FR JAMES RUGEMALIRA AHIMIZA UWEKEZAJI MKOANI KAGERA








 Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi (ICFTU/AFRO), Andrew Kailembo(kulia), akiwa katika mkutano wa wadau mbalimbali wa kujadili maendeleo ya mkoa wa Kagera uliofanyika jana.

 Wakili wa Kujitegemea, wa IMMMA ADVOCATES, Protas Ishengoma akiongoza mkutano huo.


 REV.Fr Kamugisha (kulia), ambaye ni Mkurugenzi wa Hoteli ya Kolping akichangia mada. Kutoka kushoto ni Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr, James Rugemalira na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu, Fabian Masawe.
 Wanahabari wa mkoa wa Kagera wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Utawala wa Jumuia ya Afrika Mashariki, mstaafu, Abdul Katabaro naye alipata fursa ya kuchangia katika mkutano huo muhimu wa kuhimiza uwekezaji mkoani humo.

MSHAURI wa Kimataifa wa kujitegemea (International Independent Consultant) Fr. James Rugemalira, wa Mabibo Breweries, jana aliandaa hafla ya kuzungumzia fursa za maendeleo katika mkoa wa Kagera ndani ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Hafla hiyo ilihudhiriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali  Mstaafu Fabian Massawe, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi. 

Wengine waliohudhuria ni pamoja na wana Kagera wanaoishi na kufanya Kazi nje ya mkoa wa Kagera wakiwemo wakili wa kujitegemea Bw. Protase Ishengoma wa IMMMA Advocates, mfanyabiashara na Mshauri wa Fr. James, Bw. Abdul Katabaro ambaye amestaafu kutoka utumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mzee Andrew Kailembo kutoka Bruxelles, Rev. Fr. David na Kyabukoba, miongoni mwa wengi. 

Hafla hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Kolping, mjini Bukoba, pia ilihudhiriwa na waandishi wa habari kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Fr. James alisisitiza juu ya mkoa kuzitumia fursa nyingi za uchumi zinazotokana na jiografia ya mkoa wa Kagera kupakana na nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki, zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya kwa maana hiyo kuufanya mkoa huo kuwa ndicho kiunganishi cha nchi zote (hub). 


Kwa sababu hiyo alisisitiza umuhimu wa mkoa wa Kagera kuwa na miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa uwanja wa Ki-mataifa Omukajunguti, ujenzi wa Bandari Kavu na maeneo huru ya Uzalishaji (EPZ) eneo la Kitengule na kilimo cha Matunda, mboga na mazao mengine ya chakula. Alisisitiza kuwa soko la mazao lipo katika nchi zinazouzunguka mkoa wa Kagera.

Fr. James aliitumia fursa hiyo kuelezea mipango ya kampuni ya Mabibo Breweries kuwekeza kwenye kiwanda cha kuzalisha bia aina ya Windhoek katika mikoa ya Kagera, Tanga na Kilimanjaro. 


Pia alizungumzia mpango wa kuanzisha taasisi ya ki mataifa ya uchunguzi na tiba kwa maradhi ya Kansa kitakachojulikana kama RUTAKWA BYERA INTERNATIONAL DREAM TANK CANCER CENTER ndani ya Manispaa ya Bukoba.

Naye Mkuu wa Mkoa alimshukuru sana Fr. James kwa moyo wa uzalendo wa kuhamasisha uwekezaji katika mkoa wa Kagera na yeye mwenyewe na Mabibo Breweries kuwa msitari wa mbele kwa vitendo. Kanali Massawe alimuhakikishia kwamba Serikali ya Mkoa itampatia yeye pamoja na wawekezaji wengine watakaojitokeza, ushirikiano wa dhati ili kuhakikisha uchumi wa mkoa unapanuka na kuongeza ajira kwa vijana.

Kanali Massawe aliwaambia washiriki wa hafla hiyo kuwa alipofika kwenye mkoa wa Kagera miaka saba iliyopita, mkoa ulikuwa unashika nafasi ya tatu kutoka mwisho kati ya mikoa 25 katika uchumi lakini sasa mabadiliko makubwa yamekuwepo mkoa upo kwenye nafasi ya kumi na Sita. 


Aliongeza kusema kwamba kwa fursa zilizopo, endapo zitatumiwa vizuri, basi mkoa unaweza kufanya vizuri zaidi. Kanali Massawe, aliziainisha fursa nyingi zilizopo na ambazo hazijasisimiliwa kuwa ni pamoja na Utalii ambao mkoa unavyo vivutio vingi ikiwa ni pamoja na Ziwa Victoria, mto Kagera, watu na Utamaduni wao, historia, kituo cha hija cha Nyakijoga na Makanisa makubwa yaliyojengwa zaidi ya miaka mia moja iliyopita.

Waalikwa mbalimbali waliopata fursa ya kuongea walimpongeza sana Fr. James kwa jitihada zake na kuwahamasisha /kuwashirikisha wengine katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya mkoa wa Kagera.


 Naye mwakilishi wa waandishi wa habari waliohudhuria, aliahidi kwamba watatoa ushirikiano mkubwa wa kuihabarisha jamii kwa ufasaha juu ya jitihada zote za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI