BAADA
ya kampeni zilizodumu kwa mwezi mmoja, hatimaye uchaguzi mdogo wa Ubunge
katika Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo, Pwani unatarajiwa kufanyika
leo ili kumpata mrithi wa Said Bwanamdogo aliyefariki dunia Januari 22
mwaka huu kutokana na maradhi.
Katika
kipindi chote cha kampeni, vyama vitano vilichuana kumwaga sera na
usiku na mchana katika Kata 15 za jimbo hilo, kila kimoja kikiamini
ndicho kitaibuka mshindi na hatimaye kutoa mrithi wa Bwanamdogo.
Vyama
hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachowakilishwa na Ridhiwani
Kikwete, Chadema ambacho mwakilishi wake ni Mathayo Torongey na Chama
cha Wananchi (CUF) kinachowakilishwa na Fabian Skauti.
Vingine ni AFP ambacho mpeperusha bendera wake ni Ramadhani Mgaya na NRA kinachowakilishwa na Munir Hussein.
Kwa
mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Chalinze ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo, Christina Njovu,
maandalizi yote ya uchaguzi huo mdogo yamekamilika.
Alimwambia
mwandishi jana kuwa, Jimbo la Chalinze lina vituo vya kupigia kura 288
ambavyo pia vilitumika katika uchaguzi wa mwaka 2010 na kwamba
wasimamizi wa uchaguzi wako tayari kwa kazi hiyo, huku akisisitiza
waliojiandikisha na kutambuliwa katika daftari la wapiga kura katika
jimbo hilo ni wapiga kura 92,588.
Naye
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei amesema na
kutahadharisha wananchi watakaopiga kura kufanya hivyo na baadaye
kuondoka eneo la kupiga kura umbali wa zaidi ya meta 100.
Alisema
kazi ya ulinzi na usalama katika vituo vyote ni kazi ya jeshi la polisi
na sio mtu ama kikundi chochote kiwe cha siasa ama sio cha siasa na
iwapo hilo litazingatiwa uwezekano wa upigaji kura na utangazaji matokeo
ukawa wa amani na utulivu.
Comments