JAMHURI YA MUUNGANO WA TAN ZANIA
WIZARA YA FEDHA
MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA,
MHESHIMIWA DKT. WILLIAM AGUSTAO MGIMWA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA
KWA MWAKA 2013/14

DODOMA
6 Juni, 2013
UTANGULIZI


1.          Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2013/14.

2.          Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa (Mbunge wa Mufindi Kaskazini) na Makamu wake Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula (Mbunge wa Mkinga) kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Mheshimiwa Andrew John Chenge (Mbunge wa Bariadi Mashariki) pamoja na Kamati nzima kwa ushauri wao makini.  Katika uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara kwa mwaka 2012/13.

3.          Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (Mb) na Mheshimiwa Janeth Zebedayo Mbene (Mb). Aidha, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ndugu Ramadhan M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu Dkt. Servacius B. Likwelile, Ndugu Elizabeth J. Nyambibo pamoja na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ndugu Laston T. Msongole kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Vile vile, napenda kuwashukuru Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali, chini ya Wizara kwa michango yao katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/13 NA MALENGO YA MWAKA 2013/14


4.          Mheshimiwa Spika, uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa Mpango na Bajeti ya Wizara unazingatia mambo yafuatayo: Malengo ya maendeleo ya Milenia 2015; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025; Awamu ya pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa mwaka 2011/12 - 2015/16; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA); Mwongozo wa Mpango na Bajeti wa mwaka 2013/14-2015/16; pamoja na Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma - Public Finance Management Reform Programme (PFMRP).

Usimamizi wa Uchumi
5.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Pato la Taifa liliendelea kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2011, ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 6.8 mwaka 2012.  Sekta ya fedha ambayo inasimamiwa na Wizara ya Fedha ilichangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa.  Katika mwaka 2012, sekta hii ya Fedha ilichangia asilimia 1.8 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2011.  Ongezeko hili la ukuaji lilitokana na utekelezaji madhubuti wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Fedha.
6.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho cha mapitio, Wizara pia ilitekeleza Sera ya Fedha na bajeti kwa lengo la kupunguza ukwasi na mfumuko wa bei ambapo Benki Kuu ya Tanzania iliongeza mauzo ya fedha za kigeni katika soko la fedha kama njia mojawapo ya kudhibiti mfumuko huo.  Aidha, Benki ilipandisha kiwango cha chini cha akiba ya amana za Serikali katika mabenki kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40 pamoja na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana na mitaji yao kwa mabenki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba 2012.  Hatua zote zilisaidia kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia 18.7 mwezi Aprili 2012 hadi asilimia 9.4 mwezi Aprili 2013 pamoja na kusaidia kuimarika kwa kiwango cha ubadilishaji wa shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani.  Aidha, katika kuimarisha usimamizi na maendeleo ya sekta ya fedha, Wizara imerekebisha muundo wake kwa kuanzisha Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha – Financial Sector Development Division ambayo itasimamia uandaaji na utekelezaji wa sera za sekta ya fedha na taasisi ndogo za fedha kama SACCOS na VICCOBA.

Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali

7.          Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kusimamia uandaaji na utekelezaji wa bajeti ya Serikali ya matumizi ya kawaida  na miradi ya maendeleo. Wizara imeratibu maboresho ya uandaaji wa bajeti ya 2013/14 kwa kuzingatia mzunguko mpya wa bajeti. Aidha, Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/14, uliandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali na kusambazwa kwa wakati. Vile vile, Wizara imeandaa na kusambaza nyaraka muhimu za bajeti ikiwa ni pamoja na vitabu vya bajeti ya Serikali (volume I, II, III na IV) kama vilivyopitishwa na Bunge na kitabu kinachotoa maelezo ya Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati kwa mwaka 2012/13 - 2014/15. Kitabu hiki kinasaidia kuwajulisha wananchi na wadau wengine kuhusu matokeo ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita pamoja na mwelekeo wa bajeti ijayo kwa kipindi cha muda wa kati. Kadhalika, katika kuboresha uelewa wa bajeti ya Serikali kwa wananchi, Kitabu cha Bajeti Toleo la Wananchi kwa mwaka 2012/13 kimeandaliwa na kusambazwa kwa wakati na kuwekwa kwenye tovuti ya Wizara. Kitabu hiki kimesaidia kueleza bajeti kwa wananchi wa kawaida kwa lugha rahisi na hivyo kuongeza uwazi katika kutoa taarifa muhimu za kibajeti.

8.          Mheshimiwa Spika, katika kujenga uwezo wa kuandaa mipango na bajeti kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara ilitekeleza yafuatayo: kufanya tathmini ya mchakato wa bajeti ya 2012/13 kuhusu namna bajeti ilivyoandaliwa, changamoto zilizojitokeza na jinsi ya kuzitatua;  kuwajengea uwezo maofisa wa bajeti wa Wizara, Idara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu kuandaa bajeti ya 2013/14, maboresho yaliyofanywa kwenye Mfumo wa Kugawa Fedha za Bajeti - Strategic Budget Allocation System (SBAS) na kuandaa bajeti inayozingatia utendaji -Performance Based Budgeting; na kuhuisha Mwongozo wa kuandaa mipango na bajeti, ambao umezingatia mzunguko mpya wa bajeti. Wizara imeendelea kusimamia malipo ya mishahara ya kila mwezi kwa ajili ya Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi  na Wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Usimamizi wa Misaada na Mikopo
9.          Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha usimamizi wa misaada na mikopo ili kupata matokeo yaliyotarajiwa. Mafunzo ya mfumo wa kutunza takwimu na kumbukumbu zingine za misaada na mikopo yalitolewa kwa Maafisa kutoka Wizara 21 na Washirika wa Maendeleo wapatao 20. Aidha, mapitio ya utekelezaji wa Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA), 2006 – 2011 wenye lengo la kuimarisha usimamizi wa misaada, yalifanyika.
10.      Mheshimiwa Spika, katika kuboresha usimamizi wa misaada na mikopo ya kibajeti, Wizara iliandaa mkutano wa Mwaka wa Mapitio ya Misaada na Mikopo ya  Kibajeti - General Budget Support Annual Review meeting uliofanyika mwezi Novemba 2012. Matokeo yaliyotokana na  Mkutano huo ni washirika wa Maendeleo kuipatia Serikali misaada ya kibajeti yenye thamani ya sh. bilioni 1,163.13 fedha ambayo imepangwa kutumika katika bajeti ya 2013/14. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeimarisha Mfumo wa Mapitio ya Matumizi ya Umma - Public Expenditure Review  (PER) kwa kuanzisha Sekretarieti ya pamoja yenye wajumbe wa upande wa Serikali na upande wa Washirika wa Maendeleo pamoja na kuandaa Mpango Kazi wa mwaka.

11.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inatarajia kukamilisha Mfumo mpya wa Ushirikiano wa Kimaendeleo -Development Cooperation Framework , kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Mfumo huu ndio utakaoongoza usimamizi wa Misaada na Mikopo ya Kibajeti katika kutekeleza mipango na programu za kitaifa za kukuza uchumi, kupunguza umaskini na kuleta maendeleo. Aidha, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya Mfumo wa Kutunza Kumbukumbu za Misaada na Mikopo - Aid Management Platform kwa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na Asasi za Kiraia. Vile vile, Wizara itaendelea kuandaa mikutano ya kila mwaka ya Mapitio ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti pamoja na Mapitio ya Matumizi ya Umma.

Uhimilivu wa Deni la Taifa
12.      Mheshimiwa Spika, serikali inasimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa kusimamia Deni na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004. Kwa kuzingatia Sheria hiyo, mwaka 2012 Serikali ilifanya tathmini ya kuangalia uhimilivu wa Deni la Taifa na viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa vinaonesha kuwa, deni la taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati. Mathalani, uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt) kwa Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 18.9 ikilinganishwa na ukomo wake wa asilimia 50. Hii ni ishara kuwa kiwango cha kukua kwa Deni la Taifa ni kidogo ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa. Kiashiria kingine muhimu ni uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt) kwa thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi (export) ni asilimia 56.2 ikilinganishwa na kiwango cha cha ukomo ambacho ni asilimia 200. Hii ni ishara nyingine inayotuhakikishia kuwa Deni la Taifa ni himilivu kwa kuwa kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa ni ndogo ikilinganishwa na uwezo wan chi kulipa deni hilo kwa mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa na humuma nje ya nchi.


13.      Mheshimiwa Spika, katika mkakati wa kuboresha mfumo wa usimamizi wa Deni la Taifa serikali inakamilisha taratibu za kuanzishwa kwa Idara kamili ndani ya Wizara ya Fedha pamoja na kupitia upya Mkakati wa taifa wa kusimamia madeni wa mwaka 2002 na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 ambayo ilirekebishwa mwaka 2004 na hivyo kuboresha muundo uliopo wa usimamizi wa Deni la Taifa pamoja na sheria yake.

Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
14.      Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara ilitekeleza yafuatayo: kuboresha Mfumo wa Malipo Serikalini – Integrated Financial Management System(IFIMS) kutoka mfumo wa toleo la EPICOR 7.3.5 kwenda toleo la EPICOR 9.05 kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma; kukamilisha zoezi la kutoa mafunzo ya kufanya malipo moja kwa moja benki kwa njia ya kielektroniki -Tanzania Inter-Bank Settlement System (TISS) kwa watumishi wa Hazina ndogo zote, Bunge, Mikoa, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI na Idara ya Ushirika, ikiwa ni maandalizi ya kuunganisha Taasisi hizo kwenye mtandao wa TISS ili kuboresha usimamizi wa fedha za umma.

15.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Wahasibu 200 kutoka mikoa 25 walipata mafunzo juu ya usimamizi wa fedha za umma; Wahasibu 425 kutoka wizara mbalimbali na Sekretarieti za Mikoa walipata mafunzo juu ya Viwango vya kimataifa vya kiuhasibu vya kuandaa Hesabu za Serikali International Public Sector Accounting Standards  (IPSAS) na watumishi 120 kutoka katika Wizara na Taasisi walipata mafunzo ya kusimamia Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change Management and Strategic Planning kwa lengo la  kujenga uwezo wa idara za bajeti na Mipango katika kutekeleza maboresho ya usimamizi wa Fedha  za umma.

Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma – Public Finance Management Reform Programme (PFMRP)

16.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kuendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma-PFMRP ambapo Awamu ya Nne ya Programu ilianza kutekelezwa Julai 2012 na itakamilika Juni 2017. Programu ya PFMRP pamoja na mambo mengine, imewezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanza kutumia akaunti sita za benki badala ya akaunti nyingi zilizokuwepo kwa lengo la kuendelea kuboresha usimamizi wa fedha za Umma. Aidha, Programu ilitoa fedha za kuwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuandaa Mpango Mkakati wake wa Programu ya Usimamizi wa Fedha za Umma.  Vile vile, matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa programu yaliyofanywa kama sehemu ya mapitio ya mwaka ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti yaliyofanyika mwezi Novemba 2012 yalionesha kuwa utekelezaji wa Programu ulikuwa wa kuridhisha, na uzingatiaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma katika kufanya ununuzi ulifikia asilimia 74.

17.      Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutekeleza Mpango kazi wa miaka mitano wa kuiwezesha Serikali Kuu kuandaa hesabu kwa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu –International Public Sector Accounting Standards (PSAS) accrual basis. Kwa mara ya kwanza, hesabu za Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2013 zitaandaliwa kwa kutumia viwango hivyo. Aidha, Wizara imeandaa miongozo mbalimbali na kufanya mikutano elekezi ili kuwajengea uwezo na uelewa wahasibu na wadau mbalimbali. Katika kuimarisha usimamizi  wa mapato na matumizi ya  Serikali pamoja na utoaji wa taarifa zenye ubora na uwazi, Wizara imeendelea kusimamia na kuimarisha mtandao wa malipo ya Serikali katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Hazina Ndogo pamoja na Vikosi vya Jeshi.

18.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara itaendelea kusimamia, kuimarisha na kudhibiti mapato na matumizi ya fedha za Serikali kwa kuboresha mtandao wa malipo wa Serikali. Aidha, Wizara itatoa ushauri wa kitaalamu na kuunganisha Hazina Ndogo na Sekretarieti za Mikoa ili kuziwezesha kufanya malipo kwa njia ya ki-elektroniki (TISS) kupitia Benki Kuu ya Tanzania. Vile vile, Wizara itaendelea  kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wahasibu wa Wizara, Mikoa, na Idara za Serikali ya kuandaa hesabu katika viwango vya kimataifa  IPSAS Accrual basis na kuongeza uelewa wa matumizi ya mtandao wa  EPICOR 9.05.

Sera ya Ununuzi wa Umma
19.      Mheshimiwa Spika, katika eneo la Sera ya Ununuzi wa Umma, Wizara imetekeleza yafuatayo: kukamilisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; kukamilisha rasimu ya Kanuni za Ununuzi wa Umma; kuendelea kuhuisha taarifa za maofisa Ununuzi na Ugavi katika daftari ambapo jumla ya Maofisa 989 wameingizwa katika daftari hilo. Aidha, Wizara imeendelea na taratibu za kuanzisha kada ya Ununuzi Serikalini pamoja na kusimamia na kuendeleza kada ya Ugavi nchini.

20.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kuanza utekelezaji wa  Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; kufuatilia na kufanya tathmini ya mfumo wa Ununuzi wa Umma; na kuendelea kuhakiki daftari la taarifa za maafisa Ununuzi na Ugavi Serikalini.


Mpango wa Millenium Challenge Account – Tanzania (MCA-T)
21.      Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia MCA-T imeendelea kusimamia utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC). Utekelezaji wa miradi hiyo umeendelea vizuri licha ya changamoto ambazo zimeathiri kasi ya utekelezaji kama vile mvua nyingi kwa mikoa ya Ruvuma na Rukwa na matatizo ya kiufundi. Ujenzi wa barabara ya Tanga- Horohoro ulikamilika kwa kiwango cha lami na kukabidhiwa kwa Serikali mwezi Oktoba 2012; ujenzi wa barabara za ukanda wa Mtwara yaani Songea – Namtumbo na Peramiho – Mbinga na ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Kisiwa cha Mafia unaendelea. Aidha, kazi ya kuweka lami katika barabara tano za Pemba ya Vijijini Kaskazini imeanza na ujenzi wa barabara ya Tunduma – Sumbawanga ambao umegawanywa katika sehemu tatu; Tunduma – Ikana, Ikana – Laela na Laela – Sumbawanga unaendelea.

22.      Mheshimiwa Spika, Miradi ya kupeleka umeme Zanzibar kupitia chini ya bahari na ule wa ukarabati wa mtandao wa umeme kwa mkoa wa Dodoma imekamilika. Utekelezaji wa miradi mingine ya ukarabati wa vituo vya kupoozea umeme, ukarabati wa mtandao wa umeme kwa mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Mwanza na Kigoma, ikiwa ni pamoja  na mradi wa umeme wa Jua Kigoma, inaendelea. Aidha, miradi ya upanuzi wa mtambo wa maji Ruvu chini na ukarabati wa mfumo wa maji kwa Manispaa ya Morogoro nayo pia inaendelea.

23.      Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa kuridhisha wa miradi, katika kikao cha Bodi ya MCC kilichofanyika mwezi Desemba 2012, kiliamua kuikubalia Tanzania kuidhinisha maandalizi ya Mpango wa Pili wa miradi ya MCC (MCC Compact II). Serikali imeshaanza maandalizi hayo baada ya kuunda  sekretarieti ya uratibu

Ukaguzi wa Ndani
24.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imeandaa na kutoa miongozo ya Usimamizi wa vihatarishi katika Sekta ya Umma pamoja na Mwongozo wa Uhakiki wa Ubora wa Ukaguzi wa Ndani. Miongozo hii ilizinduliwa mwezi Machi, 2013. Aidha, Wizara imetayarisha Mwongozo wa Ukaguzi wa Ndani kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na unategemewa kuanza kutumika rasmi mwezi Julai, 2013. Kadhalika, Wizara imekamilisha Mkataba wa Makubaliano kati ya Wakaguzi wa Ndani na Wateja wake  na pia kutoa kanuni za maadili ya wakaguzi wa ndani. Miongozo hiyo ina lengo la kuboresha utendaji kazi wa ukaguzi wa ndani.

Ukaguzi wa Hesabu za Serikali

25.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iliendelea kutekeleza yafuatayo: kufanya ukaguzi wa  hesabu za mafungu yote ya Wizara na Idara za Serikali, Mikoa ya Tanzania Bara, Halmashauri, Mashirika ya Umma, Balozi na Wakala wa Serikali; kukamilisha ripoti tano za ukaguzi wa ufanisi -Value for Money Audit ambapo  taarifa zote hizi zimewasilishwa hapa Bungeni tarehe 11 Aprili 2013; ukaguzi wa Mashirika 50 ulikuwa unaendelea katika hatua mbalimbali za ukaguzi; Ofisi imeendelea kukiimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ufanisi kwa kutoa mafunzo kwa watumishi saba na kukipatia vitendea kazi zaidi. Aidha, ofisi iliendelea kulipia mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 53 waliopo katika vyuo mbalimbali na kugharamia mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 400. Vile vile, ujenzi wa ofisi unaendelea katika mikoa ya Dodoma na Rukwa na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2014.

26.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14, Ofisi itatekeleza shughuli zifuatazo:  kuendelea kutekeleza mkakati wa kuwaondoa wakaguzi katika ofisi za wakaguliwa; kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vyote vya siasa nchini ili kukidhi matakwa ya sheria ya vyama vya siasa na kuendelea kufanya mazungumzo na Msajili wa vyama vya siasa namna ya kutekeleza Sheria ya Gharama za Uchaguzi; na kuziimarisha Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali – Public Accounts Committee (PAC) na Local Authorities Accounts Committee (LAAC), Kamati ya Bajeti na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara kwa kuzijengea uwezo.

27.       Mheshimiwa Spika, shughuli nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja na: kuhakiki matumizi ya fedha za Halmashauri; kushiriki kikamilifu katika jukumu jipya la kukagua Taasisi za Umoja wa Mataifa ambapo ofisi inaingia mwaka wa pili wa kuwepo kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa -UN Board of Auditors; kufanya kaguzi sita za thamani ya fedha; kuendelea na uunganishaji wa ofisi za Ukaguzi zilizoko mikoani na makao makuu kwa kutumia Mtandao Mpana -Wide Area Network (WAN); kuimarisha ukaguzi wa kiutambuzi - Forensic audit; na kuongeza idadi ya watumishi.



Sheria na Miswada ya Fedha
28.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara iliendelea kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali ili kuweka usimamizi mzuri wa kodi na fedha za umma. Baadhi ya sheria zilizofanyiwa marekebisho ni sheria mbalimbali za kodi ambazo zilipitishwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 - The Finance Act, 2012 na Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu iliyofanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali iliyopitishwa na Mkutano wa Bunge wa mwezi Februari, 2013. Aidha, marekebisho ya Mkataba wa Cotonou unaohusu ushirikiano baina ya nchi za Jumuiya ya Ulaya, Afrika na Visiwa vya Caribbean ambapo Tanzania ni mwanachama, yalipitishwa na Bunge kupitia Azimio la Bunge katika Mkutano wa mwezi Novemba, 2012.


29.      Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliandaa kanuni mbalimbali ili kuwezesha usimamizi na utekelezaji wa Sheria za Kifedha. Baadhi ya kanuni zilizotolewa ni zile za; kuanzisha credit Reference  Databank ya Utunzaji wa Taarifa za Wateja wa Benki na Taasisi za Kifedha; Pamoja na Credit Reference System. Matumizi ya Vifaa vya Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Kodi ya Mapato; Usimamizi wa Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa abiria wa ndege ambao sio raia wa Tanzania; Kanuni za Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu; na Kanuni za Sheria ya Uwekaji Stempu kwenye kazi za Wasanii.

30.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara itaendelea  kukamilisha maandalizi ya kuwezesha kutungwa kwa Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani – Vale Added Tax (VAT), Sheria ya Utawala wa Kodi - Tax Administration Act, Sheria ya Hoteli - Hotels Tax Act, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini - Government Employees Provident Fund (GEPF). Aidha, Wizara inatarajia kuwasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, pamoja na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ili kuihuisha kulingana na mazingira ya sasa ya uchumi. Vile vile, wizara itaandaa kanuni mbalimbali zitokanazo na sheria hizi ili kuwezesha utekelezaji wake.

Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma
31.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia utendaji wa Mashirika ya Umma pamoja na Taasisi zake. Majukumu yaliyotekelezwa kwa kushirikiana na Shirika Hodhi - Consolidated Holding Corporation (CHC) ni pamoja na kuendelea na zoezi la urekebishaji wa mashirika yaliyo na matatizo katika sekta za Usafirishaji, Madini, Mawasiliano, Utalii na Fedha.


32.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepata ofisi katika jengo la CHC Mtaa wa Samora na tayari watumishi wamehamia katika ofisi hiyo. Katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inatarajia kutekeleza yafuatayo: kusimamia utendaji wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma na kuboresha utawala bora kwa kuingia Mikataba ya Utendaji -Performance Contracts na Bodi za Mashirika ya Umma; kusimamia mikakati ya kurekebisha Mashirika ya Umma na uperembaji wa Mashirika ya Umma yaliyobinafsishwa; na kuimarisha usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma ili kuongeza ufanisi na mapato ya Serikali.


Mafao ya Wastaafu na Mirathi

33.      Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za pensheni, Wizara imeanza utaratibu wa kulipa Pensheni kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu badala ya vipindi vya miezi sita sita kuanzia Januari, 2012. Katika utaratibu huu, Wastaafu wanalipwa Pensheni ya miezi miwili mapema - in advance badala ya miezi mitano iliyokuwa inalipwa katika utaratibu wa awali. Pensheni inalipwa mwishoni mwa miezi ya Julai, Oktoba, Januari na Aprili. Aidha, Wizara imeendelea na kazi ya kuweka kumbukumbu za Wastaafu waliopo kwenye daftari la Pensheni la Hazina kwenye Mfumo wa Kompyuta ujulikanao kwa jina la SAPERION kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa. Hadi kufikia mwezi Aprili 2013, kumbukumbu za Wastaafu 106,030 ziliwekwa kwenye mfumo wa kompyuta. Zoezi hili litaendelea kufanyika katika mwaka 2013/14 ili kukamilisha uhifadhi wa kumbukumbu za Wastaafu wote wanaolipwa kupitia Hazina.


34.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu shughuli za mifuko ya pensheni iliyo chini ya Wizara ya Fedha. Mifuko hiyo ni Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) na Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF).
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma - PSPF

35.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2013 Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma ulisajili wanachama 332,067.  Katika kipindi hicho, Mfuko pia ulikusanya jumla ya shilingi bilioni 446.12. Kati ya makusanyo hayo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni 374.76 na mapato yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 71.36. Matarajio ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni 749.10 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2012/13. Aidha, thamani ya Mfuko hadi tarehe 30 Aprili, 2013 ilifikia shilingi bilioni 1,112.24 na unatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,226.59 mwezi Juni, 2013. Jumla ya shilingi bilioni 422.16 zilitumika kulipa mafao ikiwa ni pamoja na mafao ya kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi sawa na asilimia 93.21 ya lengo la mwaka.  Vile vile, ili kuongeza wigo wa wanachama, Mfuko umeanzisha mpango maalum wa kuchangia kwa hiyari kwa watumishi wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
 
36.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/14, Mfuko unatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 680.55, kati ya makusanyo hayo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni 539.18, na mapato yatokanayo na vitega uchumi ni shilingi bilioni 141.37. Aidha, thamani ya Mfuko inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,522.01. Mfuko unatarajia kulipa kiasi cha shilingi bilioni 522.32 kwa ajili ya mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi, ambapo jumla ya wanachama wapatao 7,647 wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa sheria. Vile vile, Mfuko unatarajia kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 1,211.39 kwenye maeneo mbalimbali ya vitega uchumi.


Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini - GEPF

37.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2013 Mfuko umesajili jumla ya wanachama 6,755 wakiwemo wananchi waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi. Katika kipindi hicho michango ya wanachama ilifikia kiasi cha shilingi bilioni 22.74 sawa na asilimia 64.60 ya malengo ya mwaka mzima. Mapato yatokanayo na vitega uchumi yamefikia shilingi  bilioni 11.64 ambayo ni sawa na asilimia 72.75 ya malengo ya mwaka mzima na thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 190.0 Machi, 2013. Aidha, Mfuko umelipa mafao ya shilingi bilioni 7.13 hadi kufikia Machi, 2013 na kufungua ofisi katika Manispaa za Temeke, Kinondoni na Ilala kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.


38.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Mfuko utaendelea na jitihada zake za kuboresha huduma kwa wanachama, kutanua wigo wa wanachama, kukuza mapato yatokanayo na uwekezaji na kusajili wanachama wengi zaidi kupitia Mpango wa Hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni na wa lazima. Aidha, Mfuko unatarajia kusajili jumla ya wanachama 16,500 na kukusanya michango yenye thamani ya shilingi bilioni 40.50. Vile vile, mapato ya vitega uchumi yataongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 19.24 na thamani ya Mfuko inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 227.


Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma - PPF

39.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Mfuko ulikusanya shilingi bilioni 229.1 kutokana na michango ya wanachama ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 21.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 188.1 zilizokusanywa mwaka 2011. Ongezeko hili lilitokana na waajiri kuzingatia sheria kwa kuleta michango kwa wakati na uandikishaji wa wanachama wapya. Aidha, idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 180,049 mwaka 2011 hadi 203,981 mwaka 2012. Mfuko pia ulilipa mafao ya jumla ya shilingi bilioni 99.4. Mafao hayo ya PPF yalijumuisha na mafao ya elimu ambayo hulipwa kwa ajili ya kusomesha watoto wasiozidi wanne wa mwanachama aliyefariki akiwa kazini. Mwaka 2012 mfuko ulisomesha watoto 1,333 kwa gharama ya shilingi milioni 683 ikilinganishwa na watoto 1,392 waliosomeshwa mwaka 2011 kwa gharama ya shilingi milioni 573. Watoto hawa husomeshwa kuanzia elimu ya chekechea hadi kidato cha nne. 


40.      Mheshimiwa Spika, mapato yatokanayo na uwekezaji yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 91.4 mwaka 2011, hadi kufikia shilingi bilioni 105.5 kwa mwaka 2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.4. Aidha, thamani ya Mfuko kufikia Desemba 2012, ilikuwa imeongezeka kufikia shilingi bilioni 1,089.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.8 ikilinganishwa na thamani ya Mfuko ya shilingi bilioni 894.5 ilivyokuwa Desemba 2011.


41.      Mheshimiwa Spika, Mfuko unatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 281.7, kuandikisha wanachama wapya 72,000 kutoka sekta ya umma na binafsi, na  kukusanya shilingi bilioni 125.6 kutokana na uwekezaji ifikapo Desemba 2013. Aidha, thamani ya Mfuko inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 1,302.68.

42.      Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na changamoto kadhaa katika Mifuko ya Hifadhi ya jamii ikiwemo: Wanachama kulalamikia kiwango kidogo cha mafao kitolewacho na baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pale wanapostaafu. Vile vile, kuna suala la malimbikizo ya madeni yanayotokana na Mifuko  kugharimia utekelezaji wa  miradi ya Serikali.  Aidha, katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo Serikali kupitia Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii imepanga kutathmini uwezo wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kupendekeza viwango vya mafao; na kuhakikisha kwamba, mifuko hiyo inakuwa endelevu.  Vile vile, Serikali inaendelea kulipa madeni ya mifuko ya jamii  kwa awamu na  pia imeunda kamati ya kuchambua na kuhakiki madeni mengine  ya baadhi ya mifuko ili kupendekeza njia endelevu ya kuyalipa.



Mamlaka ya Mapato Tanzania - TRA
43.      Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutekeleza Mpango wa tatu wa Maboresho wa mwaka 2008/09 - 2012/13 ambao umekuwa msingi wa kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato mwaka hadi mwaka. Katika jitihada za kuongeza mapato ya ndani, Wizara kupitia TRA imetekeleza yafuatayo: kuanzisha mfumo wa kimtandao wa kuwasilisha ritani za kodi - tax returns; kufanya tathmini ya maeneo hatarishi katika Utawala wa Sekta za Umma; kuweka mfumo wa taarifa wa RADDEX 2 na kutoa mafunzo kwa watumiaji; kusambaza Mfumo wa Ki-elektroniki wa Ufuatiliaji Usafirishaji Mizigo (Electronic Cargo Tracking System); na kuboresha mfumo wa utunzaji kumbukumbu na Taarifa za Magari. Aidha, TRA imekamilisha uandaaji wa Awamu ya Nne ya Mpango wa Maboresho (2013/14 - 2017/18) unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2013/14.

44.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara kwa kushirikiana na TRA itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kupanua wigo wa makusanyo na kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi.

45.      Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Mei 2013 kulitokea tatizo  la mlundikano wa makonteina Bandarini Dar es Salaam kutokana na kutokamilika kwa taratibu za kuyaondoa. Kutokana na tatizo hili Wizara ilikutana na wadau wote pamoja na wafanyabiashara ili kuondoa adha hiyo. Katika kikao hicho Mamlaka ya Mapato ilielekezwa kushughulikia suala hilo kulingana na sheria na taratibu ili wafanyabiashara waweze kulipia makonteina yao na kuyaondoa bandarini. Tunapenda ieleweke kwamba katika tatizo hili hakuna kodi yoyote iliyoongezwa kwa makonteina hayo ya wafanyabiashara na walitakiwa kulipa kodi stahili.
Huduma za Kibenki
Benki Kuu ya Tanzania

46.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kwa kupitia Benki Kuu imeendelea kutekeleza mabadiliko chanya katika sekta ya fedha ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachochea maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi. Mabadiliko ya sekta ya fedha yamesababisha utendaji mzuri wa Taasisi  za Fedha ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya mabenki kutoka benki 49 mwezi  Februari, 2012 mpaka benki 51 mwisho wa mwezi Februari 2013. Aidha, rasilimali za mabenki zimeimarika zaidi na kufikia shilingi trilioni 17.3 mwezi Februari ambapo mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi imefikia shilingi trilioni 8.8.

47.      Mheshimiwa Spika, katika kuendelea na jitihada za kuboresha upatikanaji wa mikopo, Benki Kuu  imeanzisha mfumo wa ukusanyaji  na utunzaji wa kumbukumbu za wakopaji (Databank) na utaratibu wa utoaji wa taarifa za wakopaji kwa kutumia kampuni binafsi (Credit Reference Bureaux). Mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za wakopaji umeshaanza kufanya kazi na mabenki yameshaanza kupeleka taarifa za wakopaji. Kampuni mbili za utoaji wa taarifa za wakopaji zimeshapewa leseni na wapo katika maandalizi ya mwisho ili waanze kutoa huduma ya kutoa taarifa hizo. Mfumo huu utaboresha upatikanaji wa mikopo ya muda wa kati na muda mrefu.

48.      Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Benki Kuu imetoa Mwongozo wa Huduma za Kibenki kwa Kutumia Wakala wa Mwaka 2013 (Guidelines on Agent Banking for Banking Institutions, 2013) ambao ulianza kutumika mwezi Februari, 2013. Kutolewa kwa mwongozo huu ni sehemu ya mpango wa kuweka mazingira yatakayowezesha kupanua wigo wa huduma za kibenki na kuhakikisha usalama wa benki mbalimbali zitakazojihusisha na mfumo wa utoaji huduma za kibenki kwa kutumia mawakala. Mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa huduma bora na nafuu za kibenki.

49.      Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Benki Kuu imeunda Kamati ya Kitaifa ya Uthabiti wa Mfumo wa Fedha (Tanzania Financial Stability Forum) ili kusaidia kuimarisha ushirikiano na kubadilishana taarifa kati ya wadhibiti wa sekta ya fedha kama msingi imara kwa ajili ya kuhakikisha uthabiti wa mfumo wa fedha nchini na kupanua wigo wa usimamizi katika mfumo wa fedha kutoka usimamizi unaolenga taasisi moja moja kwenda usimamizi wa mfumo wa fedha unaolenga sekta nzima ya fedha kwa ujumla wake. Aidha, taarifa inayoonesha hali halisi ya uthabiti wa sekta ya fedha inatolewa kila baada ya miezi sita.

50.      Mheshimiwa Spika, Benki Kuu za Afrika Mashariki zilikubaliana kutengeneza mfumo wa malipo utakaorahisisha malipo kwa kutumia sarafu za nchi husika. Mfumo huu ujulikanao Kama East African Cross Border Payment System - EAPS, umefikia hatua ya majaribio kupitia mifumo ya Malipo Makubwa (Real Time Gross Settlement System – RTGS) ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Mategemeo ni mfumo huu kuanza kutumika kwa nchi hizi tatu, ikiwa taratibu zote za kujiunga na mfumo huu zitakuwa zimekamilika, mwezi Julai 2013. Aidha, Nchi za Rwanda na Burundi zitakapokuwa tayari zitajiunga na mfumo huo. Kuanza kwa mfumo huu wa malipo kutarahisisha malipo katika Jumuiya na kukuza shughuli za kibiashara na uchumi.

51.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu itaandaa mapendekezo ya kutunga Sheria ya kusimamia  mifumo ya malipo nchini (National Payment Systems Act). Aidha, Benki kuu itaendelea kuandaa sera za kifedha na kusimamia utekelezaji wake. Vile vile, Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu  itafanya tathmini ya mpango wa utekelezaji wa Awamu ya  Pili ya  Mpango wa Maboresho ya Sekta ya Fedha unaoishia Juni, 2013 na kuandaa mpango wa utekelezaji wa awamu ya tatu. Kadhalika, Benki Kuu itahakikisha mwongozo wa kitaifa kuhusu elimu ya masuala ya fedha (Financial Education Framework) unazingatiwa. Mwongozo huu unalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na kutumia huduma za fedha katika shughuli zao za kila siku.

Benki ya Maendeleo TIB - TIB Development Bank
52.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13 Benki ya Rasilimali (TIB) iliendelea na utekelezaji wa marekebisho ili kuwa benki imara ya maendeleo tangu Novemba 2012 benki ilibadilisha jina na kuitwa TIB Development Bank ili kuweka wazi dhana ya benki ya maendeleo. Aidha, mchakato wa uanzishwaji wa benki ambayo kampuni tanzu inayojishughulisha na shughuli za biashara (TIB Corporate Bank) ambapo usajili wake upo katika hatua za mwisho. Mara taratibu zote zitakapokamilika, TIB itafanya kazi katika mfumo wa makampuni mawili yanayotegemeana moja likijikita kwenye shughuli za maendeleo (TIB Development Bank) na lingine kwenye shughuli za kibiashara (TIB Corporate Bank). Benki hizi zitakamilisha muundo wake ifikapo mwezi Septemba, 2013.

53.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/13, Benki ilifungua tawi  mkoani Mbeya na ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hii inafanya benki kuwa na jumla ya matawi matano na ofisi tatu za kanda. Aidha, hadi kufikia Desemba 2012, Benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 242.9 ikilinganishwa na mikopo ya shilingi bilioni 181.7 Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 74.8. Mikopo mingi ilitolewa kwenye sekta ya kilimo na usindikaji wa mazao ya kilimo (mikopo hii ni tofauti na ile ya Dirisha la kilimo). Vile vile, mtaji wa benki ulifikia shilingi bilioni 142.1 baada ya Serikali kuongeza shilingi bilioni 40. Benki ilipata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 8.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 48 toka shilingi bilioni 5.8 zilizopatikana mwaka ulioishia Desemba 2011.

54.      Mheshimiwa Spika, Dirisha la Kilimo katika Benki ya Maendeleo TIB liliendelea kutoa mikopo kwa wakopaji mbalimbali kwa riba nafuu. Tangu kuanza kwa dirisha mwaka 2010 hadi kufikia Desemba 2012, maombi yenye thamani ya shilingi bilioni 40.1 yaliidhinishwa ambapo shilingi bilioni 20.0 (asilimia 49.9) zilikopeshwa kwa makampuni; shilingi bilioni 5.7 (asilimia 14.2) kwa taasisi ndogo za fedha zinazokopesha wakopaji wadogo; na shilingi bilioni 14.4 (asilimia 35.9) kwa vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) ambavyo pia vinafaidisha wakopaji wadogo. Hii inamaanisha asilimia 50.1 ya mikopo imetolewa kwa wajasiriamali wadogo. Aidha, kuanzia Julai, 2013 Dirisha la Kilimo lililopo TIB litahamishiwa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.


55.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Desemba 2013, mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo TIB katika sekta mbalimbali inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 379.2 na faida kabla ya kodi inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 16.6.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo - TADB

56.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB. Lengo la kuanzisha benki hiyo ni kutoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu katika sekta ya kilimo inayojumuisha uvuvi na mifugo. TADB ilisajiliwa BRELA chini ya Sheria ya Kampuni ya mwaka 2002 kwa jina la Tanzania Agricultural Development Bank Limited (TADB Ltd). Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 90.0 kati ya lengo la shilingi bilioni 100 kimeshatolewa kama kianzio cha Mtaji.  Vile vile, Muundo wa benki ya kilimo na majukumu ya wafanyakazi katika nafasi mbalimbali umeandaliwa. Mwenyeketi na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wameteuliwa na ajira za maafisa waandamizi wa benki hiyo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Katika mwaka 2013/14, shilingi bilioni 10 zimetengwa ili kukamilisha lengo la mtaji wa kuanzia wa shilingi bilioni 100.

Twiga Bancorp
57.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi kinachoishia Desemba 2012 Taasisi iliendelea kupanua shughuli zake kwa kufungua tawi moja mkoani Dodoma na kuifanya taasisi kuwa na matawi matano. Katika kipindi hicho, amana za wateja zilifikia shilingi bilioni 58.41 ikilinganishwa na shilingi bilioni 54.2 Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 7.8. Aidha, mikopo iliyotolewa ilifikia shilingi bilioni 39.43 ikilinganishwa na shilingi bilioni 35.9 kwa mwaka ulioishia Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 9.8. Vile vile, Taasisi iliwekeza shilingi bilioni 4.7 kwenye Dhamana za Serikali na Amana katika Benki zingine ikilinganishwa na shilingi bilioni 19.0 zilizowekezwa katika kipindi kama hicho mwaka 2011.

58.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka unaoishia Desemba, 2013, amana za wateja zinatarajiwa kufikia shilingi bilioni 73.25 kutoka shilingi bilioni 58.41 za Desemba, 2012; mapato kutokana na shughuli mbalimbali za kibiashara yanatarajia kufikia shilingi bilioni 12.66 ikilinganishwa na shilingi bilioni 9.56 zilizokusanywa Desemba, 2012; na mtaji ghafi wa Benki (Owners’ Equity) unatarajiwa kukua kutoka shilingi bilioni 5.81 hadi shilingi bilioni 7.24 ifikapo  Desemba 2013. Aidha, thamani ya mikopo kwa wateja inatarajia kufikia shilingi bilioni 49.10 na uwekezaji katika Dhamana za Serikali na Amana za Muda Maalum kwenye mabenki unatarajia kufikia shilingi bilioni 16.80. Vile vile, Taasisi inatarajia kupata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 0.48.

Benki ya Posta - TPB
59.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012 Benki ilianzisha huduma mpya ya Platinum Account inayolenga vijana walio katika Vyuo Vikuu na Taasisi nyingine za elimu ya juu.  Manufaa ya huduma hii ni kuwawezesha vijana kujiwekea akiba na kupitishia mikopo ya elimu. Aidha, Benki iliendelea kupanua mtandao wake kwa kufungua matawi madogo  katika ngazi ya Wilaya katika vituo vya Shirika la Posta. Vile vile, Benki ilianzisha huduma ya POPOTE Quick Account, inayomuwezesha mteja kupata huduma za benki mahali popote kupitia simu ya mkononi kwa lengo la kuwafikia Wananchi walio wengi wanaoishi vijijini.


60.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, amana za wateja zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 120.92 mwaka 2011 hadi kufikia shilingi bilioni 144.56 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.4. Aidha, benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 103.34 ikilingalishwa na shilingi bilioni 66.75 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 54.83. Vile vile, uwekezaji katika vitega uchumi vya Benki ya Posta umeongezeka kutoka shilingi bilioni 117.67 mwaka 2011 hadi kufikia shilingi bilioni 146.96, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24.9. Kadhalika, Benki imepata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 3.59 ikilinganishwa na shilingi bilioni 2.58 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 39.4. Katika mwaka 2012/13, Serikali iliiongezea Benki ya Posta mtaji wa shilingi bilioni 1.5 na kufanya mtaji wa benki kuwa jumla ya shilingi bilioni 16.82.

61.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013, benki itaendelea na mkakati wake wa kuimarisha huduma zitolewazo kupitia Shirika la Posta kwa kukarabati na kuunganisha katika mtandao wa benki vituo 10 vya Posta vilivyoko Temeke, Tunduma, Kahama, Geita, Masasi, Peramiho, Njombe, Kyela, Simiyu na Kasulu hivyo kuvipa uwezo wa kutoa huduma za haraka. Vituo hivi vitakuwa ni matawi madogo na hivyo kufanya benki kufikisha jumla ya matawi 23. Aidha, benki  itafunga vifaa vya ki-elektroniki katika vituo vya mauzo. Vile vile, Benki inatarajia kupanua wigo wa mikopo kwa kuingia mikataba na Sekretarieti za Mkoa na Jeshi la Kujenga Taifa, na kuongeza kipindi cha marejesho kutoka miaka mitatu hadi minne. Kadhalika, Benki inatarajia kupata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 5.11 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.5 ikilinganishwa na faida ya shilingi bilioni 4.07 iliyopatikana mwaka 2012.

Taasisi za Kitaalam na Huduma Nyinginezo
62.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara iliendelea kusimamia taasisi za kitaalam na huduma nyinginezo ambazo ziko chini ya Wizara ya Fedha ambazo ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS; Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi – NBAA; Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi – PSPTB; na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha. Aidha, huduma nyingine zinajumuisha:  Usimamizi wa shughuli za Bima;  Masoko ya Mitaji na Dhamana; na huduma za dhamana ya uwekezaji.



Taasisi za Mafunzo
63.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara imeendelea kusimamia taasisi za mafunzo zilizo chini yake. Taasisi hizo ni Chuo cha Usimamizi wa Fedha – IFM, Taasisi ya Uhasibu Arusha – IAA, Taasisi ya Uhasibu Tanzania – TIA  Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini – IRDP, na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC .

CHANGAMOTO
64.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo zifuatazo:-

i)            Kudhibiti matumizi ya fedha za umma sambamba na kuongeza mapato ya Serikali;

ii)          Kuzingatia  kanuni na taratibu zilizoainishwa kwenye Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) na upatikanaji wa fedha kutoka kwa wafadhili wa nje;
iii)         Kuwa na Sera ya Mali ya Serikali.

iv)         Kufikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi;

v)          Kuwepo kwa mahitaji makubwa ya fedha nje ya bajeti;

vi)         Kuwepo kwa mchakato mrefu wa upatikanaji wa fedha za kugharamia Miradi ya Maendeleo hasa mikopo ya kibiashara (non-conscessional borrowing); na

vii)       Kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni ya ndani katika mafungu mbalimbali ambayo yameshindwa kuingizwa kwenye viwango vya bajeti.

65.      Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara itachukua hatua kupitia mipango na bajeti zake ili kuhakikisha kuwa changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi katika mwaka 2013/14 na kuendelea. Hatua za ufumbuzi wa changamoto hizi zitaelezwa katika hotuba ya bajeti ya Serikali itakayowasilishwa Juni 13,  2013.
Mapitio ya Mapato na Matumizi ya Mafungu ya Wizara kwa Mwaka 2012/13
66.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, majukumu ya Wizara yalitekelezwa katika mafungu sita ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 - Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22 - Deni la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 - Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha. Aidha, Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, linaombewa fedha Bungeni na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa Sheria.

Fungu 50 – Wizara ya Fedha
67.      Mheshimiwa Spika, Wizara ilitarajia kupata shilingi  bilioni 124.42 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato  yasiyo ya kodi kupitia Fungu 50. Vyanzo hivyo ni pamoja na mauzo ya mali, uuzaji wa nyaraka za zabuni na mapato kutoka katika Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali yakiwemo Gawio, Michango na Marejesho ya mikopo. Hadi  kufikia mwezi Aprili, 2013, makusanyo yalifikia shilingi bilioni 37.27 sawa na asilimia 29.97 ya lengo. Makusanyo zaidi yanatarajiwa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha baada ya Mashirika mengi kuandaa hesabu za mwaka  na ukaguzi wa hesabu hizo kukamilishwa.

68.      Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 50 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa  shilingi bilioni 98.41 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 546.51 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 70.32 sawa na asilimia 71.46 ya makadirio na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 311.28 sawa na asilimia 56.96 ya makadirio.



Fungu 23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali
69.      Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 23 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa  shilingi bilioni 75.12 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 6.12 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 49.34 sawa na asilimia 65.67 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 1.29 sawa na asilimia 21.05 ya makadirio.

Fungu 22 - Deni la Taifa
70.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13  makadirio ya matumizi ya Fungu 22 yalikuwa shilingi bilioni 2,735.91. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013 matumizi ya fungu hili yalifikia shilingi bilioni 2,226.70 sawa na asilimia 81.39 ya makadirio.


Fungu 21- HAZINA
71.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikadiria kukusanya mapato ya shilingi bilioni 8,070. Hadi kufikia Aprili, 2013, TRA ilikusanya shilingi bilioni 6,580 sawa na asilimia 97.84 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 6,725 katika kipindi hicho.

72.      Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 21 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa  shilingi bilioni 725.57 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 101.95 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Aidha, kiasi cha Shilingi bilioni 50.66 kilifanyiwa uhamisho kuongezea katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na kufanya makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa mwaka 2012/13 kuwa shilingi bilioni 152.61. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 516.61 sawa na asilimia 71.2 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 131.95 sawa na asilimia 86.46 ya makadirio.

Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu
73.      Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 13 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa  shilingi bilioni 2.16 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 0.26 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 1.01 sawa na asilimia 46.62 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 0.04 sawa na asilimia 14.72 ya makadirio.

Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
74.      Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya kawaida kwa Fungu hili yalikuwa shillingi bilioni 1.99, hadi kufikia Aprili, 2013 matumizi yalifikia shilingi bilioni 1.33 sawa na asilimia 66.83 ya makadirio.
Fungu 45- Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
75.      Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 45 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa  shilingi bilioni 55.02 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 9.62 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 39.51 sawa na asilimia 71.81 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 3.18 sawa na asilimia 33.0 ya makadirio.

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI  KWA MWAKA WA FEDHA 2013/14

76.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, majukumu ya Wizara yatatekelezwa katika mafungu saba ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 - Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22 - Deni la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 - Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha na Fungu 7-   Ofisi ya Msajili wa Hazina.       Aidha, Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo inajitegemea litaendelea kuombewa fedha Bungeni na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa Sheria.

Mapato
77.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara ya Fedha inakadiria kukusanya mapato yasiyo ya kodi yapatayo shilingi  2,718,102,000 (bilioni 2.72) kupitia Fungu 50 - Wizara ya Fedha na shilingi  124,013,512,000 (bilioni 124.01) kupitia Fungu 7-   Ofisi ya Msajili wa Hazina.        





Maombi ya Fedha
78.      Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza kwa kina utekelezaji wa majukumu na kazi za Wizara kwa mwaka 2012/13 na mpango na malengo ya bajeti kwa mwaka 2013/14,  sasa napenda kuwasilisha rasmi mapendekezo ya maombi ya fedha kwa mwaka 2013/14 kwa ajili ya matumizi ya Fungu 50, 23, 22, 21, 13, 10, 7, na  45 kama ifuatavyo:-

Fungu 50 – Wizara ya Fedha
79.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-

 (a)   Matumizi ya kawaida Shilingi 53,011,091,000 (bilioni 53.01). Kati ya hizo Mishahara ni shilingi 4,564,609,000 (bilioni 4.56) na matumizi mengineyo shilingi 48,446,482,000 (bilioni 48.45).

 (b)  Miradi ya Maendeleo Shilingi 233,669,169,000 (bilioni 233.67).  Kati ya hizo:-

(i)     Fedha za Ndani - Shilingi 10,200,000,000 (bilioni 10.20).

(ii)    Fedha za Nje - Shilingi 223,469,169,000 (bilioni 223.47).

Fungu 23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali:
80.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-

(a)       Matumizi ya kawaida - Shilingi 80,831,672,000  (bilioni 80.83). Kati ya hizo Mishahara shilingi 4,434,410,000  (bilioni 4.43) na matumizi mengineyo shilingi 76,397,262,000 (bilioni 76.40).


(b)        Miradi ya MaendeleoShilingi 4,755,547,000 (bilioni
        4.76)  Kati ya hizo:-
(i) Fedha za Ndani -Shilingi 400,000,000 (bilioni 0.40).

(ii) Fedha za Nje  -Shilingi 4,355,547,000 (bilioni 4.36).

Fungu 22- Deni la Taifa
81.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi  3,319,017,772,000 (bilioni 3,319.02). Kati ya hizo Mishahara ni shilingi 6,311,772,000 (bilioni 6.31) na matumizi mengineyo ni shilingi 3,312,706,000,000 (bilioni 3,312.71).

Fungu 21 - HAZINA:
82.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-

(a)       Matumizi ya kawaida Shilingi 1,378,142,566,000 (bilioni 1,378.14). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 2,632,424,000 (bilioni 2.63) na matumizi mengineyo shilingi 1,375,510,142,000 (bilioni 1,375.51) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya Idara na Taasisi zilizo chini ya Fungu hili, nyongeza ya mishahara ya Watumishi wa Serikali na matumizi maalum.

(b)       Miradi ya maendeleo ni shilingi 38,190,162,000 (bilioni 38.19).  Kati ya hizo:-

(i)                Fedha za Ndani- Shilingi 7,893,000,000 (bilioni 7.89)

(ii)              Fedha za Nje- Shilingi 30,297,162,000 (bilioni 30.30)



Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu:
83.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-

(a)   Matumizi ya kawaida - Shilingi 1,944,790,000  (bilioni        1.94).

(b)   Miradi ya Maendeleo, fedha za nje Shilingi 399,985,000 (bilioni 0.39).

Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
84.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2,064,424,000 (bilioni 2.06) kwa matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi 362,771,000 (bilioni 0.36) ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 1,701,653,000 (bilioni    1.70) ni matumizi mengineyo.
Fungu 7 –    Ofisi ya Msajili wa Hazina:
85.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-

(a)         Matumizi ya kawaida - Shilingi 38,088,142,000 (bilioni 38.08).   Kati ya hizo shilingi 303,192,000 (bilioni 0.30) ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 37,784,950,000 (bilioni 37.78) ni matumizi mengineyo.


(b)       Miradi ya Maendeleo - Shilingi 1,665,300,000 (bilioni 1.67)  Kati ya hizo:-

(i) Fedha za Ndani -Shilingi 600,000,000 (bilioni 0.60).

(ii) Fedha za Nje  -Shilingi 1,065,300,000 (bilioni 1.07).



Fungu 45: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
86.      Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-

(a)   Matumizi ya kawaida shilingi 57,406,414,000 (bilioni 57.40). Kati ya hizo mishahara ni shilingi  6,692,935,000 (bilioni 6.69) na matumizi mengineyo shilingi 50,713,479,000 (bilioni 50.71).

(b) Miradi ya maendeleo shilingi 21,449,100,000 (bilioni 21.45), kati ya hizo:-


(i)         Fedha za ndani shilingi 15,250,000,000 (bilioni 15.25).

(ii)        Fedha za nje shilingi  6,199,100,000 (bilioni 6.20).



HITIMISHO
87.      Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba ya bajeti ya Wizara inapatikana katika tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz) Aidha, naomba hotuba kama ilivyo kwenye kitabu  iingizwe kwenye “Hansard”.

88.        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*