CHASO IRINGA WATOA TAMKO KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA

Wanachaso wakiwa katika picha ya pamoja
 Katibu Mwenezi wa Chaso Iringa, Michael Noel akizungumza kushoto kwake ni mwenyekiti wa chaso mkoa wa Iringa Thimotheo Mkanyia.
 baadhi ya viongozi wa chaso kutoka katika vyuo vikuu vilivyoko mkoa wa Iringa wakiwa katika ofisi za chama hicho.

========  ========  ========
CHASO IRINGA WATOA TAMKO KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA

Na Denis Mlowe.

JUMUIYA ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Wanachadema Mkoa wa Iringa (CHASO) wamelaani vikali mwenendo mbovu wa Bunge Maalum la Katiba katika kuendesha na kujadili rasimu ya katiba tangu lilipoanza kwa kuendesha malumbano kila kwenye kikao na wakati mwingine wajumbe kuzomeana na kuacha kujadili mambo ya msingi yanayowagharimu Watanzania mamilioni ya Fedha.

Wakitoa msimamo mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Chaso zilizoko Tumaini katika kata ya Kihesa jana, Katibu Mwenezi wa Chaso Iringa, Michael Noel alisema bunge la katiba limepoteza imani kwa wananchi na wamekuwa wakilipwa posho kwa kodi zetu, wanataka watupatie katiba ya msimamo wa chama cha mapinduzi.

Alisema kuwa chaso haiko tayari kuona mawazo ya wananchi katika rasimu ya katiba yanapotoshwa kwa misingi ya faida ya chama kimoja hivyo wako tayari kuandamana nchini nzima endapo ccm watapitisha katiba yenye msingi ya maslahi ya chama chao.

Alifafanua kuwa wajumbe wa vyama vya siasa vya upinzani wamekuwa wakibaguliwa na wakati mwingine kutosikilizwa hoja zao hata kama za msingi kwa kuwa hawafungamani na chama cha mapinduzi.

“ Hata wenyeviti wa kamati nyingi za bunge hilo ni wa ccm kitu kinachowasaidia kuchakachua kanuni ili kuwarahisishia kutekeleza dhamira yao ya kubadilisha vifungu vya rasimu hasa mfumo wa muungano ambao umependekezwa na tume kupitia maoni ya wananchi” alisema Noel

Aliongeza kuwa kuna tuhuma za rushwa zinazosikika kila kukicha lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa wajumbe wanaotuhumiwa na tuhuma zote hizi ni dhidi ya wajumbe wa ccm wakiwamo mawaziri wa serikali na kuhoji wanafanya hivyo kwa dhamira ipi?

Noel alisema wajumbe wa bunge hilo wanatakiwa kutambua kuwa waamuzi wa mwisho ni wananchi hivyo ccm isitumie hila kuwachagulia katiba waitakayo kwa maslahi ya chama hicho na kuongeza watahamasisha wananchi popote walipo waikatae kama rasimu hiyo itachakachuliwa na kubeba msimamo wa ccm uliotangazwa na katibu mwenezi Nape Nnauye.

Alisisitiza kuwa maoni ya wananchi yazingatiwe na hawako tayari kuona chama tawala wakipuuza na kujiona wao wana hisa juu ya mfumo wanaoutaka.

“Chama cha Mapinduzi kisijidanganye kuwa mchakato huu wakiuvuruga tutaendelea kuitumia katiba iliyopo iliyosababisha taifa makovu makubwa yanayoendelea kututafuna bali watasababisha taifa kuingia katika machafuko ambayo kama busara ikitumika tunaamini katiba mpya itapatikana kwa utulivu na amani.” Alisema Noel

Alisema msimamo wa chaso kuunga mkono mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya katiba ambayo maoni yake yametolewa na wananchi walio wengi.

Aidha Noel amesema wamesikitishwa na hotuba aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete wakati akifungua bunge maalum kwa kuendeleza msimamo wa ccm kwa kutaka mawaziri watokane na wabunge.

Akifafanua alisema hotuba ya Kikwete ni kupigiria msimamo wa ccm na kukejeli maoni ya wananchi ambao ndio waliomuweka madarakani kunaashiria usaliti mkubwa kwa wananchi walioamua namna mfumo mzuri wa kuendesha nchi.
 
“Itambulike kuwa serikali iliyopo madarakani ni ya CCM lakini Tanzania na maisha ya watu wake siyo mali ya CCM, hivyo kitendo cha kuwalazimisha wananchi juu ya hatima ya nchi yao kinachofanywa na CCM hakikubaliki. Kama tunataka katiba bora lazima ibebe maoni na matarajio ya wananchi na ndio maana tuanaza na maneno ‘Sisi wananchi’ na sasa kama CCM haikubaliani na maoni ya wananchi maana yake katiba ianze na maneno ‘Sisi CCM’ kitu ambacho hakikubaliki” alisema Noel

Noel alisema kazi ya bunge maalum la katiba siyo kubadilisha bali ni kuboresha kwamba mambo gani yanapaswa kuingizwa ama kutolewa ndani ya mfumo wenyewe na kutolea mfano mambo ya muungano na yasiyo ya muungano na vyanzo vya mapato.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI