JK ASIFU UHUSIANO WA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesifia uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini akisema kuwa uhusiano huo haujapata kuwa mzuri zaidi ya ulivyo sasa.


Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Afrika Kusini kuendelea kuonyesha uongozi katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa sababu kwa kufanya hivyo Afrika Kusini itakuwa inatimiza jukumu lake la kihistoria.


Rais Kikwete alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam wakati anaagana na Balozi wa Afrika Kusini katika Tanzania Mheshimiwa Thanduyise Henry Chiliza ambaye amemaliza muda wake wa utumishi nchini.


Rais Kikwete alimwambia Balozi huyo kuwa ni nchi chache dunia kwa sasa ambazo zina uhusiano wa karibu zaidi na Tanzania kuliko Afrika Kusini. “Tumekuwa washirika wa karibu sana katika uhusiano wa kikanda na uhusiano wa kimataifa. Uhusiano wetu haujapata kuwa wa karibu zaidi ya sasa katika historia. Tunakushukuru Mheshimiwa Balozi kwa mchango wako katika kuimarisha uhusiano wetu kiasi hicho.”


Rais Kikwete pia amesifia mchango wa Afrika Kusini katika utulivu ulioko katika eneo la Kusini kwa Afrika akisema kuwa anatambua mchango na uongozi wa nchi hiyo katika hali hiyo. 


“Tunatambua uongozi wa Afrika Kusini katika eneo letu la Afrika. Ni jukumu la kihistoria la nchi hiyo ambalo Afrika Kusini lazima iendelee kulitimiza kwa kiwango kinachotarajiwa na sisi wote.”


Naye Balozi Chiliza amemshukuru Rais Kikwete kwa kumuunga mkono wakati wa uwakilishai wake na hivyo kumsaidia kutimiza majukumu yake ya kibalozi. “Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ushauri na maelekezo yako ya kiuongozi wakati wa utumishi wangu katika Tanzania. Bila kunisaidia pengine kazi yangu ingekuwa ngumu zaidi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
2 Julai, 2014

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU