Copy and WIN : http://ow.ly/KfYkt
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Nukushi: 255-22-2116600
|
|
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI.
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, amesema leo kuwa hakuna
Mtanzania kati ya watu wanane waliouwawa katika mashambulizi dhidi ya wageni
huko Durban na Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.
Mhe. Membe amewaambia
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa taarifa zilizosambazwa na baadhi
ya vyombo vya habari kwamba Watanzania watatu wameuwawa katika mashambulizii
hayo siyo za kweli.
"Nimehakikishiwa
na Waziri wa Usalama wa Afrika kusini, David Mahlobo, asubuhi hii kuwa
hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouwawa, ambao ni raia wa Ethiopia,
Zimbabwe, Malawi na Swaziland," ametaarifu Mhe. Waziri.
Amesema serikali ina
taarifa kuwa kuna Watanzania watatu waliofariki dunia nchini Afrika Kusini,
lakini hawakuuwawa katika mashambulizi ya wenyeji dhidi ya wageni.
"Watanzania hao
ni Rashidi Jumanne, ambaye imetaarifiwa alipigwa risasi katika tukio la
ujambazi, kilometa 90 nje ya mji wa Durban; mfungwa Athumani China Mapepe,
aliyeripotiwa kuchomwa kisu gerezani wakati wa vurugu za wafungwa, na Ali
Heshima Mohamed, ambaye alifariki hospitalini kutokana na ugonjwa wa TB,"
alieleza Mhe. Membe.
Mwili wa marehemu
Mohamed ulirejeshwa nchini jana kwa mazishi. Mhe. Waziri alitaarifu kuwa kuna
Watanzania 23 katika kambi iliyotayarishwa na serikali ya Afrika Kusini huko
Durban kuhudumia wageni wanaokimbia mashambulizi hayo ya wenyeji, na kuwa
utaratibu unafanywa kuwarejesha nyumbani raia 21 walioomba. "Wawili
wamesema hawako tayari kurudi."
Mhe. Membe amesema
taarifa ya serikali ya Afrika Kusini inaonyesha kuwa hali ya utulivu imerejea
Durban na Johannesburg katika saa 48 zilizopita kutokana na juhudi za Rais
Jacob Zuma na kamati maalum ya mawaziri aliyoiteua kushughulikia mashambulizi
hayo.
Mapema jana, Mhe.
Membe alimwita Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Thamsanqa Dennis
Mseleku, na kuelezea kukerwa kwa serikali
na mauaji ya wageni na akataka hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha usalama
wa Watanzania nchini Afrika Kusini
Alisema Tanzania
inaunga mkono taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambayo imelaani
vikali mashambulizi ya Waafrika kutoka nje ya Afrika Kusini. Hata hivyo,
Rais Mugabe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), amesifia hatua
zinazochukuliwa na serikali ya Afrika Kusini kukomesha mashambulizi hayo na
kurejesha utulivu.
Mhe. Membe aliwataka
Watanzania waishio Afrika Kusini na kwingineko nje ya nchi, kujitambulisha
kwenye balozi zetu ili iwe rahisi kufuatilia usalama wao na kuwasaidia pale yatokeapo
majanga.
"Hatuna takwimu
sahihi za idadi ya Watanzania waishio Afrika kusini kwa sababu wengi wao
wamekwenda huko kwa njia za panya," alisema. Inakadiriwa kuna Watanzania
10,000 waishio Johannesburg na Durban.
Akijibu swali la
mwandishi wa habari, Mhe. Membe alisema Tanzania inapaswa kutumia utajiri
mkubwa wa gesi asilia ilionao ili kuendeleza viwanda vidogo, vya kati na
vikubwa vitakavyotengeneza ajira za kuvutia kwa vijana ili wasikimbilie nchi za
nje na kuhatarisha maisha yao.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
20
Aprili 2015.
Comments