SERIKALI KUMALIZA KULIPA DENI LOTE LA MAHINDI MACHI 30


unnamedkay1 
SERIKALI imesema itajitahidi kuhakikisha inalipa deni lote la mahindi yaliyonunuliwa kutoka kwa wakulima na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ifikapo Machi 30, mwaka huu.
Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumapili, Machi 2, 2015) kwenye uwanja wa CCM wa Vwawa wilayani Mbozi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali imedhamiria kufuta deni lote.
“Hapa Mbozi tulikuwa tunadaiwa sh. bilioni 21 lakini tumetoa sh. bilioni 4.5 kwa hiyo tutabakia na deni la kama sh. bilioni 16 ambalo tunajitahidi liwe limeisha ifikapo mwishoni mwa mwezi huu,” alisema.
“Tunachoweza kuahidi kama Serikali ni kwamba, msimu huu hatutarudia kosa la mwaka jana ingawa mtihani mkubwa tulionao ni wa kushughulika na hifadhi ya chakula kwa kujenga vihenge (SILOS) ili hata kama kuna ziada n tusipate taabu ya kuhifadhi,” aliongeza.
Alisema alishakwenda Poland kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete na wao wameshakuja kuona hali halisi ilivyo. “Tumependekeza vihenge vijengwe kwenye kanda za Mbeya, Rukwa, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha au Kilimanjaro na Shinyanga ili iweze kuhudumia kanda ya Ziwa,” alisema.
Wakati huo huo, Mbunge wa Mbozi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi amesema Serikali imekwishalipa zaidi ya sh. bilioni 81 na kwamba deni lililosalia linafikia sh. bilioni 59.
“Hadi mwishoni mwa mwaka jana, tulikuwa tumeshalipa sh. bilioni 51.5/- na mwaka huu tumepata sh. bilioni 15 kutoka CRDB na hivi majuzi kuna bilioni nyingine 15 zimetoka Hazina… Agizo la Serikali ni kwamba mahindi yote yawe yamelipwa ifikapo Machi 30, naamini tutakamilisha,” alifafanua.
Alielezea pia tatizo la maji linaloukabili mji wa Mbozi na vitongoji vyake na kueleza kwamba Serikali inashughulikia tatizo hilo katika programu mbalimbali.
Mapema, akiwa katika ghala la nafaka la NFRA katika makao makuu ya wilaya ya Mbozi, Vwawa, Waziri Mkuu alielezwa kwamba kanda ya Makambako ambayo inajumuisha vituo vya Makambako na Vwawa imezidiwa uwezo na sasa wanalazimika kuhifadhi magunia ya mahindi nje kwa vile maghala yamejaa.
Meneja wa Kanda hiyo wa NFRA, Bw. Abdillah Nyangasa alisema kanda hiyo ina uwezo wa kuhifadhi tani za nafaka 34,000 ambapo kati ya hizo, tani 22,000 ni maghala ya Makambako na tani 12,000 ni maghala ya Vwawa, Mbozi.
Hata hivyo, Bw. Nyangasa alisema kanda hiyo kwa sasa kina tani za mahindi 79,496.8 zikijumuisha tani 15,738.9 za msimu uliopita licha ya tani 63,757.8 ambazo zimenunuliwa katika msimu huu
“Ili kukabiliana na uhaba wa maghala, kanda yetu hulazimika kufanya hifadhi ya nje (outside storage) kwa kutumia maturubai (tarpaulins) ili mahindi yasiharibiwe na hali ya hewa kama mvua au jua kali,” alisema Bw. Nyangasa.
Waziri Mkuu anamaliza ziara yake ya siku saba mkoani Mbeya leo kwa kufanya majumuisho na kisha kurejea jijini Dar es Salaam.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI