Kinana ajibu tuhuma za Msigwa

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana  

 Dodoma. 
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema anaamini chanzo cha kuchafuliwa kwake na wapinzani ni wadhifa wake.
Akizungumza na mwandishi wetu Dodoma jana, Kinana alisema anaamini kuwa kama asingekuwa na wadhifa huo, asingesakamwa kwa tuhuma alizoziita za uzushi.
Aprili 29, mwaka huu, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alimtuhumu Kinana kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo na kudai kuwa meli iliyokuwa chini ya uwakala wa Kampuni Sharaf Shipping inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa huko Vietnam na nyara hizo za Serikali.
“Hivi vitu havinisumbui. Hapa tatizo ni kuwa Katibu Mkuu wa CCM. ‘I am a senior officer’ (Ofisa Mwandamizi) sasa katika chama changu kama ningekuwa nimekaa nyumbani nafanya biashara zangu yasingetokea haya.
“Nataka kuwaambia tu, waelewe kuwa hawawezi kunitoa katika ajenda yangu ya msingi. Hii ni sawa na mwanajeshi anayekwenda kupigana vita na adui halafu akawa na vikundi vidogo vinakushambulia kutoka kila upande kukutoa katika lengo la msingi... ni lazima mtu ukomae na ili ufanikiwe,” alisema Kinana.
Alisema Msigwa alikuwa katika Kamati ya Ardhi na Maliasili ya Bunge tangu mwaka 2010 na ukweli wa mambo hayo anaujua... “Msigwa anajua kabisa nikiwa kama ‘shipping agent’ (wakala wa meli), sihusiki na kujua kilichopo ndani ya kontena. Wale wanaopaswa kujua ni meneja wa bandari, mamlaka ya mapato, walinzi na wakala wa kupakia na kupakua mizigo, kwa kuwa wao ndiyo wanafanya ukaguzi na kuweka seal (lakiri) …siyo kazi yetu,” alisema.
Kinana aliongeza kuwa anamini kuwa CCM ni tishio kwa wapinzani ndiyo maana wameanza kumpiga madongo kwa lengo la kupambana naye. Alipoulizwa kwa nini hajachukua hatua za kisheria kama anaona amechafuliwa na kama tuhuma hizo hazina ukweli? Kinana alijibu kuwa anajua kuna njia tatu za kuchukua kuhusiana na tatizo hilo lakini bado anazifanyia kazi.
“Kwanza unaweza kujieleza kwenye vyombo vya habari. Pia unaweza kukata rufaa kwa Spika na kesi yako kusikilizwa lakini pia unaweza kwenda mahakamani. Bado natafakari cha kufanya.”
Madai ya Msigwa
Mchungaji Msigwa alisema bungeni kuwa: “Kwa bahati mbaya ni kwamba wahusika wengi ambao wanatajwa kwa ushahidi ni makada maarufu na wengine ni viongozi waandamizi wa CCM. Tumeshuhudia watuhumiwa wengine wa ujangili ambao Ikulu imediriki kuwapatia nafasi kubwa za uongozi wa taifa hili, licha ya kutajwa kwenye ripoti ya uchunguzi kuhusiana na ujangili.”
Alisema mwaka 2009, meli ya Kampuni ya Wakala wa Meli ya Sharaf Shipping inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa China ikiwa na makontena yenye nyara za Serikali ikiyasafirisha kwenda Hong Kong.
“Nyaraka zilizopo Ofisi za Wakala wa Usajili wa Kampuni na Biashara (Brela), zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Kinana ilisajiliwa Oktoba 2003 na kupewa hati na. 47221.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*