MADIWANI CHUNYA WAANZA KUSHAURIANA KUUGAWA MKOA WA MBEYA

 
 DC Chunya Bw  Deudatus
Na Esther Macha wa Matukiodaima.com  Chunya

BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya Chunya, limependekeza mkoa mpya utakaogawanywa kutoka mkoa mama wa Mbeya, uitwe Lupa na makao yake makuu yawe Makongorosi.
Mkoa wa Mbeya kutokana na ukubwa wake wa eneo, hivi upo katika mchakato wa kuugawa ili ipatikane mikoa miwili, lengo likiwa ni kusogeza zaidi huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chunya, Kapala Makelele, aliyasema hayo wakati wa kikao maalum cha Baraza la madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
Makelele alisema:”Ukubwa wa wilaya ya Chunya ni asilimia 46 ya mkoa wote wa Mbeya, hivyo kwa Chunya kuungana na wilaya mpya ya Momba, tutaweza kuanzisha mkoa mpya wa Lupa”.
Aliongeza kuwa kwa wilaya za Chunya na Momba kuungana, zitakuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 35,436.6, hivyo ni wazi malengo ya kusogeza zaidi huduma kwa wananchi wa wilaya hizo zilizopo pembezoni yatakuwa yametimia.
Alisema eneo la Makongorosi, ambalo linapendekezwa kuwa makao makuu ya mkoa wa Lupa, lina ukubwa sahihi na vile vile lipo katika barabara kuu iendayo mikoa ya Tabora na Singida.
Kwa mujibu wa Makelele, mkoa huo iwapo utaanzishwa utaweza kukua haraka kimaendeleo kwani unazo rasilimali nyingi zikiwemo, Ziwa Rukwa, madini aina ya dhahabu, ufuta na misitu mikubwa.
Aliongeza pia wataweza kuigawa wilaya ya Chunya, ili iweze kuzaa wilaya nyingine mbili ikiwemo ya Songwe, hivyo kuweza kusogeza karibu zaidi huduma kwa wananchi wake kama lilivyo lengo la serikali.
“Kwa wilaya hii yenye ukubwa wa robo tatu ya mkoa mzima wa Mbeya,kuendelea kuwa na Mkuu wa wilaya mmoja na mkurugenzi mtendaji mmoja, inakuwa ni vigumu kwao kuweza kusimamia maendeleo ya ndani ya wilaya hii” alisema Makelele.
Kwa kauli moja Madiwani wa halmashauri hiyo, walikubali kuwa mapendekezo yao ni kuanzishwa mkoa mpya wa Lupa wenye makao yake makuu Makongorosi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na mbunge wa jimbo la Lupa, Victor Mwambalaswa, ambaye aliridhia mapendekezo hayo.
Mwisho.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI