Membe anaona dawa pekee ya kumaliza mgogoro huo
unaotishia kupatikana kwa Katiba Mpya, ni kuitisha kura ya maoni ili
wananchi waamue kwanza wanataka Muungano wa serikali ngapi ndipo
mchakato uendelee.
Katika mahojiano na Mwananchi wiki iliyopita,
Waziri Membe alisema kama ni kuepuka gharama, basi kura ya maoni
ifanyike sambamba na Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka 2015.
“Kwa maoni yangu, utengenezaji wa katiba uko sawa
na safari inayoanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma,” alisema Membe ambaye
pia ni Mjumbe wa Bunge la Katiba kutokana na kuwa Mbunge wa Mtama na
kuongeza, “Kwa hiyo mnapotaka kusafiri, ni lazima mkubaliane aina ya
usafiri kabla ya kuanza safari. Mkishaamua kusafiri kwa treni, mnajua
safari itakuwaje.”
Alisema sura ya kwanza kwenye katiba yoyote ni
muhimu kwa kuwa ndiyo inayoamua mambo mengine yanayofuata. Kwa maana
hiyo, Waziri Membe anasema ingekuwa busara kwanza kuamua muundo wa
Muungano kwa kuwa sura nyingine zinazofuata zinarejea kwenye sura ya
kwanza, jambo ambalo halikufanyika.
“Sura hii ndiyo itakayoleta mwanga wa nini
kijadiliwe kwenye sura nyingine zote. Sasa kama hatukubaliani hapo,
tutajadilije vifungu vingine ndani ya katiba hiyo?” alihoji.
Akizungumzia kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, alisema ilifanya kosa moja tu la
kuandika rasimu moja tu na kuwateulia Watanzania idadi ya serikali na
kuiwasilisha kwenye Bunge la Katiba.
Alisema wakati Tume ya Warioba ilizunguka nchi
nzima kutafuta maoni ya wananchi na kwamba wapo waliosema wanataka
serikali mbili, wapo pia waliotaka serikali moja na vilevile wapo
waliotaka tatu.
“Ilipaswa kurekodi maoni hayo kama yalivyo na
kuyapeleka bungeni ili Bunge liyapitie na kufanyia uamuzi kulingana na
mahitaji yaliyopo. Alipokosea Warioba na timu yake ni kupeleka bungeni
rasimu moja yenye maoni ya pendekezo moja tu la serikali tatu,” alisema
Membe ambaye alijinadi kuwa ana uzoefu mkubwa katika masuala hayo ya
kuandika katiba kutokana na kushiriki kutatua migogoro sehemu nyingi
duniani, ikiwamo Zimbabwe.
“Walitakiwa kuja na rasimu tatu; ya serikali tatu,
mbili au moja. Duniani kote panapokea tofauti ya mawazo katika mambo ya
msingi kama hilo, kunapelekwa rasimu nyingi bungeni ili Bunge
lijadiliane kwanza na kufikia maafikiano, kabla ya kuendelea na
kupitisha vifungu vingine.
“Hata kina Warioba walitakiwa waje na rasimu tatu
bungeni; moja iwe ile ya watu wanaotaka serikali moja, nyingine iwe ya
wale waliotaka serikali mbili na pia iletwe rasimu ya wale wanaotaka
serikali tatu. Kisha wangesema (kina Warioba) maoni yetu sisi (tume) ni
Serikali tatu. Sasa wao, mengine wameyamaliza wenyewe na bungeni
wakaleta rasimu moja tu ya serikali tatu.”
Alisema pamoja na kosa hilo, bado Tanzania ina
fursa ya kujisahihisha kwa kuitisha kura ya maoni... “Sasa, dawa yake ni
moja tu. Twendeni kwa wananchi ili waamue kwa kupewa swali moja.
Unataka serikali ngapi?” alisema.Kwa Habari zaidi
“Tunaweza kufanya kura ya maoni kwa njia mbili.
Kwanza kuitisha kura ya maoni ili wananchi wajibu swali moja tu na pili,
kama hiyo ni gharama, basi wakati wa uchaguzi mwakani, tupige kura nne.
Moja ya Rais, nyingine ya mbunge, ya diwani na boksi jingine liwe la
idadi ya serikali.”
Waziri Membe alisema suala la idadi ya Serikali ni
moyo wa mchakato mzima wa Katiba, hivyo linapaswa kupatiwa ufumbuzi
kwanza kabla mambo mengi hayajaendelea.
Kuhusu Ukawa
Alipotakiwa kuzungumzia hatua ya wajumbe wa Bunge
la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao
vya chombo hicho cha kuandika Katiba, alisema: “Jumuiya ya kimataifa
inawashangaa. Wamekuwa wakiwaunga mkono kwa mambo mengi, lakini katika
hili hawako pamoja nao.”
Alisema kitendo cha wachache kususia Bunge ni cha ajabu na hakijawahi kutokea katika nchi nyingine zaidi ya Tanzania.
“Ni ajabu wachache kujigeuza kuwa pressure group
(wana harakati). Ukiachia watu wazuie Bunge (la Katiba) kwa sababu tu
hawapo, unaua dhana ya demokrasia. Kama wachache wanatumia vibaya
kutambuliwa kwao au mwaliko, tutaiharibu nchi. Nguvu ya wachache haiko
kwenye kususia vikao, bali ndani ya Bunge la Katiba. Ninaamini baadhi
yao wanajuta kwa kususia vikao.”
Alitetea kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutoa
maoni yake wakati akizindua Bunge la Katiba kwa maelezo kuwa alifanya
hivyo ili kuwapa changamoto.
“Ilikuwa ni food of thought (kitu cha kusaidia
kutafakari). (Kikwete) Halazimishi. Hakwenda pale kama Kikwete, bali
kama presidency (taasisi ya urais),” alisema.
Membe alisema hakuna mshindi katika mchakato wa
Katiba Mpya, hivyo hakuna maana watu wakavutana kiasi cha kutaka
kuuathiri mchakato huo ambao tayari umetumia mabilioni ya shilingi.
Comments