Mkurugenzi
wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya, Dk. Mpoki Ulisubisya akiwaongozwa
Wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Rukwa kuelekea Wodini kumjulia hali Mtoto
Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana
kijijini kwao juzi.
Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stellah Manyanya akiwa anamwangalia kwa jicho la
huruma Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu
wasiojulikana na kutokomea nacho akiwa amelazwa katika Hospitali ya
Rufaa ya Mbeya.
Wakuu wa
Mikoa ya Mbeya na Rukwa wakimjulia hali Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja
cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao juzi.
Wakuu wa
Mikoa ya Mbeya na Rukwa sambamba na viongozi wa Chama cha Albino Mkoa wa
Mbeya wakiwa wameinamisha nyuso zao huku wakisali kuwaombea watu wenye
ulemavu wa ngozi ili wasipate madhara baada ya kumtembelea Mtoto Baraka
aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini
kwao juzi.
Mama
mzazi wa mtoto Baraka,Prisca Shabani akiwa na jeraha kichwani baada ya
kupigwa na watu waliomkata kiganja mtoto wake, akiwa anawasikiliza wakuu
wa mikoa ya Mbeya na Rukwa waliomfika kuwajulia hali katika Hospitali
ya Rufaa ya Mbeya wanakopatiwa matibabu.
Mtoto
Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana
kijijini kwao juzi akiwa amelala kitandani akiendelea kupatiwa matibabu.
.Waandishi
wa habari wakichukua maelezo kutoka kwa wahanga wa tukio la kukatwa
kiganja kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino).
Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
Mhandisi Stella Manyanya walifika Hospitalini baada ya mtoto huyo
kufikishwa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mtoto
huyo mkazi katika kijiji cha Ikonda kata ya Chitepa wilaya ya Sumbawanga
mkoani Rukwa alihamishiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya
kukatwa kiganja chake akitokea kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani
Momba mkoani hapa.
Akizungumza
kwa masikitiko makubwa mama wa mtoto huyo, Prisca Shaban(28) alisema
tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa saba usiku alipokuwa anarudi
ndani akitokea nje kujisaidia alivamiwa na mtu ambaye hakumfahamu na
kisha akamsukumia ndani kabla ya kumpiga kichwani kwa rungu na kisha
kupoteza fahamu.
Alisema
akiwa amepoteza fahamu mtu aliyekuwa amemvamia ndipo alipata nafasi ya
kuingia ndani na kutekeleza adhma yake ya kumkata kiganja mtoto huyo
ambaye ni mmoja kati ya watoto watatu wenye ualbino katika familia hiyo
na kuondoka nacho.
Alisema
wakati hayo yakitokea mumewe aliyemtaja kwa jina la Cosmas Lusambo
alikuwa amekwenda kulala nyumbani kwa mke mdogo kwani ilikuwa zamu ya
kwenda kulala huko kwa usiku huo lakini baada ya kusikia mayowe ya
kuomba msaada alikwenda kuungana na familia yake na kumpeleka mtoto
kituo cha afya cha Kamsamba kutokana na kuwa jirani na kijiji chao.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya, Akizungumza
baada ya kumtembelea Baraka katika wodi ya watoto kwenye hospitali ya
rufaa kanda ya Mbeya, alioneshwa kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi
kulifanyia kazi ili wahusika wapatikane na kuchukuliwa hatua.
Alisema
ni tukio ambalo linasikitisha ambalo linazidi kuendeleza vitendo vya
aibu kwa kuwafanyia ukatili wa kinyama albino kwa ujinga wa watu
wachache wanaowadanganya watu kuwa viungo vyao ni bahati ya kuleta
utajiri.
Mhandisi
Manyanya mbali na kuzungumza na familia ya waathirika wa janga hilo pia
aliongoza sara fupi ya kuwaombea albino hospitalini hapo alionesha pia
kusikitishwa na mwenendo wa mashitaka ya watu waliofanya ukatili dhidi
ya albino akisema mahakama zimekuwa na milolongo mirefu inayokatisha
tama wadau wa kupinga ukatili huo.
Mkuu huyo
wa mkoa alishauri pia kuangaliwa upya kwa sheria inayohusu masuala ya
hukumu za kifo akisema ikibidi inapaswa kubadilishwa ili iweze kutoa
haki kwa watu wanaofanya ukatili dhidi ya wenzao.
Alisema
sheria ya sasa kumtaka rais pekee kuwa mtu wa mwisho kutoa uamuzi
kunyongwa kwa mtu aliyehukumiwa inakosa nguvu ya kutekelezwa kutokana na
majukumu mengi aliyonayo na kushauri kuwa ni vyema vyombo vya sheria
vipewe mamlaka ya mwisho ya kutekeleza adhabu hiyo.
Na Mbeya yetu
Comments