AGAPE YAONGOZA KIDATO CHA SITA

Na Mwandishi Wetu
SHULE ya Sekondari Agape iliyoko Mbagala Dar es Salaam, imeshika nafasi ya kwanza katika mkoa huo na kuwa katika shule 20 bora kitaifa kwa shule zenye watahiniwa chini ya 30 katika mtihani wa kidato cha sita.

Mkuu wa shule hiyo, Rabson Fungo, amesema siri ya mafanikio hayo ni nidhamu ya wanafunzi, ushirikiano na kujituma kwa walimu.

Fungo aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Jambo Leo na kufafanua kuwa wamekuwa wanapokea wanafunzi wenye uwezo wa kawaida na kuwanoa katika muda wote wanapokuwa shuleni.

Alisema kutokana na uwepo wa nidhamu ya hali ya juu miongoni mwa wanafunzi, imekuwa ni rahisi kutekeleza mipango mbalimbali ya kuwaendeleza wanafunzi ikiwemo kufanya mazoezi.

Mkuu huyo wa shule alisema kwa matokeo hayo, wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kidato cha sita wataendelea na elimu ya chuo kikuu huku kukiwa hakuna daraja la nne wala sifuri katika matokeo hayo yaliyotangazwa wiki iliyopita.

Fungo amewataka wanafunzi wote waliopata fursa ya kusoma katika ngazi mbalimbali hapa nchini kutumia fursa hiyo kujifunza kwa bidii ili kuliokoa taifa katika hatari ya kutokuwa na wataalamu katika siku zijazo.

Akifafanua zaidi, alisema baadhi ya wanafunzi wanapenda njia za mkato ili wafaulu ikiwemo kufanya udanganyifu wa mitihani.

Alisema kufanya hivyo ni kujidanganya na kulidanganya taifa kwani ushindani katika ajira na utandawazi utawachuja wanafunzi wababaishaji na kutoa ajira kwa vijana wa nchi jirani bila kujali kuwa ni Watanzania au la.

Ametoa mwito kwa wamiliki wa shule kuzingatia kuwa dhamana waliyopewa na taifa katika kuwaelimisha vijana ni kubwa na ni ya heshima hivyo wasiruhusu udanganyifu katika mitihani katika shule wanazozimiliki.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI