SIRI MPYA YAFICHUKA KUUAWAWA KWA WANAJESHI WA TANZANIA DARFUR NCHINI SUDAN.

RAIS wa Sudan, Omar Bashir, amesema atachukua hatua zote za kuwasaka kwa kila hali watu waliohusika na tukio la kuwaua askari saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika Jimbo la Darfur Jumamosi iliyopita.

Mbali ya mauaji hayo, askari wengine 14 walijeruhiwa vibaya, huku mmoja wapo hali yake inaelezwa kuwa mbaya.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana, ilisema Rais Bashir alitoa kauli hiyo, baada ya kufan

ya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete kwa simu.
“Rais amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Bashir, kufuatia kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania, walioko katika ulinzi wa kimataifa wa amani katika Jimbo la Darfur na kumtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo,

“Katika mazungumzo ya viongozi hao, Rais Omar Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kumuahidi kuwasaka hadi kuwakamata wale wote waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema, Rais Bashir amemhakikishia Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini waliohusika ni wahalifu ambao lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon naye alimpigia Rais Kikwete simu na kumpa pole kutokana na tukio hilo.

Taarifa hiyo, ilisema hadi sasa hakuna kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na shambulio hilo, ingawa kumekua na kutupiana lawama baina ya vikosi vya kiserikali na vikundi vya waasi katika Jimbo la Darfur.

Mwishoni mwa mwaka jana, wanajeshi wanne kutoka Nigeria, waliuawa karibu na El Geneina magharibi mwa Darfur, ambapo pia inaelezwa na Umoja wa Mataifa kuwa wanajeshi wapatao 50 wameuawa tangu kikosi kianze kazi ya kulinda amani mwishoni mwa mwaka 2007.

SILAHA

Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema kuna uwezekano mkubwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), likafanya mabadiliko katika baadhi ya vipengele vyake.

Kwa mujibu wa sura namba sita ya mkataba wa UN, majeshi yanayolinda amani katika Jimbo la Darfur hayaruhusiwi kubeba silaha za kivita.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ali, alisema kutokana na shambulio hilo ni wazi kuwa UN itachukua hatua kuhakikisha kuwa wanajeshi waliopo Darfur wanajihami.

“Bila shaka, tukio hili litatoa tahadhari nyingine ikiwamo ya kujihami na hatari kwa kutumia sura namba saba, wataweza kujibu mapigo,” alisema Ali.

Naye, Ofisa Habari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi la Tanzania (JWTZ), Meja Joseph Masanja alisema lengo la majeshi ya kulinda amani ya UN, ni kutafuta suluhu ya amani na si kupigana vita kwenye Jimbo la Darfur.

MIILI KUWASILI

Kuhusu miili ya wanajeshi saba waliouawa kuletwa nchini, Ali alisema wanawasiliana na UN, kupata taarifa za uhakika za kuwasili miili hiyo.

“Ikumbukwe kuwa kikosi cha Tanzania kipo chini ya mwamvuli wa UN, hivyo shughuli zote zipo chini ya UN.

“Hatuna sababu ya kuficha, tunasubiri taarifa sahihi kutoka UN ndipo tuufahamishe umma, hadi sasa hatujaletewa taarifa inayoeleza siku ambayo miili hiyo itawasili,” alisema Masanja.

MAKAIDI

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Dk. Emmanuel Makaidi ameishauri Serikali kuwarejesha askari wa JWTZ, wanaolinda amani katika nchi za Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizungumza na MTANZANIA juzi, Dk. Makaidi alisema Serikali inapaswa kufanya hivyo, ili kuepusha uwezekano wa askari wa Tanzania kukumbwa na vifo vingine kutokana na mashambulizi yanayofanywa na vikundi vya waasi wa nchi hizo.

Alisema kazi wanayoifanya askari hao nchini Sudan, haina maslahi ya moja kwa moja kwa Tanzania na kwamba sababu zilizotolewa na JWTZ kuhusu vifo hivyo hazijitoshelezi.

“Sababu za vifo vya askari wetu zilizotolewa na jeshi ni za kitoto, hivi unawezaje kulinda bila silaha tena ugenini, eti umekwenda kulinda amani, hii ni sababu ya maana kweli?” Alihoji.

Alisema nchi isiburuzwe kwa kisingizio cha kulinda amani barani Afrika na kwamba ushinikizwaji wa aina hiyo ni matokeo ya nchi kuwa na sera mbaya ya mambo ya nje.

Sarah Mossi, Rachel Mrisho na Esther Mbusi (Dar es Salaam).
CHANZO MTANZAANIA

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.