WATANZANIA WATAKIWA KUSAIDIA WATU WASIOJIWEZA KWENYE JAMII

  Waziri Membe akizungumaza wakati wa ziara yake kituoni hapo. Kulia ni Mama Dorcas Membe. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Paul Makonda akifuatiwa na Padri Timoth Maganga wa Kanisa Katoliki la Kigogo Mburahati.
Padri Timoth Maganga wa Kanisa Katoliki la Kigogo Mburahati akitoa shukrani zake za pekee kwa Waziri Membe kutembelea kituoni hapo.

Msimamizi wa Nyumba ya Furaha na Amani, Sista Bakitha akiongea machache kumkaribisha Mhe. Membe mara baada ya kufika kituoni hapo akiambatana na mkewe Dorcas na familia yake kwa jumla kusherehekea Siku Kuu ya Pasaka pamoja na Watoto Yatima na Wazee wanaolelewa kwenye kituo cha Nyumba ya Furaha na Amani.
 
 Akinamama walemavu na wasiojiweza wanaolelewa katika kituo hicho.
 Waziri Membe akitoa msaada kwenye kituo hicho
 Waziri Membe pamoja na Mkewe Mama Dorcas Membe katika picha ya Pamoja na Masista wanaolea watoto yatima katika kituo hicho
 Waziri Membe akikata keki pamoja na Sista Bakitha kama ishara ya kusherehekea Siku Kuu ya Pasaka pamoja na Watoto Yatima na Wazee wanaolelewa kwenye kituo cha Nyumba ya Furaha na Amani. Pembeni ni Mama Dorcas Membe nae akifurahia
Waziri Membe akiwalisha keki watoto.
Mama Dorcas Membe akiwalisha watoto keki.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) akimtazama kwa furaha mmoja wa watoto yatima wanaolelewa kwenye kituo cha Nyumba ya Furaha na Amani kilichopo Kigogo Mburahati, Jijini Dar es Salaam. Waziri Membe alikitembelea kituo hicho wakati wa Siku Kuu ya Pasaka.
Mhe. Membe pamoja na Mkewe Mama Dorcas Membe wakipata maelezo juu ya watoto waishio katika kituo hich kutoka kwa Sista Mary Bakhita.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuwasaidia watu wasiojiweza waliopo kwenye jamii wakiwemo watoto yatima, walemavu, wazee na wajane.

Waziri Membe ametoa wito huo hivi karibuni alipotembelea Kituo cha Kulelea Watoto Yatima na Wazee cha Nyumba ya Furaha na Amani kilichopo Mburahati Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Membe alisema kuwa katika jamii za watu kumekuwa na makundi ambayo yanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa watu wengine ambao kwa namna moja au nyingine wamejaaliwa kipato kidogo na afya. Alisema kuwa ni wajibu wa watu wa aina hiyo kuwasaidia wale wanaohitaji kama vile watoto yatima, walemavu, wazee na wajane.

Waziri Membe ambaye alikuwa amefuatana na Mke wake, Mama Dorcas Membe aliguswa sana na historia ya baadhi ya watoto yatima aliowatembelea kituoni wakiwemo wale waliotupwa jalalani na kuokotwa wakiwa kwenye hali mbaya.

“Lipo kundi linalopata mateso na matatizo katika jamii zetu tunazoishi. Ni vizuri Watanzania tukajenga utamaduni wa kutembelea sehemu kama hizi ili kujionea wenyewe hali halisi.

Kwa kweli ni hali ya kusikitisha kuona baadhi ya watoto walitupwa na kuokotwa jalalani na wengine tayari wakiwa wamepata majeraha ya kung’atwa na mbwa. Hivyo ni wajibu wetu sote kuwasaidia kwa chochote kidogo tunachojaaliwa kupata”, alisema Waziri Membe.

Aidha, Mhe. Membe aliwapongeza na kuwasifu Masista wa Shirika la Mama Theresa ambao ndio wasimamizi wa kituo hicho kwa kuwalea watoto, vijana na wazee wenye matatizo mbalimbali na kuwaomba waendelee kujipa moyo katika kazi hiyo kwani ni njia moja wapo ya kumtumikia Mungu.

Awali akimkaribisha Waziri Membe kituoni hapo, Sista Mkuu wa Kituo hicho, Sista Mary Bakhita, alisema kuwa wamefurahia sana ziara hiyo ya Mhe. Membe hususan katika Siku Kuu ya Pasaka kwani ni faraja kubwa kwao kwa Watoto na Wazee wanaolelewa kituoni hapo.

“Tumefarijika sana kula pasaka pamoja nawe Mhe. Waziri. Watoto na Wazee hawa wanajisikia vizuri pale wanapotembelewa na tunaomba uendelee na moyo huo huo”, alisema Sista Bakhita.

Wakati wa ziara hiyo Mhe. Membe na familia yake walitoa zawadi mbalimbali kwa kituo hicho ikiwemo vyakula, sabuni na fedha kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali kituoni hapo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI