Mwaka wa uchaguzi,Kikwete atoa salamu za mwisho za mwaka

Rais Jakaya Kikwete
  1. Daftari la Kudumu: Tume ya Taifa ya Uchaguzi mwezi huu itaanza kuandikisha wapigakura kwa kutumia mfumo wa utambuzi wa alama za mwili (BVR) ambao hata hivyo katika majaribio umezua malalamiko.
  2. Kuvunja Bunge: Bunge la 10 litatimiza muda wake wa miaka mitano katika mkutano wake wa 20 utakaomalizika kwa Bunge hilo kuvunjwa mwezi Julai.
  3. Mwaka mgumu: Shughuli za kura za Maoni, uandikishaji wapiga kura, Uchaguzi Mkuu na Vitambulisho vya Taifa zinatarajiwa kutafuna fedha nyingine na hivyo kuufanya mwaka huu kuwa mgumu kifedha.
  4. Kura za maoni: Watanzania watapiga kura za maoni za ama kupitisha au kuikataa Katiba Inayopendekezwa Aprili 30, hatua ambayo kwa vyovyote itaweka upya mustakabari wa Taifa.
  5. Uteuzi wagombea: Kuanzia Mei vyama vya siasa vitaanza kupitisha wagombea na majina yao kupelekwa NEC kwa uteuzi ili kuviwakilisha kwa nafasi za urais, ubunge na udiwani
  6. Uchaguzi Mkuu: Mwishoni mwa Oktoba kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa baina ya chama tawala na upinzani.

Dar es Salaam. Mwaka wa uchaguzi umeingia. Usiku wa kuamkia leo, Watanzania wameupokea mwaka mpya 2015 huku tafakari kubwa ikiwa ni matukio makubwa yatakayotokea mwaka huu, ukiwamo Uchaguzi Mkuu na kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Mbali na uchaguzi wa rais wa awamu ya tano, wananchi wataamua ama kuipitisha au kuikataa Katiba Inayopendekezwa, mambo ambayo wasomi, wanasiasa na wanaharakati wameonya kuwa yanatakiwa kuendeshwa na kusimamiwa kwa weledi na umakini mkubwa.
Vilevile, kutokana na matukio hayo kugharimu fedha nyingi, wataalamu wa uchumi wanatabiri kuwa mwaka huu utakuwa mgumu na itakaowalazimu Watanzania kufunga mikanda zaidi.
Pia, macho na masikio ya wananchi yako kwa vyama vya upinzani ambavyo vimeungana na kuzaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuona kama vitasimamisha mgombea mmoja wa urais na katika nafasi za ubunge na udiwani kama vilivyokubaliana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Maandalizi ya uchaguzi huo yanaanza mwezi huu kwa wapigakura kuandikishwa upya katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, ambalo tangu mwaka 2009 halijawahi kuboreshwa na hivyo kusababisha wengi kushindwa kupiga kura katika uchaguzi wowote uliofanyika baada ya 2010.
Pengine jambo ambalo linasubiriwa kwa hamu na wananchi ukiacha Uchaguzi Mkuu na Katiba Mpya ambayo kampeni zake zitaanza Aprili 30, ni mchakato wa ndani ya vyama vya siasa wa kupata wagombea urais, hasa kutokana na mvutano ulioanza kujitokeza ndani ya CCM na mvutano unaotarajiwa ndani ya Ukawa.
Matukio
Tukio litakaloanza mwaka huu ni lile la Januari 30 la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ambao utakamilika Aprili 28 ukifanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kulingana na uandikishaji wa majaribio uliofanyika katika majimbo matatu ya Kawe, Kilombero na Katavi, shughuli yenyewe inatarajiwa kuvuta hisia na hamasa za Watanzania wengi hasa kutokana na muda, matatizo ya kukwama kwa mashine za kielektroniki (BVR) na wingi wa watu waliojitokeza.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ametangaza tarehe ya upigaji Kura ya Maoni kuwa ni Aprili 30.
Februari mwaka huu, CCM imeahidi kutoa msimamo wake kuhusu wanachama wake walioanza kufanya kampeni mapema kujihusisha na vitendo vilivyokiuka maadili ndani ya chama na jamii. Huenda chama hicho kikawaengua baadhi yao kwa kuongeza muda wa onyo hivyo kujikuta wakishindwa kuwania nafasi hiyo, iwapo watabainika kuendelea kukiuka maadili ya chama, licha ya awali kuonywa na kupewa adhabu ya kutojihusisha na masuala hayo mpaka baada ya miezi 12.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; mawaziri Bernard Membe (Mambo ya Nje), Stephen Wasira (Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.


