PHIRI APAA NA SKWADI ZIMA LA SIMBA SC ZENJI LEO, WAKIRUDI HUKO SASA…


Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
BAADA ya kocha Mzambia Patrick Phiri kusaini Mkataba wa mwaka mmoja jana, kikosi cha Simba SC kinakwenda kambini visiwani Zanzibar leo kuweka kambi rasmi ya kujiandaa na msimu.
Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva ameambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, kikosi kinaondoka asubuhi ya leo kwenda Zanzibar na kitarejea siku chache kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu na ratiba itatoka wiki moja kabla.
Tayari SImba SC imekamilisha usajili wake na wachezaji wote walikuwa wanahudhuria mazoezi mjini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Simba SC wanakwenda Zanzibar leo kuweka kambi rasmi ya kujiandaa na msimu

Phiri amerejea Simba SC baada ya miaka minne tangu aondoke mwaka 2010, akirithi mikoba ya Mcroatia Zdravko Logarusic aliyetupiwa virago mwishoni mwa wiki.
Haijulikani mshahara wa Phiri utakuwa kiasi gani, lakini mara ya mwisho aliondoka Simba SC akiwa analipwa dola za Kimarekani 5,000 (zaidi ya Sh. Milioni 7.5) kwa mwezi. 
Kocha huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2009/2010, aliyezaliwa Mei 3 mwaka 1956, alifanya kazi kwa awamu tatu tofauti akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi kati ya mwaka 2004 na 2010 kwa mafanikio makubwa- na sasa anataka kurejesha enzi za wana Simba ‘kutembea vifua wazi’.
Mzambia huyo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba SC, misimu ya 2004/2005 na 2009/2010 na pia alishinda Makombe ya Tusker mwaka 2005 la Tanzania na Kenya.
Phiri ni kocha anayekubalika zaidi mbele ya mashabiki wa Simba SC miongoni mwa makocha waliowahi kufundisha klabu hiyo- rekodi yake ya kukumbukwa zaidi ikiwa ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2009/2010 bila kufungwa hata mechi moja.
Lakini pia, namna alivyoweza kuiongoza Simba SC kuwatambia watani wa jadi, Yanga SC ni jambo lingine linalomfanya awe kocha mwenye heshima ya kipekee Msimbazi.
Katika awamu zote tatu alizofundisha Simba SC awali, Phiri hajawahi kufukuzwa- kwani amekuwa akiondoka mwenyewe kwa sababu mbalimbali.
Phiri ni kocha mwenye mafanikio tangu anacheza soka katika klabu za Rokana United (sasa Nkana F.C.) na Red Arrows zote za nyumbani kwao, Zambia kama mshambuliaji.
Alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia kilichocheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1978 na 1982, kabla ya kuiwezesha Chipolopolo kufuzu kwa AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana. 
Akiwa kocha, Phiri pia aliiongoza timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Zambia kucheza Fainali za kwanza kabisa za Kombe la Dunia nchini Nigeria mwaka 1997 kabla ya kushinda tuzo ya kocha bora wa mwaka nchini mwake mwaka 1999.
Simba SC Jumapili ilivunja mkataba na Mcroatia, Zdravko Logarusic ikiwa ni siku moja tu baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na ZESCO ya Zambia katika mchezo wa kirafiki Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Loga ambaye aliongezewa Mkataba wa mwaka mmoja mwezi uliopita- inadaiwa amefukuzwa kwa sababu za kutotii miiko na maadili ya klabu na Rais Aveva alisema kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kumvumilia kwa kiasi cha kutosha.
Loga ameondoka Simba SC baada ya kuiongoza katika mechi 21 tangu Desemba mwaka jana, kati ya hizo akishinda nane, sare tano na kufungwa nane.
Loga aliyerithi mikoba ya Mzalendo, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’, aliikuta Simba SC bado ipo kwenye mbio za ubingwa msimu uliopita, lakini mwishowe ikamaliza nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City, Yanga SC na Azam FC mabingwa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*