Mkurugenzi aunganishwa kesi ya Simba

Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Idd Simba
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group Limited, iliyonunua hisa za Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam, Robert Simon Kisena ameunganishwa katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Idd Simba na wenzake.Pia washtakiwa hao wamebadilishiwa kesi, kutoka kesi ya jinai ya kawaida na kuwa kesi ya uhujumu uchumi.

Kutokana na mabadiliko hayo, washtakiwa walisomewa mashtaka sita yakiwamo ya rushwa,uhujumu uchumi,matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh8.4 bilioni.Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya alidai mahakamani kuwa baada ya kuchambua ushahidi wamebaini kuwa makosa hayo yanaangukia katika Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Mbali na Idd Simba ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Kisena ambaye ni mshtakiwa wa nne, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 3 ya mwaka 2013, ni Salimu Mwaking’inda na Victor Alfred Milanzi.Mwaking’inda, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo alikuwa Mkurugenzi wa UDA na Milanzi ambaye ni mshtakiwa wa tatu, alikuwa ni Meneja Mkuu wa UDA.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka hayo mapya jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na walisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali Awamu Mbagwa. Hata hivyo Kisena hakuwapo jana mahakamani wakati wenzake wakisomewa mashtaka.

Washtakiwa waliokuwapo mahakamani jana nipamoja na Simba, Mwaking’inda na Milanzi waliokana mashtaka yote.

Wakili Tibabyekomya alidai kuwa Kisena hakuwapo mahakamani hapo jana kwa kuwa taratibu za kumfikisha mahakamani zilikuwa bado hazijakamilika.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka waliyosomewa jana, shtaka la kwanza la kula njama linawahusu Simba na Milanzi na Kisena.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la vitendo vya rushwa, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, shtaka la pili la vitendo vya rushwa linamhusu Kisena peke yake, hata hivyo shtaka hilo halikusomwa kutokana na mshtakiwa huyo kutokuwapo mahakamani.

Shtaka la tatu ni la vitendo vya rushwa ambalo linawahusu Simba na Milanzi. Wakili Mbagwa alidai kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, walikubali kupokea Sh320 milinoni kutoka kwa Kisena ushawishi wa kuiuzia Simon Group hisa za UDA ambazo zilikuwa bado hazijagawiwa.

Katika shtaka la nne ambalo ni la matumizi mabaya ya madaraka, linawahusu Simba , Mwaking’inda na Milanzi.
Chanzo: Mwananchi Mei 01.2013

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU