wakuu wa wilaya waupinga mfumo

Na John Banda, Dodoma
BAADHI ya Wakuu wa Wilaya hapa Nchini wameonekana kuukataa  mfumo mpya wa utaratibu wa utoaji ruzuku ya pembejeo kwa mikopo kwa wakulima na kudai kuwa mfumo huo hautawasaidia wakulima bali watanufaika wachache kama yalivyokuwa Mabilioni ya JK.


Wakuu hao wa Wilaya  walitoa kauli hiyo jana Mjini hapa wakati wakichangia mapendekezo ya utoaji ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa Wakulima kwa kutumia mikopo .

Mmoja wa Wakuu hao wa Wilaya Anthoni Mataka ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero alisema kuwa mfumo huo kwa wakulima wa kawaida ni tatizo kwani hawawezi kumudu kukopa kutokana na suala hilo kuwa janga na kwamba wakulima hawatanufaika bali watanufaika wachache.

“Mfano mzuri tukumbuke yale mabilioni ya JK nani alinufaika kama sio wajanja wachache ambao ndio walinufaika na fedha zile, ni vyema Serikali ikaliangalia suala hili kwa umakin.”
Aliitaka Serikali kutekeleza mfumo huo mpya wa utoaji ruzuku ya pembejeo  kwa mkopo kwa Wakulima kwa majaribio tena kupitia Vyama vichache vya wakulima vya  akiba na mikopo (SACCOS) ili kuona kama mfumo huo unafaa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chemba Francis Isaack alionyesha wasiwasi na kutaka kujua  Serikali imejipangaje katika ukopeshaji huo wa ruzuku za pembejeo kwa mkulima mmojammoja na mipaka yake.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo alisema kuwa kuhusu mfumo huo Serikali inatakiwa kuwa makini na vilevile  ijipange.

“Utaratibu huu mpya wa utoaji ruzuku ni vyema tukawa makini na kukajipanga ili tuweze kuufanikisha  kwani ni suala gumu na linahitaji uangalifu.”Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Singida Parseko Kone alionekana kuwa kinyume na wakuu wenzake kwa madai kuwa hivi sasa baadhi ya benki nyingi ni kero kutokana na kuwanyonya wakulima katika utozaji wa riba kubwa.

Kone alitolea mfano wa suala la mazao ghalani kwa Mkoa wake ilikuwa ni tatizo hivyo ni vizuri Serikali ikaliangalia suala hilo kwa umakini wa hali ya juu.

Licha ya Wakuu hao wa Wilaya kuonekana kupinga utaratibu huo baadhi ya Wakuu wa Mikoa wameonekana kushinikiza utaratibu huo utumike na kuwataka Wakuu hao wa Wilaya kutoogopa bali wakatekeleze suala hilo kwa kujiamini.

Kufuatia kuwepo kwa kauli hiyo ya baadhi ya wakuu hao wa Mikoa Mbunge wa Maswa Magharibi(CHADEMA )John Shibuda  na kusema kuwa kila mfumo una kasoro zake  na anashangazwa na kitendo cha Serikali kushindwa kuondoa kasoro hizo zilizopo katika mfumo wa utoaji ruzuku na badala yake huja na mmbadala ambao sio suluhusho.

“Mara nyingi Serikali ikiona jambo linaharibika huwa inaamua kuja na mmbadala wake badala ya kufanya masahihisho,nilitegemea kabisa hapa tutajadili mapungufu ya mifumo hii ya utoaji ruzuku wa pembejeo lakini sivyo, nasema hivi ukitaka kujikinga na maralia ni vizuri ukaondoa mazalia ya mbu hapo ndo maralia yatakwisha.”Alisema Shibuda.

Warsha hiyo ya siku mbili kuhusu usambazaji wa pembejeo za kilimo imewakutanisha Wakuu  wa Wilaya wa hapa nchini,Wakuu wa Mikoa pamoja na Kamati ya Maji,kilimo na mifugo.

Awali,Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Christopher Chiza alisema kuwa tafiti  zinaonyesha kuwa  sababu kubwa za uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula  nchini  hususani Zao la Mahindi  kupungua na kuwa chini yakilo 500 kwa ekari ni matumizi madogo ya pembejeo bora za kilimo.

Alisema kuwa wakulima wengi nchini wameacha kutumia mbegu bora za kilimo  na mbolea  kutokana na kuwepo  kwa bei kubwa za  ruzuku za mbegu bora za kilimo  na mbolea kwa wakulima wadogo.

Chiza alieleza kuwa ruzuku kwa wakulima imekuwa ikichukuliwa tofauti lakini walengwa wakubwa wanao takiwa kupata ruzuku hizo za pembejeo za kilimo ni wakulima .
MWISHO.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*