Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hajaletewa majina ya
watu 16 waliohukumiwa kifo kutokana na mauaji ya maalbino nchini kwa sababu
safari ya kisheria ya majina hayo kufikishwa kwake ni ndefu.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana,
Jumapili, Aprili 12, 2015 wakati alipozungumza
katika ibada maalum ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Liberatus Sangu
kuwa Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Shinyanga.
Akizungumza katika ibada hiyo
iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga
na mbele ya viongozi wengi wa Kanisa hilo wakiwemo maaskofu wakuu, maaskofu na
maaskofu wasaidizi 38, Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo kujibu madai kuwa
Serikali yake haichukui hatua za kutosha kukabiliana na mauaji ya albino na pia
kufafanua juu ya shinikizo ambalo linatolewa na baadhi ya mashirika yasiyokuwa
ya serikali (ngo’s) yakimtaka Rais kutia saini ya kuruhusu watu hao wanyongwe.
Rais Kikwete aliwaambia viongozi hao
wa dini: “Ninayo maombi maalum kwenu viongozi wa dini. Naomba mtusaidie
kuielimisha jamii ili iachane na imani za kishirikina. Vikongwe wanauawa kwa
sababu tu ya kuwa na macho mekundu na ujinga uliokithiri unaosababisha
Watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kusakwa na kuuawa kikatili kabisa.”
“Nawaombeni sana viongozi wa dini
tusaidiane katika kukomesha ujinga huu mkubwa kwa kutoa elimu kwa waumini wenu,
ili wajue kuwa vikongwe wana macho mekundu kwa sababu ya kutumia samadi ya
ng’ombe kupikia kwa muda mrefu na kuwa kiungo cha albino hakiweza kuleta utajiri
wowote,” Rais aliwaambia viongozi hao wa dini.
Kuhusu madai kuwa Serikali yake
haichukui hatua za kutosha kukabiliana na mauaji ya albino, Rais Kikwete
aliwaambia viongozi hao: “Tumewatia mbaroni watuhumiwa wengi wa
mauaji ya albino. Watu 16 tayari wamehukumiwa kifo na wengine wanasubiri…kesi
zao zinaendelea kusikilizwa. Yapo maneno maneno, lakini binafsi kama Rais
sijaletewa majina ya watu hao.”
Aliongeza: “Ni lazima tuelewe jinsi mfumo
wetu wa kutoa haki unavyofanya kazi hasa katika eneo hilo la kunyonga ama
kutokunyonga. Ni mlolongo mrefu. Katika kesi za watu kuhukumiwa kifo, kwanza
kukata rufani ni lazima na wala siyo jambo la hiari ama matakwa ya
aliyehukumiwa. Pili, tukimalizana na
rufani ni lazima Kamati ya Msamaha (Committee on Prerogative of Mercy) nayo
ifanye kazi. Kwa hiyo ni utaratibu mrefu kidogo.”
Mhashamu Baba Askofu Sangu ambaye
aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francesco kuwa Askofu Februari 2, mwaka huu, 2015,
amechukua nafasi ya hayati Baba Askofu Aloysius Balina ambaye alifariki dunia
Novemba 6, 2012.
Wakati wa uteuzi wake, Mosinyori Sangu
alikuwa anafanya kazi kwenye Idara ya Uenezaji Injili Ulimwenguni katika makao
makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican ambako alifanya kazi kwa miaka minane.
Mwisho.
Imetolewa
na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
13
Aprili,2015
Comments