Wagonjwa 316 wapata huduma za madaktari bingwa

 Daktari Bingwa wa akina Mama Dk. Mrema (wa pili kutoka kulia) akimsikiliza kwa makini mmoja wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo kwa lengo la kutoa ushauri wa tiba sahihi.
  Wagonjwa wakisubiri kuonana na Daktari Bingwa wa magonjwa ya Kawaida..
 Wauguzi katika Hospitali ya Maweni wakitoa namba kwa wagonjwa waliojitokeza kuonana na madaktari bingwa wa Hospitali ya Muhimbili.
 Wagonjwa wakisubiri kuonana na daktari bingwa wa upasuaji.
 Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee na timu ya madaktari bingwa katbla ya kuanza kazi rasmi.

Na Grace Michael, Kigoma
JUMLA ya wagonjwa 316 ndani ya siku mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Maweni mkoani Kigoma wamefanikiwa kuonana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao wapo mkoani humo kwa mpango unaoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mbali na wagonjwa hao kuonana na madaktari hao, jumla ya wagonjwa 11 ndani ya muda huo nao wamefanikiwa kufanyiwa upasuaji na madaktari hao hali inayoonesha kuwepo uhitaji mkubwa wa madaktari katika mikoa ya pembezoni ambayo miundombinu yake bado haijaimarika.
Hayo yanafanyika katika Mkoa wa Kigoma ndani ya mpango wa NHIF ambao ulizinduliwa mapema Aprili mwaka huu mkoani Lindi ambako nako timu ya madaktari bingwa watatu waliweka kambi katika Hospitali ya Mkoa na kufanikiwa kutoa huduma kwa mamia ya wananchi.
Katika Hospitali ya Maweni, timu ya madaktari wanne kutoka Muhimbili ilianza kazi rasmi jana (Jumatatu) na itakaa hospitalini hapo kwa muda wa siku saba lengo ni kutumia wataalam hao kitaifa.
Wagonjwa wanaonufaika na mpango huu ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na wananchi kwa ujumla ambao wanapata huduma kupitia utaratibu wa kawaida.
Wagonjwa waliofanikiwa kujiandikisha kwa lengo la kupata huduma kutoka kwa wataalam hao ni kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Kigoma ambapo wanaeleza kuwa ni fursa ya kipekee kuipata.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wagonjwa ambao wamepata huduma ambao walifikishwa hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya waliushukuru Mfuko kwa kuanzisha mpango huo ambao moja kwa moja unawagusa wananchi hasa wa kipato cha chini.
Kwa upande wa watumishi hospitalini hapo, wanasema kuwa wataitumia fursa hii vyema hasa katika kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa madaktari hao bingwa ili waweze kuboresha huduma zao kwa wagonjwa hata watakapobaki wenyewe.
Idadi ya wagonjwa inazidi kuongezeka kila kukicha hatua inayowalazimu madaktari hao kufanya kazi kwa zaidi ya saa 15 bila ya kupumzika.
Akizungumzia mwitikio huo, Naibu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Hamis Mdee, alisema kuwa mwitikio huo ni faraja kwa Mfuko ambao lengo lake ni kutoa huduma kwa Watanzania na kuhakikisha afya zao zinaimarika.
“Sisi kama Mfuko tunaona faraja sana tunapoona wagonjwa wamefika hapa na kupata huduma hizi ambazo pengine wasingeweza kuzipata hivyo tutaendelea na mpango huu kwa kuwa unagusa moja kwa moja uhai wa wanachama wetu na wananchi kwa ujumla,” alisema Mdee.
NHIF imeanzisha mpango huu na utatekelezwa katika mikoa mbalimbali ya pembezoni ikiwemo Rukwa, Katavi, Pwani, Lindi na Kigoma.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.