Na
Veronica Simba
Serikali inaendeleza
jitihada za kuachana na matumizi ya nguzo za umeme za miti na badala yake kutumia
nguzo za zege ikiwa ni hatua mojawapo ya kuboresha huduma ya usambazaji na upatikanaji
wa umeme nchini.
Hayo yalibainika
mwishoni mwa wiki katika kikao baina ya uongozi wa Kampuni ya Sunshine Group
Ltd na wataalam wa sekta ya umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na
Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
Katika kikao hicho,
Kampuni ya Sunshine iliwasilisha mapendekezo (proposal) ya kuanzisha kiwanda
cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini.
Akieleza msimamo wa
Serikali kuhusu mapendekezo hayo, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent
Luoga alisema Serikali ina dhamira ya kutumia nguzo za umeme zilizotengenezwa
kwa zege na kuachana na za miti zinazotumika sasa kutokana na manufaa yake.
Mhandisi Luoga
aliyataja manufaa ya kutumia nguzo za zege kuwa ni pamoja na uimara wa nguzo
husika. “Huwezi kulinganisha uimara wa nguzo za zege na hizi za miti
tunazotumia hivi sasa. Nguzo za zege ni madhubuti na imara zaidi,” alisema.
Akifafanua zaidi,
Mhandisi Luoga alisema, kutokana na uimara wa nguzo za zege, uhai wake ni wa
muda mrefu kulinganisha na nguzo za miti.
“Uhai wa nguzo za
zege ni kati ya miaka 70 hadi 100, wakati uhai wa nguzo za miti ni miaka 50,”
alisema Luoga na kusisitiza kuwa sifa hiyo ya uhai mrefu wa nguzo za zege
inazalisha manufaa mengine kwa Serikali na wananchi kwa ujumla endapo nguzo
hizo zitatumika.
Akielezea manufaa
yanayotokana na uhai mrefu wa nguzo za zege, Mhandisi Luoga alisema Serikali
itatumia fedha kidogo kutokana na nguzo za zege kudumu kwa muda mrefu, tofauti
na nguzo za miti ambazo uhai wake ni mdogo.
Aidha, faida nyingine
za kutumia nguzo za zege, zilizotajwa na wataalam katika kikao hicho ni pamoja
na kuwa rafiki wa mazingira ambapo huepusha ukataji wa miti.
Nyingine ni uwezo
wake wa kutopitisha maji na kutoshika moto kwa urahisi (water and fire proof).
Akihitimisha mazungumzo
husika, Kamishna Luoga alisema Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na
Kampuni hiyo pamoja na wawekezaji wengine wenye nia ya kutengeneza nguzo za
umeme za zege ili kufikia makubaliano yatakayowezesha pande zote mbili
kunufaika.
“Mkakati wetu ni kwa
Tanesco kutengeneza nguzo za zege kwa matumizi ya ndani ya nchi lakini ni vema
tukapata wawekezaji wengine watakaosaidia kutengeneza nguzo hizo kwani mahitaji
ni makubwa sana,” alisema.
Comments