Mei utakuwa na tukio la aina yake pale Ukawa na CCM pamoja na vyama vingine vitakapokuwa vikiteua wagombea urais, ikiwa ni baada ya wengi waliojitokeza kuchujwa katika vikao vya ndani vya vyama hivyo.
Juni mwaka huu, Rais Kikwete atalivunja Bunge baada ya kumalizika kwa Mkutano la Bajeti utakaoanza Aprili mwaka huu, ukiwa tayari umepitisha bajeti ya Serikali ambayo sehemu yake itatumiwa na Serikali mpya ya awamu ya tano. Pamoja na kwamba siyo utaratibu wa kikanuni, lakini kwa utamaduni wa Bunge la Tanzania, Rais Kikwete anaweza kutoa hotuba ya kulivunja Bunge.
Miezi inayotarajiwa kuwa na changamoto kubwa ni kuanzia Julai hadi Oktoba ambayo itakuwa ya kampeni za uchaguzi ambao wagombea urais, ubunge na udiwani watakuwa wakinadi sera zao.
Mwishoni mwa Oktoba, ndipo utakapofanyika Uchaguzi Mkuu na Tanzania kupata rais mpya ambaye mpaka sasa ni vigumu kutabiri atakuwa nani na atatoka chama gani. Hali hiyo inatokana na CCM hadi sasa kuwa na makada zaidi ya 14 wanaotajwa kuutaka urais wakiwamo wanne ambao tayari wametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo. Kwa upinzani, viongozi wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD vinavyounda Ukawa ndiyo wanaopewa nafasi za kugombea nafasi hiyo. Hao ni Profesa Ibrahim Lipumba, Dk Willbrod Slaa, James Mbatia na Freeman Mbowe huku vyama vyenyewe vikisema vinaweza hata kumpata mtu nje ya muungano huo.
Uchambuzi wa kisomi
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam (Tudarco), Lois- Singa Metili alisema mwaka 2015 ni kipindi cha mpito ambacho endapo mambo yote yaliyopangwa yatakwenda sawa, miaka inayofuata itakuwa mizuri kwa Watanzania.
“Hatujui kura za hapana au za ndiyo kwenye Kura za Maoni ya Katiba zitakuwa ngapi, hatujui kama NEC itapewa meno ya kutosha ya kusimamia uchaguzi ili tupate rais kwa njia ya haki.”
Alisisitiza kuwa iwapo haki itatumika katika kupitisha mambo hayo, nchi itajenga msingi imara kwa maendeleo ya watu wake kwa miaka mingi ijayo.
Alisema kwa kuwa Tanzania mwaka 2014 ilitajwa vibaya kwenye vyombo vya habari vya Magharibi, ikihusishwa na kashfa za rushwa, inabidi taasisi zote nchini kurekebisha kasoro hiyo.
Kuhusu siasa, Metili alisema CCM itakuwa na kibarua cha kumpata mgombea mwenye sifa atakayekubalika kwa wananchi. Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kutokana na mwaka 2015 kukabiliwa na mambo mazito ya kitaifa yanayohitaji fedha nyingi, Serikali itakuwa katika wakati mgumu kifedha.
Dk Ngowi aliutaja mwaka huu kuwa ni wa kipekee kwa kuwa licha ya kuhitaji fedha nyingi, utaongezewa maumivu na hatua ya wahisani kukataa kutoa msaada kwa sababu ya kashfa ya escrow iliyotokea mwishoni mwa 2014.
Alieleza kuwa ingawa maisha ya wananchi yanaweza yasibadilike sana, lakini Serikali itahiitaji kujipanga upya katika kukusanya fedha.

Uchambuzi wa Dk Ngowi unaungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila aliyesema mwaka huu uchumi wa nchi utaporomoka kwa sababu ipo katika mahitaji makubwa ya fedha za uchaguzi, uandikishaji Vitambulisho vya Taifa na vya kupigia kura sambamba na upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya.
“Uchumi unakua lakini maendeleo ya uchumi hayaonekani kwa sababu ya matumizi mabaya ya fedha za umma pamoja na uchumi kukuzwa na sekta za madini, utalii, mawasiliano ambazo hazibebi watu wengi kama ilivyo katika kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema licha ya mwaka huu kuwa na mambo mengi muhimu, Serikali haionekani kuchukua hatua za dharura.
Dk Kijo- Bisimba alisema ili taratibu ziende kama zilivyopangwa, ilitakiwa hadi sasa nakala za Katiba Inayopendekezwa ziwe zimeshasambazwa kwa wananchi, lakini hilo linaonekana kusuasua.
“Maboresho ya Daftari la Wapigakura yalitakiwa yawe tayari, lakini mamlaka hazijajipanga kama ulivyoona kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema Watanzania wanaingia mwaka mpya wakiwa wamechanganyikiwa, hawajui nani anasema ukweli kuhusu fedha za escrow kama zilikuwa ni za umma au la... “Bunge lilisema fedha zile ni za umma, lakini huyu mwingine naye kasema siyo fedha za umma.”Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (Duce), Dk Aneth Komba alisema; “Ninachokiona mwaka huu utakuwa mfupi sana kutokana na mambo kuwa mengi.”
JK atoa salamu za mwisho za mwaka akiwa Rais
Rais Jakaya Kikwete jana alitoa salamu zake za Mwaka Mpya kwa mara ya mwisho katika utawala wake huku akisema mwakani atakuwa akifuatilia salamu kama hizo kupitia televisheni na redio akiwa kijijini kwake Msoga mkoani Pwani.
Katika hotuba hiyo yenye maneno 5,988 iliyojaa mapitio ya mambo mbalimbali ya mwaka 2014, Rais Kikwete alisema wakati Rais wa awamu ya tano akitoa zake za kwanza za mwaka mpya, yeye atakuwa raia wa kawaida na itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa.
Sanjari na hayo, Rais aliwaagiza viongozi wa Serikali wanaowawekea vikwazo wafanyabiashara wanaouza mazao nchi za nje kuacha vitendo hivyo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kutimiza azma yao.
Alisema uzalishaji mazao mwaka huu umeongezeka hadi tani milioni 16.2 ukilinganisha na tani milioni 14.38 za mwaka 2013 na kwamba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) si mnunuzi wa mazao yote hayo, hivyo mengine yatanunuliwa na wafanyabishara wanaotakiwa kushawishiwa kuyanunua kwa wingi.
“Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo,” alisema Rais Kikwete.

 Aliwataka Watanzania kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwani kushindwa kufanya hivyo kutawanyima fursa ya kupiga kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa pamoja na Uchaguzi Mkuu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI