MAAFISA WA JESHI LA MAGEREZA WAPEWA MAFUNZO KUHUSU TAKWIMU RASMI


unnamed (28)Meneja Tawala wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Gabriel Madembwe (katikati) akiwahutubia Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao Makuu ya Jeshi hilo wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Takwimu Rasmi yaliyofanyika leo mkoani Morogoro. Kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Dkt. Frank Mkumbo na kulia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Makao Makuu Bw. Edward Kaluvya.
unnamed (29)Baadhi ya Waandishi wa Habari wakichukua habari wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Takwimu Rasmi kwa Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Amabilisi uliopo mkoani Morogoro.
unnamed (30)Makamu Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Dkt. Frank Mkumbo akiwa katika mahojiano na Waandishi wa Habari mara baada ya ufunguzi wa Mafunzo ya Takwimu Rasmi kwa Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Amabilisi uliopo mkoani Morogoro.
………………………………………………………………………………………..
Na Veronica Kazimoto
Morogoro
Wito umetolewa kwa Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao Makuu ya Jeshi hilo kuwahimiza maofisa waliopo chini yao kutumia takwimu mbalimbali zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ili zisaidie katika kuandaa mipango na kutoa maamuzi mbalimbali ya kazi zinazofanywa na jeshi hilo.
Wito huo umetolewa leo na Meneja Tawala wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Gabriel Madembwe wakati akifungua Mafunzo ya Takwimu Rasmi kwa Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi hilo yaliyofanyika katika ukumbi wa Amabilisi uliopo mkoani Morogoro.
Madembwe amesema kuwa maafisa wengi katika Jeshi la Magereza wakijua umuhimu wa matumizi ya takwimu itasaidia kuleta mabadiliko hasa katika kupanga mipango yao kwenye maeneo yao ya kazi.
“Napenda kusisitiza kuwa ili mabadiliko yatokee sehemu yoyote ile; iwe nyumbani, kazini au katika jamii, ni lazima kuwepo na kichocheo cha mabadiliko hayo, hivyo ninyi mtakuwa kiungo muhimu katika kuleta mabadiliko yenye kutoa maamuzi kwa kuzingatia matumizi ya takwimu rasmi”, amesema Madembwe.
Nae Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka Makao Makuu Dar es Salaam Bw. Edward Kaluvya amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo kwa sasa wamekuwa wakitumia sana takwimu katika maeneo mengi ya kazi zao.
“Mafunzo haya yatatusaidia kujenga uelewa wa pamoja na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusiana na uzalishaji, uhifadhi na utumiaji wa takwimu kwa usahihi katika kutoa maamuzi na kupanga mipango endelevu katika Jeshi letu la Magereza”, amefafanua Kaluvya.
Mafunzo haya ya siku tatu yanatolewa na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kilichopo jijini Dar es Salaam na yamefadhiliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupia Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu Tanzania (TSMP).
Lengo kuu la Mpango huu ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo imara wa kitaifa wa kuratibu, kukusanya, kuhifadhi na kusambaza takwimu nchini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI