Teknolojia ya McDonald Liveline ni zaidi ya taaluma

Mwakamele akiwaonesha maofisa wa KPCL, baadhi ya vifaa vinavyotumika katika kazi hiyo. (PICHA ZOTE KAMANDA WA MATUKIO BLOG)

Na Said Mwishehe
WATANZANIA tunakila sababu ya kujivunia pale tunapoona mmoja wetu amebahatika kuwa na teknolojia ambayo inaweza kutuondoa hapa tulipo na kutufikisha hatua nyingine ya maendeleo.
Moja ya sababu ya kufurahia ni kwamba tunaweza kutumia tekonolojia hiyo kwa ajili ya kujenga uchumi imara. Kila Mtanzania anatamani kuona tunapiga hatua zaidi na kuimarisha uchumi wetu.
Nikiri kwamba zipo teknolojia ambazo tukizitumia vizuri nchi yetu inaweza kuokoa fedha nyingi ambazo zinapotea bila sababu. Kwa mfano katika sekta ya umeme malalamiko ni makubwa kutokana na umeme kukatika mara kwa mara.
Mbali ya wananchi kulalamikia kukosekana kwa umeme kutokana na matengenezo ambayo yanafanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), bado kukatika huko kuna sababisha hasara kubwa kwa taifa.
Shughuli za maendeleo zinashindwa kufanyika endapo itakosekana nishati ya umeme. Pia Serikali inapata hasara kwa sababu muda ambao umeme umekatika, maana yake mita haitasoma. Hali hiyo inakwamisha, Tanesco kupata mapato ya kujiendesha.
Swali la kujiuliza ni nani anapenda kuona umeme unakatika mara kwa mara na kukwamisha shughuli za maendeleo? Jibu hakuna.
Kusema hakuna anayefurahishwa pekee haitoshi lazima kama Watanzania tuwe na njia mbadala ya kutatua tatizo hilo ambalo limekuwa sugu ndani ya nchi yetu.
Katika kutafuta ufumbuzi wa suala la kukatika kwa umeme bila sababu ya msingi, Donald Mwakemele ameamua kuanzisha kampuni binafsi inayofahamika kwa jina la McDonald Liveline Technology.
Kampuni hiyo, ipo mkoani Morogoro na kazi yake kubwa ni kufanya kazi ya kutengeneza umeme bila kuukata.
Kwa Afrika Mashariki ni kampuni pekee na kwa Afrika ni moja ya kampuni kubwa inayofanya kazi hiyo ya Liveline Technology ambapo nyingine iko Afrika Kusini.
Ni bahati iliyooje Tanzania kuwa na kampuni hiyo ambayo anayesimamia na mwenye utaalamu huo ni Mtanzania mwenzetu.
Kuwepo kampuni hiyo ambayo pia inatoa mafunzo ya kutengeneza umeme bila kuukata, imefanya watalaamu mbalimbali kuja nchini kujifunza taaluma hiyo ili kukabiliana na matatizo ya kukatika umeme katika nchi zao.
Mfano mzuri, viongozi wa Shirila la Umeme nchini Kenya, hivi karibuni walifika mkoani Morogoro ili kujionea taaluma mbadala ya kutengeneza umeme bila kuukata.
Akizungumza zaidi kuhusu teknolojia hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mwakamele anasema ni muhimu kwa nchi mbalimbali duniani.
Anasema kutokana na umuhimu wake amefanikiwa kufanya kazi ya kutengeneza umeme nchi mbalimbali mbali ya Tanzania.
Sifa kubwa ya teknolojia hiyo inaokoa hasara ambayo ingetoa wakati wa kutengeneza umeme ukiwa umekatwa na kufanya shughuli za maendeleo kushindwa kufanyika katika eneo husika.
“Unapokata umeme wakati unafanya matengenezo unakuwa umesimamamisha shughuli za watu wengi na kuwakosesha kipato, ilihali kuna njia mbadala ambayo ni hii teknolojia ya kufanya matengenezo bila kukata umeme.
