Na Seif Mangwangi,
Monduli
RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete jana aliwakumbuka
askari walioshiriki kwenye vita ya ukombozi wa kuiokoa nchi ya Msumbiji dhidi
ya kikundi cha Renamo waliokuwa wakipigana kutaka kushika utawala wa nchi hiyo
mwaka 1986 hadi 1988 kwa kuwatunuku nishani maalum.
Nishani hiyo iliyoenda
sanjari na utolewaji wa Nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Jeshi la Ulinzi la
Wananchi Tanzania kwa maafisa ambao bado wanatumikia jeshi hadi Septemba mosi
mwaka huu, jumla ya Maafisa na Askari 59 wa jeshi hilo ikiwemo 37 waliopigana
vita ya ukombozi nchini Msumbiji.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete
Nishani ya operesheni safisha Msumbiji ilitolewa kwa askari wa jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania walioko kwenye utumishi, waliostaafu na waliofariki
ikiwa ni katika kuenzi na kuthamini mchango wao katika vita hivyo vya ukombozi.
Miongoni mwa waliopewa
nishani hizo ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi na kujenga Taifa, Jenerali
Davis Mwamunyange huku Mkuu wa Utumishi Jeshini, Luteni Jenerali Samuel Ndomba
akijikuta akitunukiwa nishati mbili za Miaka 50 pamoja na ya operesheni safisha
Msumbiji.
Askari waliofariki
dunia na nishani zao kupokelewa na ndugu na jamaa zao ni pamoja na Meja Ayubu
Swedi Twalipo, Kapteni Bruno Stanslaus Mtillu, Mteule Hamad
Sharifu, Mteule Othman Mpemba, Mzee Juma na Koplo William Laizer.
Waliostaafu na
kushiriki katika vita hivyo vya ukombozi ni pamoja na Jeneralil David Musuguri,
Luteni Jenrali Martin Mwakalindile, Meja Jenrali Nicolaus Miti, Brigedia
Jenrali Hassan Ngiwilizi, Brigedia Jenerali Wilfred Kabunda, Kanali Juma
Khamisi.
Wengine ni Kanali Said
Mtonga, Kanali Limbe Masanja, Luteni Kanali Maulid Pandu, Luteni Kanali Said
Hassan, Meja Sartunini Kubuva, Kapteni Issa Haji, Luteni Asajile Swebe, Luteni
Khamisi Faki, Sajini Kassimu Haji, Sajini Hamid Juma na Private Haji Hamza.
Katika hafla hiyo
iliyofanyika katika ukumbi wa Jenerali Kiwelu, viongozi mbalimbali walishiriki
ikiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa,
Dkt Hussein Mwinyi, Mawaziri wakuu wastaafu Edward Lowasa na John Malechela na
viongozi wa dini mbalimbali mkoani Arusha.
Comments