Ndege ya CRJ-200 yaboresha utendaji wa ATCL, yarejesha imani kwa abiria

Ndege ya Shirika la ndege la Air Tanzania aina ya CRJ-200, yenye uwezo wa kubeba abiria 50, ikiwa imetua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe mkoani Mbeya hivi karibuni 
=====  =======  ===
SHIRIKA la Ndege la Air Tanzania limeweka rekodi ya ongezeko la abiria kwa asilimia 57 wiki chake baada ya kupokea  ndege ya kukodi yenye uwezo wa kubeba abiria 50 aina ya CRJ-200 pamoja kuiongezea uwezo wa kuruka kwa wakati kwa asilimia 98.

Aidha, shirika hilo limeweza kutoa nauli maalum kwa sikukuu za Pasaka kwa abiria wa mkoani Mtwara ambao kwa sasa watakuwa wakilipa shilingi 250,000/- ikijumuisha kodi zote, kwa tiketi ya kwenda na kurudi.

Hayo yalidhihirishwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lazaro, wakati akitathmini utendaji wa kipindi kifupi wa ndege hiyo iliyokodishwa pamoja na kuangalia mchango wake wakibiashara katika shirika hilo.

Kapt. Lazaro alisema kwa ujumla, ujio wa ndege ya CRJ-200 mapema mwezi Machi mwaka huu umesaidia kuboresha utendaji na kufikia kiwango cha juu, hali inayoipa uongozi wa shirika sababu za kujivunia kwa maamuzi yao ya kukodisha ndege hiyo.

“Inabidi nikubali kuwa ndege imepokelewa vizuri na wateja wetu. Ndani ya wiki chache tu ikiwa inafanyakazi, tumepata ongezeko kubwa la abiria wetu na huduma zetu zimeweza kuaminika zaidi na wateja wetu wengi. Kwa maana hiyo, matokeo yamekuwa ni mazuri sana,” alisema Kapt. Lazaro.

Alibainisha kuwa kinyume na taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari vikidai kwambandege iliyokodishwa ya CRJ-200 ni mzigo kwa shirika ikilinganishwa na ndege yake aina yaBombardier Dash-8, ndege hiyo mbali na kuimarisha utendaji wa ATCL, pia imeisaidia shirika kuokoa fedha na muda.

“Hatutajitendea haki sisi wenyewe au kwa waliyotukodishia ndege hiyo kama tukiruhusu sisi wenyewe tujiingize kwenye mjadala wa muundo wa gharama au mchango wake wa kimapato, kwa muda huu mfupi. Inatosheleza kusema kuwa lengo letu la kukodisha ndege hii ambalo lilikuwa ni kubwa kuliko mengine limefanikiwa,” Ofisa Mtendaji huyo mkuu alisema.

Kapt. Lazaro aliongeza kuwa, kuongezeka kwa idadi ya abiria wanaosafiri na Air Tanzania kumetokana na ukweli kuwa muda inayotumia ndege ya CRJ-200 kusafiri umekuwa mchache zaidi ukilinganisha na ndege nyinginezo  zinazosafiri njia hizo, kwa hivyo uokoa muda wa abiria na pia abiria wengi ufurahia huduma za ATCL wakiwa safarini.

“Mbali na muda mfupi wa kusafiri, ndege hiyo imeboresha zaidi utendaji wa shirika kwa asilimia 98. Ujio wa ndege hii umerudisha imani miongoni mwa abiria wetu ambao sasa wanauhakika wa kusafiria kwa kufuata muda uliyopangwa,” alisema.

Hivi karibuni shirika hilo la ndege la Air Tanzania lilizindua safari za kwenda katika mkoa wa Mbeya kwa kupitia uwanja mpya wa kimataifa wa ndege wa Songwe ikitumia ndege yake ya CRJ-200.

Dakika 58 za safari kati ya Dar es Salaam na Mbeya, ambayo imepangwa kuwa siku nne kwa wiki; Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili, imepokelewa vizuri na abiria na wafanyabiashara wanaosafiri toka Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam.

Taarifa za awali kutoka katika shirika hilo zilisema kuwa abiria sasa watafurahia safari za kila siku za kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, mara nne kwa wiki kwenda Mbeya na itakuwa inasafiri kwenda Comoro katika siku za Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.

Shirika hilo pia limefuta adhabu zinazotozwa kwa abiria wanaoshindwa kusafiri na wale wanaobadilisha safari zao, ili kuwasaidia abiria wao kutoingia gharama za ziada pale wanapopatwa na dharura kabla ya kusafiri.
“Hatuamini kabisa katika kuwaadhibu abiria wetu wapendwa,” alisema Kapt. Lazaro.

Mkakati wa utanuzi wa shirika hilo la ndege la taifa ni pamoja na kufungua njia ya Tabora – Mpanda pamoja na kurejesha njia zake zote za zamani.
Kwa sasa ATCL inasafiri katika maeneo 8 nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na Mtwara, Mwanza, Tabora, Kigoma, Dar es Salaam, Mbeya, Bujumbura na Moroni nchini Comoro.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI