ZITTO ZUBERI KABWE AELEZA KUWA KITAKACHOVUNJA MUUNGANO SI SERIKALI TATU BALI NI......!!!.


 Mjumbe wa Bunge la Katiba, Zitto Kabwe.

Dodoma. 

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Zitto Kabwe amesema kuandikwa kwa Katiba isiyokubaliwa na pande zote kutasababisha gharama kubwa kuliko zile zinazotajwa za serikali tatu.
Akichangia hoja kwenye Bunge hilo jana, Zitto alisema kuna kila sababu ya kukaa na kukubaliana ili kupata Katiba itakayokubalika pande zote.


“Muundo wa Muungano una hatari ya kuvunjika iwapo hakuna matakwa ya dhati ya watu kuungana... Maneno ya kusema Serikali tatu zitavunja Muungano ni ya siasa na hayana msingi wa kisayansi. Urusi ilivunjika sababu haikuwa na demokrasia na siyo sababu ya idadi ya Serikali,” alisema.


Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema hofu ya gharama inayotajwa katika uendeshaji wa muundo wa serikali tatu haina msingi wowote kwa kuwa hakuna ushahidi wa kitaalamu unaothibitisha gharama hizo.


“Nimesikia watu wanasema eti tutalazimika kujenga ikulu mpya, nani kasema lazima tuwe na marais watatu? Tunaweza kuwa na rais mmoja kwenye nchi na wakuu wa nchi washirika wawili… Ni jambo la makubaliano tu,” alisema.


Alisema bajeti ya mwaka huu ni Sh18 trilioni, kati ya hizo Sh5.3 trilioni ndizo zinazohudumia wizara za Muungano, lakini serikali ina uwezo wa kukusanya kodi zaidi ya Sh10 trilioni pamoja na mapato mengine.


“Kuna jumla ya Sh2.3 trilioni hatuzikusanyi kila mwaka kutoka kwenye kampuni kubwa, kwa uwezo wetu wa pato la ndani asilimia 17 tunao uwezo wa kuendesha serikali ya muundo wa idadi yoyote.


“Hofu ya Serikali ya Muungano kutokuwa na fedha ni sababu halisi, ni kweli kwamba ushuru wa bidhaa pekee yake hauwezi kutuendeshea serikali. Sasa nini kazi yetu, tunaingia hapa ili kuboresha hayo maeneo, kama hatuwezi tumekuja kufanya nini hapa?” alihoji.


Jussa akomaa
Mjumbe wa Bunge hilo, Ismail Jussa jana alisisitiza kwamba Wazanzibari wengi hawapo tayari kuendelea na mfumo wa serikali mbili kwa sababu unawatesa na kuwadhalilisha.


Jussa ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia CUF, alisema haoni haya kuzungumzia suala hilo kwa niaba ya Wazanzibari.


“Hoja nyingi zimetoka (kuhusu Muungano), lakini naendelea kuzungumza kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar na katika hili sioni haya kwa sababu naamini kwamba wanakisimamia kile ambacho sisi tunasimamia nacho ni Zanzibar yenye mamlaka kamili,” alisema Jussa.MWANANCHI

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU