*Wakulima
waorodhesha madhambi ya kiwanda
*Wamhusisha
Mkapa kukimiliki, Kinana ataka suluhu
Na Mwandishi Wetu, Mvomero
WANANCHI
wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro
wamekishtaki Kiwanda cha Sukari Mtibwa kuwa kimekuwa kikifanya dhuluma kubwa
zidi ya wakulima wa miwa huku wakimuomba Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM), kufanya kila analoweza kuhakikisha mgogoro uliopo kati ya pande
hizo mbili unapatiwa ufumbuzi.
Pia
wamesema kwa hali iliyofikia imefanya wananchi wa Wilaya ya Mvemero kutokuwa na
imani na Serikali na katika hilo wanaomba pia CCM kufanya kila linalowezekana
kutafuta ufumbuzi ili wananchi hao warudishe matumani kwa chama hicho ambacho
bado kinakubalika kwa Watanzania wengi.
Wakati
hayo yakiendelea, uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa umeweka wazi kuwa
kinatambua baadhi ya changamoto zilizopo baina yao na wakulima na kwamba sasa
ni wakati wa kutafuta ufumbuzi wake na kuanza ukurasa mpya lakini pia wakaomba
CCM kuiomba Serikali kuangalia wawekezaji wa ndani kwani kuna sukari
inayotokana nje na kufanya wakose fedha.
Wakizungumza
wilayani hapa jana wakulima wa miwa na wawakilishi wao walimambia Kinana
aliyeambatana na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho akiwemo Katibu wa
Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, walisema mgogoro umedumu kwa miaka 10 lakini kwa
bahati mbaya hakuna majibu ya suluhu hali inayofanya wananchi wajiulize maswali
bila majibu.
Walisema
kuwa yapo mambo mengi ambayo hawafuri kuona yakifanywa na wawekezaji wa kiwanda
hicho kwani badala ya kuwa na manufaa kwao sasa kimekuwa mateso ambayo sasa
yanahitaji ufumbuzi wa kudumu.
Walitaja
baadhi ya matatizo makubwa yanayofanywa na kiwanda cha Mtibwa ni kucheleweshwa
kwa malipo ya miwa, kiwango kidogo cha malipo pindi wanapopeleka mazao yao
kuuza kiwandani, madeni sugu kwa wasataafu wa kiwanda lakini kubwa zaidi wanadai
kuna dhuluma ambayo imekuwa ikifanywa na uongozi wa kiwanda hicho.
Akizungumza
wakati akieleza matatizo wanayokumbana nao wakulima wa miwa, mmoja wa
wawakilishi wa wakulima hao, Alfan Mbila alisema wakulima wamekata taa kutokana
na vitendo vinavyofanywa na kiwanda hicho.
“Wakulima
hawalipwi kwa wakati, wastaafu nao hawalipwi mafao yao na hata wakienda
mahakamani wanashangaa wanashindwa kesi na mwekezaji kuibuka mshindi hata
katika kesi zao za msingi za madai.
“Tumefika
mahali sasa wakulima tunajiuliza maswali mengi, hivi kiwanda hiki ni cha
nani?Maana haiwezekani uongozi wa kiwanda cha Mtibwa kuwa na nguvu kubwa kuliko
Serikali.Umekuja Kinana na Nape tunaamini hili mtalimaliza na kupata ufumbuzi
wa kudumu.Tumechoka na inafaka mahali tunaona ni bora tukapewa kibali tuanze
kiwanda chetu cha kusindika miwa ili tuachane na Mtibwa,”alisema.
Wananchi
hao ambao waliamua kutumia mkutano huo kukishtaki kiwanda hicho na kukitaka
chama hicho kuchukua hatua zaidi walikwenda mbali na kudai huenda kata ya
Turiani imekwenda upinzani kwasababu ya wananchi kutofurahishwa na mwenendo na
matendo ya kiwanda hicho na matokeo yake
kuichukia Serikali.
Mkulima
mwingine Ramadhan Mhuta alisema kuwa matatizo mengine kati yao na kiwanda cha
Mtibwa yalianza tangu mwaka 1998 baada ya kupewa kiwanda hicho kutoka kwa
Serikali na tangu wakati huo yameibuka mambo mengi ambayo yamefanya mgogoro
kuwa mkubwa na kuonekana kama umekosa ufumbuzi wake.
“Tunaomba
Kinana hili uchukue kama changamoto ambayo inahitaji majibu yatakayomaliza
tofauti zilizopo.Imefika mahali wananchi wanachukua wawekezaji hao.Wapo wengine
wanaamini kiwanda hiki ni mali ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.Hivyo pamoja na
majibu mtakayotoa, tunataka kufahamu hiki kiwanda ni mali ya nani?Alihoji
Mhuta.
Mwakilishi wa wakulima wa kata ya Kanga,
Mohamed Hamis alisema kuwa tatizo lililopo si mwekezaji bali ni matendo yake
ambayo yanaonekana ni dhuluma dhidi ya wakulima.
Alisema
kinachotakiwa Kinana anatakiwa kutafuta ufumbuzi ambao utaondoa migogoro
iliyopo na si vinginevyo huku akiweka wazi kuwa hata Nape akiamua kuwa
mwekezaji si tatizo bali matendo yake kama hatafurahisha wananchi hilo ndilo
litakuwa tatizo.
Akijibu
baadhi ya tuhuma zilizoelekezwa dhidi ya kiwanda hicho, Mwakilishi wa Kiwanda
cha sukari Mtibwa, Hamad Yahya Juma alisema alisema madai yaliyotolewa na
wananchi si ya kweli na kwamba wamekuwa wakijitahidi kadri wanavyoweza kutenda
haki.
Aliongeza
kuwa waatambua kuna baadhi ya changamoto zilizopo zikiwemo za kutolipa baadhi
ya michango ya PFF lakini kwani wakati
lakini kwa ujumla wanalipa.
Kuhusu
madai ya wastaafu kutolipwa, alisema Mtibwa haidai na wastaafu ila kinachotokea
kuna madeni ya kurithi ambayo yalitokana na Serikali huko nyuma kutolipa lakini
kwa uungwana wa kiwanda chao uliamua kurithi deni na kwa kiwango kikubwa
wamefanikiwa kulipa.
Akizungumzia
suala la dhulma wakati wa uvunaji miwa shambani, alisema hiyo si kweli kwani ni
miaka mitatu sasa miwa inavunwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya
ushirika, inapofika mahali wakulima wanatoa lawama kwa kiwanda si kutenda haki
na katika hilo aliwataka wawe wakweli mbele ya Kinana.
Wakati
hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mvomero , Jonas Van
Zeland alitumia nafasi hiyo kuwambia Kinana kuwa wanakidai kiwanda sh.milioni
280 ambazo zinatokana na makato ya wakulima ambazo zinatakiwa kwenda kwenye
halmashauri.
Akijibu
hoja hizo wakati akifanya majumuisho, Kinana alisema yapo mambo nane ya msingi
ambayo yametolewa na wakulima hao lakini hataki kuingia kwenye mkumbo wa ahadi
ambazo hazitekelezeki na kwa hali hiyo ameamua kukutana tena na wawakilishi wa
pande zote ili kuzungumzia kwa kina na kupata ufumbuzi wa kudumu.
“Hili
si la kutoa majibu ya haraka, nipeni muda na mimi nifahamu.Naomba wawakilishi
wa makundi yote pamoja na uongozi wa kiwanda Jumatatu tukutane Morogoro.Ziara
yangu inakwisha Jumapili lakini sitaondoka hadi tukae tuzungumze.
“Kwa
hali ilipofikia sasa, ukionekana tu unapita pita huku Mtibwa unaonekana na wewe
unahusika na kiwanda hicho.Wengine wanaamua kusingizia kiwanda hiki ni mali ya
kigogo wakati mwingine anatajwa mzee Mkapa.
“Masikini
huku ni kusingizia, lakini hayo yote yanatokana na kuwepo kwa matatizo
yaliyokosa majibu.Kama hakukuwa na matatizo wakulima wanalipwa vizuri na kila
kitu kinakwenda sawa usingesikia kiwanda kinamilikiwa na nani.Kama kuna dhuluma
ndio hayo yote yanaibuka,”alisema Kinana.
Alitoa
angalizo kuwa, CCM haishughulikii mgogoro huo kwasababu ya kutafuta kura maana
hiyo si hoja, bali inafanya hivyo kwa kuwa tumekabidhiwa dhamana na Watanzania
ya kuliongoza taifa hili na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.
“Hivyo
kinachofanyika hapa, ni kazi yetu sisi CCM kama chama tawala.Tukianza kuingiza
mambo ya kukosa au kupata kura kwa sasa hayana maana.Tukitafuta ufumbuzi wa
matatizo wananchi watapima wenyewe na si kuangalia kura zao,”alisema Kinana.
Mwisho
Comments