STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 31 Machi, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
leo amefanya mazungumzo na ujumbe wa Umoja wa Ulaya-EU ambapo
wamezungumzia masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano kati ya
jumuiya hiyo na Zanzibar.
Katika
mazungumzo hayo Dk. Shein ameishukuru Jumuiya ya Ulaya kwa misaada yake
mingi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kuwa misaada
hiyo imekuwa chachu katika kuongeza kasi ya kuleta maendeleo nchini.
Aliueleza
ujumbe huo ulioongozwa na Mwakilishi wa Umoja huo katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Balozi Filiberto Ceriani Sebregondi kuwa Serikali
na wananchi wa Zanzibar wanathamini sana ushirikiano wake na Umoja wa
Ulaya na wametiwa moyo kuona Umoja huo umekuwa wakati wote ukiziunga
mkono jitihada zao za kuijenga Zanzibar.
Baadhi
ya misaada inayotolewa na Umoja huo ni pamoja na msaada katika bajeti,
sekta ya nishati hususan utafutaji wa nishati mbadala, marekebisho
katika sekta ya sheria, uimarishaji wa taasisi zinazoshughulikia masuala
ya demokrasia, utamaduni na pamoja na mradi wa kijamii katika kupiga
vita ukatili dhidi ya watoto.
Dk.
Shein ameuhakikishia ujumbe huo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Jumuiya hiyo na wanachama
wake kwa kuwa Umoja huo na wanachama wake ni marafiki wa kweli wa
Zanzibar na watu wake.
Wakati huo huo Mwakilishi
wa Umoja huo nchini, Balozi Filiberto Ceriani Sebregondi mbali ya
kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumpa fursa yeye na ujumbe wake kukutana
nae alieleza kuwa mazungumzo kama hayo yanatoa nafasi ya kubadilishana
mawazo na viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujifunza
kutoka kila upande kuhusu namna bora ya kuimarisha na kuendeleza
ushirikiano wao.
Alieleza kuwa wakiwa Unguja wataonana na watu mbalimbali na ziara yao hiyo itawapeleka hadi kisiwani Pemba kujionea hali halisi ilivyo kisiwani huko.
Mazungumzo
hayo yalihudhuriwa na Naibu Mwakilishi wa Umoja huo Bwana Tom Vens na
mabalozi wa nchi wanachama wa Umoja huo nchini ambao ni Ubelgiji,
Ufaransa, Ujarumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Hispania, Sweden na
Uingereza.
Comments