SPIKA MAKINDA AKERWA NA KIBONZO DHIDI YA BUNGE.

HABARILEO.5SPIKA WA BUNGE ANNA MAKINDA.Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
WAZIRI wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ameeleza kukerwa na kibonzo (katuni) kilichochapishwa na gazeti la Sunday Nation la nchini Kenya hivi karibuni kikilibeza na kulidhalilisha Bunge la Tanzania.
Kabla ya kuwasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini hapa jana, Waziri Sitta alisema kibonzo hicho kilililenga katika kulichafua Bunge na kulishushia hadhi mbele ya jamii jambo ambalo halikubaliki.
Waziri Sitta alisema kibonzo hicho kilionesha wabunge wa Bunge la Tanzania wakiwa wamelewa, wan
avuta bangi, wamevaa nguo za nusu uchi na matendo mengine ya ovyo ovyo.
“Kitendo hiki kilichofanywa na gazeti hili ni kitendo kibaya na kinachoweza kuleta mfarakano baina ya nchi hizi mbili jirani.
Hatuwezi kukubali kitendo chochote cha kulidhalilisha Bunge letu tukufu kama ilivyofanywa na gazeti hili,” alionya Sitta.
Wakati huo huo sakata la Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuamuru kufungiwa kwa gazeti la kila siku la The Daily Monitor kwa kufichua njama za Rais huyo za kumuandaa mtoto wake Muhoozi Kainerugaba kuwa Rais wa nchi hiyo jana lilizua vuta nikuvute bungeni.
Vuta nikuvute hiyo ilianza pale Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka ujao wa fedha kwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Raya Ibrahim Khamis (Viti Maalum- Chadema), alipotoa kauli ya kulaani kitendo hicho cha Rais Museveni ndani ya Bunge.
Akisoma maoni hayo ya kambi ya upinzani, Raya alisema sasa hivi kumezuka wimbi la kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema matukio ya kuvifungia vyombo vya habari na kuwadhuru waandishi wa habari kwa sababu za kulinda maslahi ya watawala yanazidi kuongezeka kwa kasi kubwa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo Raya alipomaliza kusoma hotuba yake hiyo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Maafa na Bunge, William Lukuvi, akitumia kanuni ya 68 ya Bunge akiomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama kuhusiana na hotuba hiyo.
Kutokana na kanuni hiyo, Lukuvi alimtaka Mhagama akemee kauli hiyo dhidi ya Rais Museveni akisema kitendo hicho kinaweza kuharibu uhusiano baina ya Tanzania na Uganda kutokana na Museveni kukifahamu vizuri Kiswahili.
Hata hivyo kabla ya Mwenyekiti wa Bunge kutoa mwongozo wake kwa jambo hilo alisimama Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) akinukuu kanuni namba 63 kifungu kidogo cha 2, ambapo alisema amesimama ili kumuelekeza Mnadhimu Mkuu wa Serikali bungeni (Lukuvi) kuhusiana na mwongozo aliouomba.
“Mheshimiwa Mwenyekiti (Mhagama) kanuni hii inatamka wazi kwamba Mbunge atasimama bungeni na kuzungumzia habari ambayo imeandikwa au kutangazwa na vyombo vya habari.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani amezungumzia jambo ambalo lilitangazwa na BBC (Shirika la Utangazaji la Uingereza), “ alisema Mnyika.
Hatua hiyo ilimfanya Mhagama kuahidi kutoa ufafanuzi wa suala hilo katika kikao cha jioni jana, ingawa alisema kitendo cha Mnyika kumjibu Waziri Lukuvi kwa mwongozo aliotaka Kiti cha Spika kumjibu kilikuwa ni kukiuka kanuni za Bunge.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.