“Endapo teknolojia hiyo ya matengenezo bila kukata umeme itatumika, Tanzania itaweza kuokoa fedha na muda ambavyo vimekuwa vikipotea kila umeme unapolazimika kukatwa kwa ajili ya matengenezo kama ya kubadilisha nguzo au kukata miti iliyo karibu na nyanya za umeme,”anasema Mwakamele.
Anaongeza kuwa hakuna sababu ya kukata umeme wakati wa kubadilisha vikombe, kubadili nguzo au sehemu ambayo waya umekatika maana , ipo njia mbadala ya kutengeneza huku umeme ukiendelea kuwepo.
Pamoja na hayo anasema kuwa kutokana na kuona umuhimu wa teknolojia hiyo ambayo aliipata nchini Ujerumani na kufaulu vizuri aliamua kuanzisha chuo ambacho kinafundisha watalaamu wengine ili kuhakikisha inasambaa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
“Hii ni teknojia muhimu ambayo inapatikana katika nchi chache sana duniani.Hivyo kazi iliyopo mbele yangu ni kubwa kwani natakia kuhudumia nchi nyingi za Afrika na wakati mwingine nchi za Magharibi.
“Hivyo mbali ya kufanya kazi kupitia kampuni yangu, bado nimeamua kuanzisha chuo cha Liveline technology ili kufundisha watu wengine.
“Kwa isivyo bahati ni kama ule msemo wa Nabii hakubaliki kwao maana, hapa kwetu, wanaohusika na nishati ya umeme wala hawaoni umuhimu wake.Hawataki kuja kujifunza ili tuwe na wataalamu wengi zaidi. Nilitoa ofa kwa Tanesco walete watu wao niwafundishe lakini kimya.Sijui kwanini , niliamua kutoa ofa hiyo bila malipo na hiyo inatokana na uzalendo kwa nchi yangu,”anasema Mwakemele.
Pamoja na hayo anaweka wazi kuwa, kampuni yake inauwezo wa kuunganisha umeme bila kutumia nguzo za chuma, bali magogo yanayotoka, Iringa na maeneo mengine ya nchi yanatosha kufanya kazi hiyo na eneo likapata umeme kwa gharama nafuu.
Anasema nchi kama Marekani kuna eneo ameweka umeme kwa kutumia nguzo na sifa kubwa ya kutumia nguzo za miti zinapunguza gharama kuliko kutumia nguzo ya chuma.
“Kwa mfano Mkoa wa Iringa kuna sehemu kubwa ambayo haina umeme, tunaweza kutumia nguzo za magogo tukapeleka umeme na baadaye uchumi ukiimarika ndipo sasa tunaweza kuweka nguzo za chuma.Tutakuwa tumepeleka umeme kwa gharama na fuu,”anasisitiza.
Wataalamu kutoka Kenya waliofika kupata ufafanuzi kuhusu teknolojia hiyo , wanasema kuwa wanapaswa kuwa nayo kwa nchi ya Kenya ili kuondoa malalamiko yanayotolewa na wananchi ya kukatiwa umeme.
Wataalamu waliofika katika kampuni hiyo kupata ujuzi huo ni Meneja wa Operesheni na Huduma wa kampuni hiyo Noah Omondi, Mwalimu wa matengenezo ya mtandao wa ugavi wa umeme Peter Waweru na Meneja msaidizi wa huduma na matengenezo wa mkoa wqa Nairobi Charles Mwaura.
Akizungumzia teknolojia hiyo, Noah Omondi anasema wanaamini teknolojia hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa na hasa kwa kuzingatia tatizo la umeme nchini kwao ni kubwa kiasi cha kuwa wanapoteza fedha nyingi na kusababisha hasara kwa kampuni hiyo.
“Sasa tumeweka malengo yetu na tunachohitaji ni kusonga mbele si kurudi nyuma ndiyo sababu  ya kutufanya sisi kuja, Tanzania baada ya kupata sifa za kampuni hii ya Mwakamele,”anasema.
Naye Omondi anasema kwa kuanza kutekeleza malengo yao wamekuja kupata elimu hiyo ili kuona namna gani wanaweza kuleta watu wao kujifunza utaalamu huo ili waanze kuutumia nchini kwao.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI