YANGA SC NAYO KUNUFAIKA NA MAMILIONI YA AZAM YA TV WALIYOLAMBA SIMBA SC JANA, TAYARI WANA BONGE LA OFA MEZANI

Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 19, 2013 SAA 2:58 ASUBUHI 
WAKATI jana Simba SC imeingia Mkataba wa miaka mitatu na Kampuni mpya ya Habari nchini, Azam Media Group, kwa ajili ya kipindi cha Televisheni, wenye thamani ya Sh. Milioni 331, imebainika wapinzani wao wa jadi, Yanga SC wameikalia ofa kama hiyo kutoka kampuni hiyo inayomilikiwa na bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
Vyanzo kutoka Azam Media vimesema kwamba, kampuni iliandaa Mkataba sawa kwa klabu hizo na kupeleka ofa kwa wakati mmoja, lakini Simba SC wakajibu na jana wamemalizana, wakati Yanga SC hadi sasa wapo kimya.
Lakini Azam wanaisubiri Yanga SC wakati wowote ikiwa tayari nao watapewa Mkataba mnono kama huo wa mamilioni.
Mtani kalamba bingo; Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage akikumbatiana na Wakili wa Azam, Shani Chrstoms baada ya kupewa Mkataba mnono. Wengine kulia ni Mzee Said Mohammed na Abubakar Bakhresa.

BIN ZUBEIRY ilimtafuta Katibu wa Yanga, Lawrence Mwalusako ambaye alisema kwa upande wa timu hiyo suala la Mkataba wa TV lilikuwa linashughulikiwa na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga ambaye hakupokea simu alipopigiwa kuzungumia suala hilo.
Mkataba wa Simba yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam unahusu kipindi maalum cha klabu hiyo, kitakachojulikana kama Simba TV Show ambacho kitarushwa katika kituo kipya cha Televisheni, Azam TV.
Ni matarajio pia Azam Media itafikia makubaliano na Yanga SC kwa ajili ya kipindi kama hicho ambacho kitatoa fursa kwa wapenzi wa timu hiyo kushuhudia programu za mazoezi ya timu, mahojiano ya wachezaji, makocha, viongozi na masuala mbalimbali ya maendeleo ya klabu. 
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage, kwa pamoja na Katibu, Evodius Mtawala na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini, Hamisi Kilomoni waliiwakilisha klabu hiyo katika utiaji saini wa Mkataba huo mnono kwenye ukumbi wa Kibo, jengo la PSPF, Dar es Salaam jana.
Upande wa Azam uliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Abubakar Bakhresa, Meneja Mkuu, Said Mohamed na Mwanasheria, Shani Christoms ambao waliikabidhi Simba SC hundi za fedha hizo kwenye hafla hiyo.
Meneja wa Azam Media, Mzee Said alisema kwamba Mkataba huo ni mwanzo tu, lakini kampuni hiyo imejipanga kusaidia zaidi soka ya Tanzania kwa kuingia mikataba mingi yenye manufaa kwa mchezo huo nchini.
Na hawa lini? Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji (wa pili kushoto) akiwa na Wajumbe wa Baraza la Wadhamini, kulia Balozi Ammy Mpungwe, kushoto kwake, Waziri George Mkuchika, Francis Kifukwe na Makamu Mwenyekiti Clement Sanga.  

Mzee Said alisema Azam Media inaleta mapinduzi na ukombozi katika medani ya michezo Tanzania na kwamba Watanzania wakae tayari kushuhudia mambo makubwa muda si mrefu kupitia Azam TV.
Alhaj Rage, pamoja na kuwashukuru Azam Media kwa Mkataba huo mnono, alisema klabu inategemea kujikomboa zaidi kiuchumi kutokana na mikataba ya udhamini kama hiyo na muda si mrefu wataingia mikataba mingine itakayokuza zaidi pato la klabu.
“Nimesikia pia mnataka kununua haki za Televisheni za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mimi nasema karibuni na katika hilo, natoa angalizo, mkinunua haki za TV za Ligi Kuu, naomba mtoe fungu sawa kwa kila klabu, hakuna kubagua eti huyu apate kidogo, yule apate zaidi, hapana,”.
“Lazima mpira wa miguu katika nchi hii maendeleo yafike kila sehemu na tuondoe ubinafsi wa kujifikiria eti sisi Simba ndiyo tupate zaidi, hapana. Hiyo si haki, lazima na zile klabu ndogo pia nazo zinufaike sawa na sisi kwa kuwa tunacheza ligi moja,”alisema Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM).

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.