MSIBA WA ALBERT NGWAIR UPO MBEZI BEACH, TARATIBU ZA MAZISHI ZAANZA

mangwair_img
                                     R.I.P MANGWEA
Na Mwandishi wetu
FAMILIA ya msanii Albert Mangwea aliyefariki dunia jana nchini Afrika Kusini, imeanza taratibu za mazishi na jioni hii inafanya kikao Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam.

Nyota wa Bongo Fleva, Albert Mangwea maarufu kama Ngwair, alifariki dunia jana jioni akiwa nchini Afrika Kusini kutokana na kuzidiwa na matumizi ya dawa za kulevya. Wakati mwili wake unakimbizwa hospitali ya St Hellen Joseph, rafiki yake naye, msanii pia M To Te P alikuwa katika hali mbaya, pia kwa utumiaji wa dawa za kulevya ambako hadi sasa amelazwa kwa matibabu na taarifa zinasema anaendelea vizuri.

Kaka wa marehemu Ngwair, Kenneth Mangwea amesema msiba upo Mbezi Beach, Goigi mjini Dar es Salaam na taratibu za kuirejesha miili ya marehemu nyumbani zimeanza.

Kimuziki, Ngwair aliibukia mkoani Dodoma ambako alikuwa katika kundi moja na Dark Master, Noorah na Mez B na amekuwa akishirikiana na M To The P tangu akiwa msanii anayechipukia baada ya kuhamia Dar es Salaam.

Baada ya kuja Dar es Salaam, Ngwair akapata dili Bongo Records chini ya mmiliki wa studio hizo, Petter Matthysse ‘P Funk’ aliyemuinua zaidi kimuziki na kumfanya awe miongoni mwa wanamuziki nyota nchini.

Wimbo wake wa kwanza kutamba ni Gheto Langu mwaka 2003 ambao ulimpatia umaarufu kabla ya kutoa albamu yake ya kwanza a.k.a Mimi mwaka 2003 ambayo ilimpatia mafanikio makubwa na kubadili maisha yake.

Hata hivyo, mafanikio hayo yalimlevya na kujitumbukiza kwenye utumiaji wa dawa za kulevya, hivyo kujikuta akishindwa kufanya kazi ya muziki kwa usanifu na kuanza taratibu kufilisika hadi kuuza mali zake zote, ikiwemo gari aina ya Jeep.

Ngwair kutoka kwenye kupanga nyumba nzima maeneo ya Sinza, Dar es Salaam akajikuta anarejea kuishi katika ‘magheto’ ya washkaji zake sehemu mbalimbali Dar es Salaam.

Mwaka 2010, Athumani Tippo, mmiliki wa maduka ya Zizzou Fashions alijaribu kumuinua tena msanii huyo baada ya kumchukua kwenye lebo yake na kumuwezesha kutoa albamu ya pili, Nge.

Hata hivyo, Nge haikufanya vizuri sana na kuzidi kumchanganya msanii huyo hivyo kutopea kwenye dimbwi la utumiaji wa dawa za kulevya na ‘kuharibika zaidi’.

Mafanikio yake zaidi ni kushinda tuzo ya Kilimanjaro Music Awards kama mwana Hip Hop Bora wa mwaka 2005.

Mwaka 2003, msanii Wayne Wonder aliyekuja kutumbuiza kwenye Fiesta aliondoka na CD ya wimbo Mikasi ya Ngwair baada ya kuvutiwa na kibao hicho alichowashirikisha Mchizi Mox na Ferooz.

Ngwair alijaribu sana kumuinua kimuziki M, lakini pamoja na ukweli kwamba alikuwa ana kipaji, lakini hakufanikiwa, ingawa aliwahi kutoa albamu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI