SOMA USHAURI WA JAJI BOMANI KUHUSU MFUMO WA MUUNGANO
Thursday, June 13, 2013
JAJI MARK BOMANI |
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani ametoa wito wa
kupingwa kwa kura ya maoni kwa wakazi wa Tanzania Visiwani ili kuona
kama wanahitaji mfumo gani wa Muungano kabla ya kuendelea na mchakato wa
sasa wa rasimu ya Katiba mpya .
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ukumbi wa Idara ya
Habari –MAELEZO , Jaji Mack Bomani alisema anaipongeza tume ya Jaji
Joseph Warioba kwa kazi nzuri na pia kwa mapendekezo yake juu ya
Muungano wa Tanzania.
Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo Jaji Bomani alitoa historia fupi
juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo ameeleza kuwa muungano
huo ulipendekezwa na hayati Sheikh Abeid Amani Karume na hayati
Mwalimu Julius Nyerere, ambao walikutana mara baada ya Mapinduzi ya
Zanzibar Januari, mwaka 1964.
Jaji Bomani aliongeza hayati Karume alipendelea nchi mbili kuungana
na kuwa nchi moja , lakini hayati Nyerere alisita kidogo kwa
kuogopa kwamba ingeonekana Zanzibar imemezwa na Tanganyika na pengine
kuleta maasi Zanzibar hivyo kupendekeza kuundwa mfumo wa muda mfupi
wakati mfumo wa kudumu ukifanyiwa kazi.
“Suala la Muungano ndilo suala kubwa kuliko yote katika mchakato wa
Katiba mpya. Niliwahi kuto ushauri nao ni kwamba ifanyike kura ya
maoni ya wananchi hasa Zanzibar kama wanautaka muungano au la na kama
wanautaka uwe muungano wa mfumo gani ? Mpaka sasa maoni ambayo
yanasikika ni maoni ya viongozi mara Zanzibar ijitoe kwenye muungano
mara tuwe na muungano wa mkataba,” alisema Jaji Bomani.
Akijibu maswali aliyoulizwa na waandishi wa habari ,Jaji Mack Bomani
amesema katika uundwaji wa Serikali tatu anaamini utaweza kumaliza
migogoro inayojitokeza mara kwa mara hasa upande wa Zanzibar kuogopa
kumezwa.
“Woga wa gharama za mfumo wa Serikali tatu hauna msingi. Inategemea
Serikali hizo unazifanya vipi. ipo mifano mingi mno duniani ya miungano
ya mfumo mbalimbali,” alisisitiza.
Pia ameongezea kuwa kama kutaundwa Serikali tatu basi iwe Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Akiongezea kuhusu katiba mpya amesema “kwa maoni yangu si lazima kazi
hii ya katiba iishe kabla ya 2015, tupate muda wa kutosha ili tuweze
kupata katiba ya kueleweka na kukubalika na kila mtu”
Comments