Mwiba wa mauaji ya vikongwe kupatikana kupitia nishati ya umeme Shinyanga

unnamed1rMkuu wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini Anna Rose Nyamubi (katikati aliyeshika kipaza sauti) pamoja na Mbunge wa Jimbo la Solwa Salum Ahmed ( wa tatu kutoka kulia) pamoja na wakazi wa Lyabusalu wilayani Shinyanga Vijijini wakiimba na kucheza kwenye uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.
unnamed2rWaziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo wakati wa utoaji wa hotuba ya uzinduzi wa mradi huo
unnamed4rWaziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi huo
……………………………………………………………………………………
Na Greyson Mwase
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini Anna Rose Nyamubi amesema kuwa kupatikana kwa nishati ya umeme katika wilaya hiyo kutapunguza mauaji ya vikongwe ambao wamekuwa wakiuwawa kutokana na kuwa na macho mekundu yanayosababishwa na moshi wa majiko ya kuni.
Nyamubi ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vjjijini (REA) Awamu ya Pili uliofanyika katika Kata ya Lyabusalu wilayani Shinyanga Vijijini. Mradi huo ulizinduliwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
Alisema kuwa katika wilaya ya Shinyanga Vijijini kumekuwa kukijitokeza mauaji ya wazee wenye macho mekundu kwa dhana ya kuhusishwa na vitendo vya kishirikina, dhana ambayo ni potofu kabisa
Alieleza kuwa vikongwe wengi wameathirika na moshi wa majiko ya kuni, yanayopelekea macho mekundu na kuongeza kuwa mara baada ya wilaya hiyo kupata neema ya umeme na wananchi wake kuanza kutumia nishati ya umeme kwa kupikia itapunguza waathirika wa moshi wa majiko ya kuni na kupunguza vifo.
Aliendelea kusema kuwa nishati ya umeme itawezesha wananchi wa wilaya hiyo kuanzisha viwanda vidogo vidogo kama vya kukoboa nafaka kama mahindi, mpunga na kujiingizia kipato na hivyo kupunguza umasikini.
“ Wito wangu ni kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hii ya kuwa na umeme kwa kujikwamua kiuchumi na kubuni miradi mbalimbali badala ya kutegemea kufanyiwa kila kitu na Serikali.
Mbali na kuwataka wananchi kuunganisha nyumba zao na miundombinu ya umeme iliyowekwa, amewataka wananchi kuanzisha vikundi vidogo na kuanzisha miradi midogo itakayowakwamua kiuchumi.
Wakati huo huo akizungumza wakati wa uzinduzi huo Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)- Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joyce Ngahyoma aliwataka wananchi kuchangamkia mradi huu kwa kuunganisha umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 ambayo ni kodi tu kwani gharama zote zimebebwa na serikali, kabla ya mradi huo kumalizika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Mhandisi Ngahyoma alieleza kuwa mara baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ya Mradi wa REA wateja watakaoomba kuunganishiwa umeme watalipa shilingi 177,000 au kusubiri awamu ya tatu ya mradi wa REA inayotarajiwa kuanza mapema mwezi Julai.
Akizungumzia suala la uwekaji wa mifumo ya umeme kwenye nyumba za wananchi Ngahyoma aliwataka wananchi kuepukana na kutumia vishoka na badala yake watumie wakandarasi waliosajiliwa na Serikali kwani Tanesco haitahusika na utapeli utakaofanywa na vishoka.
Aliwataka wateja wenye kutaka kuunganishiwa umeme kufika katika ofisi za Tanesco na kulipia ili wataalamu wake wakague mifumo ya umeme katika nyumba zao kabla ya kuwaunganishia na huduma ya umeme.
Akizungumzia changamoto katika utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini uliotekelezwa na REA Awamu ya Pili Ngahyoma alieleza kuwa ni pamoja na wateja kudai fidia, idadi ya mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko uwezo wa mradi, na miuondombinu kama barabara kuwa mibovu hali iliyopelekea kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi
Katika wilaya ya Shinyanga jumla ya vijiji tisa vilinufaika na mradi wa umeme vijijini unaofadhiliwa na REA Awamu ya pili kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI