SUMAYE AFICHUA SIRI YA MIRADI MINGI INAYOKUWA MIBOVUMIBOVU, TAYARI WAKUBWA WA NCHI YA TANZANIA WAMECHUKUA PASENTI YAO.


Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye akihutubia wakati akizindua Kituo cha Maendeleo ya Vijana(TYDC) jijini Mwanza jana. Picha na Michael Jamson 

Mwanza.
 

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye jana aliamua kutoa ya moyoni wakati alipobainisha kuwa kujengwa kwa kiwango cha chini kwa miradi mingi, kunatokana na wakubwa kupewa ‘pasenti’ za rushwa na kampuni zinazoshinda zabuni hizo.

Sumaye, ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu, alisema hayo jana katika Chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza wakati akizindua kikundi cha vijana kinachoitwa Tanzania Youth Development Centre (TYDC), tawi la Mwanza.


“Hii ni rushwa ya ulafi. Hii wananchi wanaweza wasiione moja kwa moja, lakini ina maumivu makali na mabaya ya muda mrefu kwa nchi,” alisema mtendaji huyo mkuu wa zamani wa serikali.


“Hii ni rushwa ya wakubwa wanaotoa uamuzi kwa miradi mikubwa ya taifa na muhusika anawekewa asilimia zake fulani za gharama za mradi kama fedha zake binafsi na fedha hizi au chochote walichokubaliana wakapeana kwa utaratibu wowote watakaokubaliana,” aliongeza Sumaye.


“Hapa lazima mradi husika utajengwa chini ya kiwango kwa sababu kubwa mbili; kwanza, sehemu ya fedha za mradi zimeingia mfukoni mwa mtu kwa hiyo ili zilizobaki, ni lazima zitakuwa za kurashiarashia mradi; pili; ambaye angesimamia mradi huo anafumbwa macho, haoni tena, amezibwa masikio hasikii tena na amefungwa mdomo hasemi tena.


“Rushwa hii ina gharama kubwa kwa uchumi kwa sababu miradi tunayokopea fedha nyingi au hata kama ni fedha zetu, inashindwa kukamilika kwa wakati au inakamilishwa tu, lakini haina maisha marefu kama ambavyo ilitegemewa.”


Sumaye ambaye hakuweka bayana miradi hiyo, alisema:
“Hasara nyingi ni kuwa zile kampuni zenye uwezo wa kufanya kazi bila rushwa haziwezi kupata kazi kwa sababu ya kuzidiwa ujanja na watoa rushwa. Hili nalo ni la hatari sana kwa uchumi wetu.”


Dawa za kulevya
Akizungumzia dawa za kulevya, Sumaye, ambaye ni waziri mkuu mstaafu pekee aliyeshika wadhifa huo kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, alisema biashara ya dawa za kulevya hufanywa na watu wazito ama kwa fedha zao au kwa madaraka yao.


Alisema kwa sasa Tanzania inaonekana kuwa kituo muhimu cha kupitishia dawa hizi kwenda na kutoka nchi nyingine.


“Hii siyo sifa nzuri kwa nchi yetu... ukiachilia mbali madhara ya kupitishia nchini mwetu, dawa hizi huathiri vijana na kuwageuza mazezeta kwa baadhi ya wanaotumia.”


Sumaye alisema kinachotisha zaidi ni uhalifu unaofanywa kwa vijana kwa kuwatumia kama kontena la kubeba dawa na zaidi ni kuhatarisha maisha yao. “Wapo wengi waliopoteza maisha kwa njia hii,” alisema.


Biashara ya dawa za kulevya imekuwa ikihusishwa na vigogo ambao ni wanasiasa na wafanyabiashara, lakini hadi sasa hakuna mtu maarufu aliyefikishwa mahakamani zaidi ya wahusika kusema wana orodha ya wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.


Sumaye, ambaye aliteuliwa kuwa mlezi wa taasisi hiyo, aliahidi kupambana na vitendo hivyo viovu.


“Nimeamua kuwa mlezi wa vijana wote Tanzania.
Nitakemea vitendo vyote viovu niwe madarakani au nisiwe madarakani. Nitapambana kwa nguvu zangu zote kuhakikisha vitendo viovu vinakomeshwa,” alisema.


“Katika uhalifu kama wa dawa za kulevya, wanaotumiwa kuyabeba ni vijana. Kwa hiyo vijana wakiamua kuwa hakuna tena kutumika kama makontena wanaweza. Vijana mkiamua kuwa hakuna kujihusisha au kutumwa katika ujambazi, ujambazi utafutika au kupungua sana.”


Urais 2015
Sumaye, ambaye alikuwa mmoja wa makada wa CCM waliopigwa kufuli na Kamati Kuu ya CCM kutojihusisha na vitendo vya kampeni kabla ya muda, alisema kama Watanzania watamuomba kugombea urais mwakani, yupo tayari kufanya hivyo kwani suala hilo halina tatizo kwake. Alisema Kanuni za CCM hazimzuii mwanachama wa chama hicho kutangaza nia, bali inazuia kufanya kampeni kabla ya muda.


Hata hivyo, Sumaye alisema kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwarubuni vijana kwa kuwaahidi kuwapa nafasi za uongozi wakati wakifahamu hawawezi kufanya hivyo.


Awali, Sumaye alitaka ieleweke kuwa umoja wa vijana wa TYDC ni mchanganyiko wa itikadi zote, kwa kuwa unahusisha vijana wa CCM, Chadema, CUF, TLP, NCCR Mageuzi na vijana wasiokuwa na chama chochote cha siasa.


Kuhusu vijana hao, Sumaye alisema wana jukumu la kupanga aina ya nchi wanayotaka kuishi, kwani ujana una maslahi kwa maisha yao yaliyobaki ambayo ni miaka mingi ijayo.


“Naomba niseme kwamba vijana ndiyo waamuzi wa kiongozi wanayemtaka, anayeweza kuwasaidia kubadilisha maisha yao. Siyo vyema kuwadanganya kwa kuwapa fedha au kuwaahidi vyeo. Kinachotakiwa ni kuwasaidia kuwatafutia fursa za kuwajengea uwezo wa kujiajiri ili wajipatie maendeleo,” alisema Sumaye.


Sumaye alisema sasa ni kipindi cha uchaguzi, hivyo fedha nyingi zinatembea hasa kwa vijana ili mtoa fedha aweze kuchaguliwa kwenye nafasi anayoomba.


Alisema watu hao ambao wamekuwa wakitoa fedha ili kuchaguliwa, wameamua kuweka na majina ya utoaji fedha hizo ili kuhalalisha uovu huo, kwani wana malengo ya kununua wapiga kura na wanaitwa wakarimu, wasiotoa huitwa wachoyo.


“Ni jambo la kusikitisha kuona watu wanahalalisha hadi majina ya utoaji rushwa kwa sababu tu ya kutaka kununua wapiga kura, inawezekana kabisa wapo vijana ambao wameingia kwenye mtego huo mbaya, wanadanganywa kupewa rushwa au cheo lakini ni vyema wakajiuliza kwamba vyeo hivyo vitawatosha wangapi?” alisema Sumaye.


Alisema siku zote mtu ambaye hatoshi kwenye nafasi anayotaka, lazima atatumia kigoda kufikia anapotaka, ndiyo maana wanahangaika kutoa fedha na kwamba mbaya zaidi mtu huyo akiingia madarakani lazima ataweka maslahi yake binafsi mbele.


Sumaye aliwataka vijana walio chini ya mwavuli wa TYDC kuhakikisha kuwa wanatoa elimu ya kutosha kwa vijana zaidi ili wawe jeshi lenye utii kwa jamii na kuwa jeshi lisilokubali kutumika kwa maslahi binafsi.


“Vijana nawaomba nyote muwe wazalendo wa kweli kwa nchi yenu. Ninyi ndiyo taifa la leo na litakalokuwepo kesho na muhimu zaidi lenye uwezo wa kujenga nchi muitakayo.


Tusikubali kudanganywa tukaharibu nchi yetu kwa shida za muda mfupi,” alisema.


Alalamikia hujuma
Akizungumza mapema kabla ya kusoma hotuba yake, Sumaye alilalamika kuhujumiwa na baadhi ya watu.


“Kuna baadhi ya watu ambao walipata taarifa kwamba nipo huku na wakaanza kunifanyia vitimbwi,” alisema Sumaye huku akigoma kueleza vitimbwi hivyo kwa madai hayupo kwenye mkutano wa kisiasa.MWANANCHI

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI