WIZI MPYA WA KUIBA WATOTO WAIBUKA, NDANI YA WIKI HUIBWA WATOTO WANNE JIJINI DAR ES SALAAM.


Mtoto aliyeibwa, Merryn Reppyson

MTINDO mpya wa kuiba watoto jijini Dar es Salaam, umezusha hofu kwa wazazi na walezi hali inayofanya baadhi yao kuhofia kutoka nyumbani na kuwaacha watoto wao na wasichana wa kazi.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini katika kipindi cha wiki moja, watoto wanne wameibwa na watu wasiojulikana na kutokomea nao katika mazingira ya kutatanisha.

Moja ya tukio ambalo linaendelea kuvuta hisia za watu wengi ni lile lililotokea eneo la Changanyikeni karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, Merryn Reppyson (3), alipotea Julai 15, mwaka huu baada ya mtu asiyejulikana kumchukua kutoka nyumbani kwao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mama mzazi wa Merryn, Elida Fundi, alisema mtu aliyemuiba mtoto wake alifika nyumbani kwake na kuomba kwenda msalani.

Elida alisema alipokutana na dada wa kazi mlangoni mtu huyo alimuulizia Merryn na wazazi wake.

Alisema baada ya mtu huyo kufika ndani ya nyumba aligonga mlango akidhani kuwa mtoto yupo peke yake, lakini baada ya kugonga na kusikia sauti ya mtu mzima ikimkaribisha alilazimika kuomba kuingia msalani.

“Huyu mtu alivyokuwa akiingia getini kwangu alipishana na dada mlangoni, alihisi mtoto atakuwa ndani peke yake, baada ya kukuta kuwa ndani kuna mtu mwingine tofauti na dada aliyepishana naye getini, alilazimika kuomba kwenda msalani.

Dada aliyekuwa pale nyumbani alimuelekeza choo cha nje, alivyotoka huko alikuta mtoto akiwa pale nje akamchukua na kuondoka naye, hicho kilikuwa ni kitendo cha kama dakika tano tu.

Nimechanganyikiwa kabisa hapa, mtoto ameibwa na hatujampata mpaka sasa, aliyemuiba anaonekana anatufahamu kwa sababu dada anasema alikuwa anakuja siku moja moja hapa nyumbani na kutuulizia mimi na mume wangu wakati anajua muda huo tunakuwa kazini.

Lakini pia alikuwa anamfahamu mtoto wangu mpaka kwa jina, akija hapo anakuwa anamuita kabisa kwa jina, anamuuliza mama yupo? Baba yupo,” alisema Elida.

Alisema kuwa mtu aliyemuiba mtoto huyo alifika nyumbani kwake kwa siku tatu tofauti na siku ya tatu ndipo alipomuiba.

Alifafanua dada aliyemkaribisha mtu huyo, alishangaa baada ya kuona mtu aliyeomba kujisaidia ameondoka bila kuaga.

Alieleza pia kuwa dada huyo alishangaa kutomuona mtoto nje hata hivyo, akajipa matumaini kuwa atakuwa ameingia chumbani.

“Dada wa kazi ambaye alikuwa amepishana na yule mgeni getini, aliporudi nyumbani alimuulizia Merryn kwa kuwa hakumuona ndipo walipoanza kumtafuta huku wakiwauliza majirani ambao walidai alipita na mjomba wake ambaye alikuwa anaenda kumnunulia ndizi,” alisema.

Alisema wakati wakiendelea kumtafuta mtoto huyo walifika kwenye genge lililo karibu na nyumba yake na kuambiwa kuwa mtoto huyo alifika hapo na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mjomba wake na kumnunulia ndizi kisha wakaondoka.

“Tukio hili limenishangaza kwa kuwa hatujawahi kugombana na mtu, itakuwa tu wamemchukua ili kututisha au tuwape pesa, lakini hatuna ugomvi na mtu,” alisema Elida.

Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo ambalo limeripotiwa katika kituo cha polisi cha Changanyikeni, mpaka sasa hakuna taarifa zozote zilizotolewa zinazohusiana na upatikanaji wa mtoto huyo.

Alisema majibu ambayo wamekuwa wakiyapata kutoka polisi ni kuwa uchunguzi bado unaendelea.

Wakati matukio hayo yakiendelea msichana, Islam Yasin (16), amepotea katika mazingira ya kutatanisha uko Mbezi Msakuzi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Islam ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mpigi Majohe, alipotea tangu Julai mosi hadi sasa hajulikani alipo.

Taarifa za kupotea kwake zimeripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Mbezi kwa Yusuf na kufunguliwa jalada lenye kumbukumbu ya RB/6451/2014.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mama mzazi wa binti huyo, Conses Buberwa, alisema katika kipindi cha wiki mbili wamekuwa wakimtafuta binti yake bila mafanikio.

Alisema yeyote mwenye taarifa za kupotea kwa msichana huyo atoe taarifa katika kituo chochote cha polisi kilichopo jirani naye au apige simu namba 0657004332.

Siku ya tukio, Islam alikuwa amevaa blauzi nyekundu na kubeba kanga doti moja za aina tofauti ambazo alizihifadhi kwenye mkoba wake.

Kauli ya Polisi
Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo huku akisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wake.

“Ni kweli tumepata taarifa hizo tunazifanyia kazi ili tuweze kujua ni kina nani waliowaiba watoto hao, lakini bado ninaendelea kukusanya matukio ya aina hii kutoka katika vituo vyote vya polisi ili tuweze kubaini ukubwa wa hali ya matukio haya,” alisema Wambura.

Waziri Simba
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, aliliambia gazeti hili kuwa wizi huo unatokana na wazazi kutokuwa makini katika masuala ya ulinzi kwa watoto.

“Jukumu la wizara ni kulinda haki za watoto, ulinzi wa mtoto binafsi ni kazi ya mzazi Serikali haiwezi ikaweka polisi kila nyumba yenye watoto kwa ajili ya ulinzi,” alisema Waziri Simba.

Alisema hivi sasa wazazi wamekuwa hawana muda na watoto wao na hata kushindwa kufuatilia taarifa za watoto wao.

“Serikali itaendelea kuwatafuta watu wanaofanya vitendo vya ukatili wa watoto na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) katika mikoa 18 ya Tanzania Bara na Visiwani, imebaini kuendelea kushamiri kwa vitendo hivyo huku matukio 996 ya udhalilishaji yakiripotiwa kutokea katika wilaya sita za Zanzibar.

Kati ya matukio hayo, 242 yalihusu ubakaji, vipigo vilikuwa 388, ndoa za utotoni 42, kutelekezwa 96, mimba za utotoni 228, ambapo kwa upande wa Tanzania Bara ukionyesha kuwa Wilaya ya Babati mkoani Manyara inaongoza ikiwa na matukio 132.

Ripoti ya Utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto Tanzania, iliyotolewa na Serikali pamoja na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) mwaka 2011, ilidhihirisha kuwa msichana mmoja kati ya watatu na mvulana mmoja kati ya saba nchini Tanzania hukumbwa na unyanyasaji wa kijinsia kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.MTANZANIA

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI