SUMRY LATUMBUKIA MTONI NA KUUA TISA, 53 WAJERUHIWA

Na Willy Sumia, Katavi
KATIKA hali isiyo ya kawaida basi la kampuni ya Sumry limetumbukia mtoni na kuuwa watu tisa na kujeruhi abiria wapatao hamsini na tatu katika mto Iku uliopo katika kijiji cha Sitalike wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa sita usiku kuamkia Julai 5, 2013 basi hilo lilipokuwa likitokea mjini Sumbawanga kuelekea Mpanda mkoani Katavi likiwa na abiri waliokuwa wametoka Mbeya.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Katavi Emanuely Nnley alisema jana kuwa ajali hiyo ilihusisha basi aina ya Nissan Diesel lenye namba T909 AZT mali ya kampuni ya Sumry lililokuwa likiendesha na dereva aliyetajwa kwa jina na Stephano Chimane maarufu kwa jina la Ntungu.

Alisema basi hilo lilipofika katika daraja hilo lenye kona kali na mteremko dereva wake alishindwa kulimudu na kulenga daraja hali iliyosababisha tairi za nyuma kupanda juu ya ukingo na kudumbukia mtoni ambapo dereva wa basi hilo aliweza kutoka na kukimbilia kusikojulikana.

Alifafanua kuwa juhudi za uokoaji zilianza kufanyika usiku huo huo ambapo majeruhi 53 waliokolewa na maiti tisa za wanaume watatu na wanawake watano na motto mmoja wa kike ziliopolewa katika maji.

Alisema hali ya majeruhi inaendelea vizuri isipokuwa majeruhi watatu walikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Rukwa kwa matibabu zaidi na kufafanua kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kuliongoza gari, ubovu wa gari na wembamba wa daraja
Akizungumza na gazeti hili Afisa Mwandamizi wa SUMATRA mikoa ya Rukwa na Katavi, David Chiragi alisema basi hilo lilikuwa limeiba njia kwani leseni yake inaliruhusu basi hilo kufanya safari za Sumbawanga Kirando na siyo Sumbawanga Mpanda kwa mujibu wa leseni iliyotolewa mwezi Juni mwaka huu.

Alisema hata upana wa daraja ilipotkea ajali hiyo ni mdogo sana ambapo vipimo vinaonesha daraja hilo lina upana wa mita 3.5 (tatu na nusu) tu wakati basi lina upana wa mita nne na nusu hivyo kujenga mazingira ya ugumu wa dereva kulenga daraja inapotokea msukosuko wa aina yoyote hasa wakati wa usiku na hivyo kuwataka wakala wa barabara mkoani Katavi kuangalia namna ya kupanua daraja hilo na kuboresha eneo hilo.

Alisema katika kipindi cha Januari hadi July 2013 zaidi ya ajali tisa zimetokea katika daraja hilo zikihusisha magari makubwa saba na madogo mawili kutokana na madereva kushindwa  kumudu magari yao na kulenga daraja hilo.

Alisema pia basi hilo lina makosa ya kutembea nje ya ratiba, kuiba njia na kuzidisha abiria hivyo ofisi yake imechukua hatua ya kuvunja safari za mabasi ya kampuni ya Sumry za mchana na badala yake mabasi yote yataondoka Sumbawanga na Mpanda majira ya asubuhi pekee.

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wakiongea kwa tabu katika hospitali ya wilaya ya Mpanda jana walisema kuwa dereva wa basi hilo alikuwa akiendesha kwa mwendo wa taratibu sana tangu mwanzo wa safari hali iliyowapa shaka kuwa huenda alikuwa hajui kueondesha magari au basi hilo lilikuwa na hitilafu kwani waliondoka mjini sumbawanga majira ya saa kumi na moja jioni na kufika eneo hilo saa saba na nusu usiku tofauti na mwendo wa kawaida ambapo walitakiwa kufika saa nne usiku eneo hilo.

Kondakta wa basi lililopata ajali alisema kuwa dereva huyo alikuwa mgeni wa njia pia alikuwa hajazoea kuendesha mabasi aina ya Nissan Diesel hali iliyomlazimu kumuelekeza njia wakati wote wa safari lakini ilipofika eneo la mteremko wa mto Sitalike Iku alimueleza kuwa mbele kuna daraja jembamba na kona kali dereva huyo alibadili gia ikagoma na kuanza kuporomoka hadi mtoni.

Mkuu wa mkoa wa Katavi Dr Rajabu Rutengwe alitoa rambi rambi kwa wafiwa wote na kuwapa pole wahanga wa ajali hiyo mbaya kutokea tangu mkoa huo uanze.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA