikao mbalimbali vilivyofanyika toka mwaka 2005 vikishirikisha wadau wote wa Sekta ya Utangazaji, wakiwemo wamiliki wote wa vyombo vya habari vya utangazaji wa televisheni nchini. Serikali imejiridhisha kuwa mchakato wote wa kuelekea mfumo wa utangazaji ulifanywa kwa umakini mkubwa na kwa muda wa kutosha, elimu imetolewa na inaendelea kutolewa. Aidha, ni dhahiri kuwa watoa huduma za miundombinu ya dijitali waliopewa leseni tangu 2010 wameendelea na wajibu wa kuweka mitambo ya dijitali sehemu mbalimbali nchini na zoezi linaendelea vizuri.
Serikali haitavumilia kikundi au mtu yeyote atakayeonekana kupotosha au kufifisha mchakato wa kuhamia katika mfumo wa utangazaji wa dijitali. Aidha, Serikali inaiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuendelea na utaratibu, ratiba ya zoezi zima la uzimaji wa mitambo ya analojia kama ilivyotolewa na Serikali. Vile vile, Serikali inaiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kupitia Kamati ya Maudhui kuchunguza endapo kauli zilizotolewa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari kwa kutumia muda mrefu kuelezea kauli zao katika vyombo vyao vya habari kama hawakukiuka sheria na kanuni za Utangazaji kwa nia ya kupotosha umma kwa kusudio la kudhoofisha maamuzi haya ya Serikali.
Pamoja na tathmini ya awali ambayo Serikali, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imefanya na kuonyesha kuwa mchakato wa uhamaji unaendelea vizuri, Serikali itafanya tathmini ya kina baada ya kumaliza awamu ya kwanza ya uzimaji wa mitambo ya kurushia matangazo ya analojia kwenye miji 7 ambayo kwa sasa inapata matangazo kupitia mfumo wa utangazaji wa dijitali. Tathmini hiyo itaendana na kufanya mkutano wa wadau wote wa utangazaji nchini ili kuweza kupata maoni yao kabla ya kuanza awamu ya pili ya uzimaji kwenye miji 14 ambayo itapata huduma za matangazo ya dijitali hivi karibuni.
Serikali inaomba wananchi kupuuza upotoshaji unafanywa kuhusu ukweli wa mabadiliko ya mfumo wa utangazaji wa kutoka analojia kwenda dijitali. Aidha, tunaomba vyombo vya habari kuendelea kutoa ushirikiano na kuendelea kuunga mkono juhudi hizi muhimu kwa kuelimisha umma kuhusu ukweli katika mchakato wa uhamiaji katika mfumo wa utangazji wa dijitali. Serikali itaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau ili kuhakikisha kuwa uhamiaji unakamilika mapema kabla ya ukomo wa matangazo ya analojia tarehe 17 Juni 2015.
Imetolewa na:
Prof. Makame M. Mbarawa (Mb.)
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI