Abwao, Lukuvi walipuana


Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Chiku Abwao akizungumza bungeni jana alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio na matumizi Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Picha na Edwin Mjwahuzi.  

Dodoma.  
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Iringa, Chiku Abwao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi jana waligeuza Bunge kama jukwaa la kufanyia kampeni za kuwania ubunge kwa jimbo la Isimani kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Hali hiyo ilifanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia wakati Abwao akizungumza na kumtaka arudi kwenye hoja,badala ya kumshambulia Lukuvi na kupiga kampeni, lakini Mbunge huyo alishikilia kuwaalikuwa anachangia mjadala wa wizara kwa kujadili manyanyaso ya polisi dhidi ya wafuasi wake.
Akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2013/14, Abwao ndiye alianza kumshambulia Lukuvi baada ya kumtuhumu kuwa alikuwa anatumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kubambikia watu kesi.
Abwao ambaye alitumia nafasi hiyo kuwa atawania ubunge katika jimbo hilo ili kumng’oa Lukuvi, alisema kuwa wale wanaomuunga mkono wamekuwa katika kipindi kigumu jimboni humo kutokana na kunyanyaswa na polisi.
“Lukuvi amezoea kunipachika sifa kuwa mimi ni mzoefu wa kufungua baa tu, lakini ameshindwa kuzitaja sifa zangu nyingine kuwa mimi ni mwanamke wa shoka na ni tishio kwenye nafasi yake ya ubunge.
Pia alimtuhumu Lukuvi kwa kushindwa kupeleka maendeleo katika kipindi cha miaka 10 akiwa Mbunge wa Isimani.
“Jamani watu wa Isimani mnajua wenyewe mmekuwa na wabunge mawaziri kwa miaka 20, lakini maendeleo hakuna. Umeme unatoka Kidatu unapita juu ya Isimani na pia barabara ni mbovu,” aliongeza Abwao.
Naye Lukuvi hakubaki nyuma kwani aliibuka na kumjibu Abwao kuwa maneno yake ni sawa na ya `mganga njaa’ na aliwataka polisi wasishtushwe na maneno ya mbunge huyo.
“Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza, inakuwaje mbunge azungumzie mambo ya Isimani katika mjadala huu wakati watu wanazungumzia masuala ya muhimu ya Arusha,” alisema Lukuvi akimaanisha suala la kulipuliwa kwa Kanisa Katoliki huko Arusha.
“Ukiona vyaelea ujue vimeundwa, Isimani umeikuta na utaiacha, wananchi mjionee wabunge wa Iringa tupo wengi na kila mmoja anafahamu uwezo wake,” alisema Lukuvi, ambaye pia alisifia polisi na kusema wale wanaowashutumu basi wana kasoro.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU