HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, AKIFUNGUA MKUTANO WA NNE WA MABALOZI WA TANZANIA TAREHE 25 MEI, 2015 KATIKA HOTELI YA RAMADA - DAR ES SALAAM

Rais
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano wa Nne wa Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi. Mkutano huo umefanyika katika Hoteli ya Ramada Jijini Dar es Salaam ukiwa umebeba Kaulimbiu isemayo “Diplomasia ya Tanzania 

Mhe. Bernard Kamillius Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
Balozi Hassan Simba Yahya, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
Mabalozi wote;
Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;


Shukran na Pongezi
Nakushukuru wewe Mheshimiwa Waziri na Viongozi wenzako wa Wizara kwa kunialika kushiriki ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Mabalozi wa Tanzania. Mkutano huu ni wa pili katika awamu yangu na wa nne baada ya ule wa tatu uliofanyika Zanzibar, mwaka 2008.  Nafarijika kuona kuwa Wizara imeendelea na utaratibu huu mzuri wa kuwakutanisha Mabalozi kujadili utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya nchi yetu. Utaratibu huu unatoa fursa ya kujitathmini, kupeana mrejesho na kuweka malengo na mikakati mipya.  Ni matumaini yangu kuwa utaratibu huu mzuri utaendelezwa na Serikali zinazofuatia.
Kauli Mbiu
Mheshimiwa Waziri;
Nimeipenda kauli mbiu ya Mkutano inayosema “Diplomasia ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025”. Imebeba ujumbe muafaka hasa ukizingatia kuwa tuko katika hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya kuanza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka 5. Kama mjuavyo Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Muda Mrefu wa miaka 25 unaotekelezwa kwa Mipango mitatu ya muda wa kati wa miaka mitano kila mmoja  kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa. Shabaha kuu ya Dira hiyo ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Kama tunavyofahamu, Sera ya Mambo ya Nje ni muendelezo wa sera ya ndani, hivyo ni jambo la busara kuitana na kukumbushana nafasi na wajibu wa Wizara katika kuchangia jitihada za Serikali kufikia lengo hilo. Nimefurahishwa na mada mlizochagua na watu mliowaalika. Naamini mkutano huu utakuwa na mafanikio makubwa.
Hali ya Dunia
Waheshimiwa Mabalozi;
Sote tunafahamu kuwa tangu kuzinduliwa kwa Sera ya sasa ya Mambo ya Nje, mwaka 2004, mambo mengi yamebadilika. Hii ni kweli kwa hapa nchini na hata duniani.  Mafanikio mengi yamepatikana na changamoto kubwa na ndogo zimejitokeza. Kuyumba kwa uchumi wa dunia mwaka 2002 na 2009 kumekuja na athari nyingi hususan kwa nchi maskini na zinazoendelea. Misaada ya maendeleo kutoka nchi tajiri imepungua na masoko ya bidhaa zetu kama pamba, tumbaku na dhahabu yamekuwa yanayumba. Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto nyingine ambayo inatishia ustawi wa nchi maskini. Bado majadiliano na nchi zilizoendelea yanaendelea ili watimize wajibu wao wa kihistoria wa kutusaidia kujenga uwezo wetu wa kukabiliana na athari zake. Hivi sasa sote tumeweka matumaini yetu kwenye mkutano wa Paris, Desemba 2015 kupata mkataba ulio bora. Tusipofanikiwa itakuwa hatari kubwa. Tanzania iendelee na jitihada zake kama tulivyofanya wakati wa kuongoza Kamati ya Marais wa Umoja wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (CAHOSCC).  
Ndugu Mabalozi;
Vitendo vya uhalifu wa kimataifa na ugaidi navyo vinazidi kushamiri duniani na kutuathiri hata sisi. Zamani tulikuwa tunasikia mambo hayo yakitokea nchi za mbali, lakini, hivi sasa nasi ni wahanga wa uhalifu huo. Mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya inaangamiza vijana wetu. Hivyo basi lazima tushiriki katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.   Ndovu wetu wanatishiwa kumalizwa na majangili  na washirika wa  mitandao ya kimataifa; na matishio ya ugaidi yanaviweka vyombo vya ulinzi na usalama kuwa katika hali ya tahadhari wakati wote. Majawabu ya changomoto hizi hayawezi kupatikana kwa juhudi za nchi moja peke yake, yanahitaji ushirikiano na jumuiya ya kimataifa. Mabalozi mnao wajibu wa kuendelea kutafuta wabiya wa kushirikiana nasi katika mpambano haya.
Utandawazi unaostawishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia umeleta fursa na una changamoto zake nyingi pia. Ukweli huo ndiyo iliyotufanya kutunga Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Mitandaoni (Cyber Crime Act) hivi karibuni.  Vilevile, Jumuiya za Kikanda zinazidi kuimarika katika kila kona ya dunia. Tanzania ni mwanachama wa EAC na SADC. Ushiriki wetu umekuwa na tija na kuleta maslahi ya kiuchumi na kibiashara. Hata hivyo hatuna budi kujituma na kujipanga vizuri zaidi ili tuweze kunufaika zaidi.
Mafanikio ya Diplomasia ya Tanzania
Waheshimiwa Mabalozi;
Pamoja na mabadiliko hayo na changamoto zake, inatia moyo kuona diplomasia ya nchi yetu imeendelea kustawi. Tanzania ina jina kubwa kikanda na kimataifa kuliko nguvu zetu za kiuchumi na kijeshi. Kwa ajili hiyo tumekuwa tunaaminiwa na kushirikishwa katika shughuli na mambo mbalimbali.  Tumeendelea kuwa sauti ya watu wasio na sauti na wanyonge na kuwa kimbilio lao.  Ni kwa ajili hiyo tumeaminiwa katika majukumu muhimu na Jumuiya za kikanda na kimataifa hususan AU, SADC na UN. 
Jambo lingine la kujivunia sote kuhusu diplomasia yetu ni kuwa na uhusiano mzuri na nchi jirani na mashirika ya kimataifa. Nimeingia madarakani  Tanzania ikiwa haina adui, na naondoka bila adui. Kwa jumla tumefanikiwa kuimarisha udugu, urafiki na ushirikiano na majirani zetu wote.  Pale palipotokea upepo mbaya, tumetumia njia za kidiplomasia kuondoa tofauti zetu tukiongozwa na hekima ya wahenga kuwa: “unaweza kuchagua rafiki lakini huwezi kuchagua jirani”.
Hali kadhalika, tumepokea wageni wengi waliofanya ziara nchini ikiwemo marais wa mataifa makubwa duniani yakiwemo Marekani na China.  Ziara hizo ziliitangaza nchi yetu na kufungua milango ya fursa kwa nchi yetu ya kunufaika kwa misaada ya maendeleo, biashara na vitega uchumi.
Vilevile, tumepanua wigo wa mahusiano kwa kuongeza marafiki na wabia wengine wa maendeleo. Katika kipindi cha miaka 10 nchi 6 za Brazil, Oman, Uturuki, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Namibia zimefungua ubalozi nchini Tanzania.  Aidha, nchi 16 za Morocco, Malta, Equador, Montenegro, Azerbaijan, Bosnia na Herzegovina, Moldova, Saint Vincent na Grenadies, Fiji, Paraguay, Kosovo, Geogia, Kyrgyzstan, Visiwa vya Marshall, Visiwa vya Solomon, na Kazakhstan zimeanzisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi yetu. Nchi yetu pia imefungua Ofisi za Ubalozi katika nchi 7 za Brazil, Uholanzi, Malaysia, Oman, Kuwait, UAE na Comoro.  Kama hali itaruhusu tunatarajia kufungua Ubalozi nchini Uturuki na Algeria kabla ya kumaliza kipindi changu cha uongozi.
Mahusiano haya mapya na yale ya zamani ambayo tumeendelea kuyapalilia yamefungua fursa nyingi kwa nchi yetu na watu wetu.  Mahusiano haya yametuwezesha kupata mikopo na misaada ya kimaendeleo ambayo imeziongezea Serikali zetu mbili: Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo.  Tunapojisifu leo hii kwa hatua kubwa katika kujenga miundombinu msingi ya mawasiliano, uchukuzi na nishati na upanuzi na uboreshaji mkubwa wa huduma za jamii kuna michango muhimu ya wadau wa nje. Haya ni matokeo chanya kazi yenu nzuri ya kuyajenga na kuyastawisha mahusiano mazuri na mataifa.  Miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme, barabara, bomba la gesi, viwanja vya ndege, mkongo wa taifa ni matokeo ya mahusiano hayo.  Nawashukuru sana kwa mchango wenu huo.
          Maeneo mawili mapya katika Sera yetu ya Mambo ya Nje katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ni ushirikishwaji wa Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) na ushiriki wa Ulinzi wa Amani (Peace-keeping Operation).  Ni katika kipindi hiki tumetunga Sera ya Diaspora na kuamsha hamasa ya kuwatambua na kuwashirikisha Watanzania wenzetu waishio nje katika gurudunu la maendeleo. Hatukuweza kukidhi haya yao ya uraia pacha lakini tumefanikiwa kuwapa haki mahsusi kwenye Katiba Pendekezwa. 
Tumeshiriki katika shughuli za ulinzi wa amani kule Darfur Sudan, Lebanon na DRC chini ya operesheni za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.  Aidha, tumeshiriki  katika utatuzi wa migogoro katika bara la Afrika ukiwemo ule wa Comoro na kurejesha umoja wa nchi hiyo.
Mpango wa Taifa 2015 – 2020
Waheshimiwa Mabalozi,
Mafanikio niliyoyataja ni sehemu tu ya mafanikio mengi tuliyoyapata katika kutekeleza Sera yetu ya Nje. Nchi yetu iko salama na haina maadui bali marafiki duniani kote. Tumefanikisha kuvutia misaada ya maendeleo, vitega uchumi na biashara, mambo ambayo yamechangia  katika jitihada za nchi yetu kukuza uchumi na kupunguza umaskini.  Jukumu kubwa lililo mbele yetu ni kutumia fursa zetu kuwa na mahusiano mazuri na mataifa na mashirika ya kimataifa pamoja na ya kijiografia na maliasili yetu kujenga uwezo wetu wa kiushindani kikanda na duniani.
Mheshimiwa Waziri;
Mtakumbuka kuwa, malengo makuu ya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano tunaomalizia ulilenga kuondoa vikwazo vya ukuaji wa uchumi. Shabaha yake ni:
(a)            kujenga uwezo wa nchi yetu kukuza uchumi na kuondoa umaskini haraka;
(b)           kujizatiti kutumia fursa zilizopo nchini kukuza mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi yetu na nyingine katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa;
(c)             Kukuza ajira ili kupunguza tatizo la ajira linalowakabili vijana.
Siwezi kusema tumefanikiwa kila kitu, lakini tumepiga hatua ya kuridhisha na tumeonyesha muelekeo mzuri.  Hali ya uchumi kwa maana ya viashiria vya uchumi jumla, tupo mahali pazuri.  Pato la Taifa limekuwa kwa wastani wa asilimia 7 na kuongezeka kutoka Dola za Kimarekani bilioni 14.4 mwaka 2005 hadi Dola za Kimarekani bilioni 43 mwaka 2015. Hivyo hivyo, pato la wastani la Watanzania nalo limeongezeka kutoka Dola za Kimarekani 375 mwaka 2005 hadi Dola za Kimarekani 944 mwaka 2014.
Katika kipindi cha muongo mzima sasa, makusanyo ya kodi yameongezeka kutoka shilingi billion 177.1 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 800 mwaka 2015. Tumefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kutoka asilimia 18 mwaka 2011 hadi asilimia 4.5 mwaka huu. Hivi karibuni thamani ya sarafu yetu imekua inapungua dhidi ya dola ya Marekani. Hatuko peke yetu thamani ya dola ya Marekani imepanda dhidi ya sarafu zote duniani. 
Katika kipindi hiki pia tumefanikiwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji yaani upanuzi na uboreshaji wa bandari, ujenzi wa barabara na uimarishaji wa reli na uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini. Aidha, tumerekebisha baadhi ya sheria zilizokuwa zinatukwamisha ili kuboresha mazingira ya uwekezaji.  Nimefurahi kuwa katika mkutano huu wahusika watapata fursa ya kuzungumza na Mabalozi kuhusu maeneo hayo. Kwa ujumla, tumeweka msingi mzuri wa ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kuelekea mwaka 2025.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka 5 ambao tunauanza katika mwaka wa fedha ujao, unalenga katika kuhamasisha mapinduzi ya viwanda kwa lengo la kuongeza thamani ya maliasili zetu na bidhaa za kilimo, kujenga uwezo wetu wa biashara ndani na nje ya eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukuza ajira. 
Mpango huu unalenga kujenga juu ya mafanikio ya mpango wa kwanza. Hivyo, utekelezaji wa mpango huu unahitaji sana tuvutie vitega uchumi na teknolojia za kisasa nchini kwa lengo la kuchochea mapinduzi ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.  Tukifanikiwa katika haya tutaweza kuitumia vizuri fursa tulizonazo na ile ya kijiografia ya kuzungukwa na soko kubwa.
Ndugu Waziri na Ndugu Mabalozi;
Nchi inawategemea ninyi kutumia nafasi mlizonazo kuvutia wawekezaji zaidi, teknolojia za kisasa na kutafuta masoko ya bidhaa zetu.  Hili ni jukumu lenu la msingi katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. Nawataka muwe wabunifu na makini katika kuwaunganisha wafanyabiashara wa nchini na wenzao wa nje mnakowakilisha nchi yetu.  
Katika dunia ya sasa na huko tuendako, usalama na ustawi wetu utategemea zaidi uwekezaji na biashara na si misaada ya maendeleo ambayo imeendelea kuwa isiyotabirika na isiyotosha.  Hamna budi sasa kuongeza msukumo kwenye kuvutia watalii, wawekezaji, kutafuta masoko na kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania kufanya biashara nje.  Ningefarijika sana kama mtajipima na kujisifu kwa uchangiaji wenu kwa uchumi na kuwawezesha wafanyabiashara wetu kujitanua kimataifa. 
Zama za sasa haitoshi kujisifu kwa uhodari wa kuandika ripoti na kuhudhuria mikutano. Tujisifu pia kwa kuchangia kukuza uchumi wa nchi. Ni vizuri kujiuliza mtachangia vipi kuwezesha uchumi wetu kukua na hivyo uwezo wa Serikali kuongezeka kipato ili bajeti za balozi ziweze kuongezeka.  Kila mtu ajiulize ubalozi wake umechangia nini na kiasi gani? Je, nini kifanyike ili ubalozi huo uweze kuchangia zaidi.  Ni matumaini yangu kuwa mkutano huu utatafuta majawabu na maswali haya.  Huo ndio mtazamo chanya wa kuelekea nchi ya uchumi wa kati mwaka 2015.
Waheshimiwa Mabalozi;
Mnatakiwa pia kutafuta wabia wapya wa maendeleo na kuimarisha ushirikiano nao. Hawa siyo wengine bali ni mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na Watanzania wenzetu waishio nje (Diaspora). Nchi zinazotoa misaada ya maendeleo hupitishia kiasi kikubwa mikononi mwa NGOs. Aidha, mifuko ya misaada ya watu binafsi Bill and Melinda Gates Foundation zinatoa michango muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wakati mwingi inazidi hata ile tunayopata kutoka nchi wahisani. Bado ipo nafasi ya kuongeza ushiriki wa taasisi za namna hii kwa maendeleo yetu. Isitoshe taasisi nyingine zina ushawishi mkubwa kwa mashirika ya kimataifa, Serikali na sekta binafsi. Hivyo basi, tukiweza kuimarisha uhusiano na taasisi hizi tutafaidika katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo.
Watanzania wanaoishi nje ya nchi nao wanaweza kutoa mchango  muhimu. Mazungumzo yangu nao yanaendelea kuzaa matunda. Wengi wameonesha hamasa kubwa ya kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo nyumbani. Zipo nchi duniani zinazonufaika na diaspora zao na sisi inaweza kuwa hivyo. Tumeanza lakini bado tunahitaji kuongeza juhudi. Mkutano huu uje na mawazo mazuri juu ya nini kifanyike kuwafanya Watanzania walio nje wachangie zaidi ya wafanyavyo sasa.  Tuangalie wenzetu hao wanafanya vipi na kuiga yale mazuri tuyafanye.
Uboreshaji wa Maslahi na Mazingira ya Kazi ya Watumishi wa Nje
Mheshimiwa Waziri;
Waheshimiwa Mabalozi,
          Katika kipindi cha Awamu ya Nne tumeendelea kuboresha mazingira ya kazi ya Balozi zetu na maslahi ya watumishi wake.  Nasema tumejitahidi kwa kuwa tofauti na watumishi wa kada nyingine serikalini, kada ya utumishi wa nje mahitaji yake ya kifedha ni makubwa sana. Hii ni kutokana na kuzingatia mazingira yao ya kufanyia kazi nje ya nchi yetu.  Tumeendelea kuiboresha hali kadri uwezo wetu wa fedha uliporuhusu.  Ninyi ni mashuhuda wa maboresho ya msingi tuliyoyafanya katika Kanuni za Watumishi wa Nje (Foreign Service Regulations). Tumerekebisha viwango vya posho ya nje (Foreign Service Allowance), posho ya wenza na ya elimu kwa watoto wa watumishi wakiwa ubalozini.  Aidha, tumewapatia balozi vitendea kazi ikiwemo magari ya uwakilishi yenye hadhi na heshima inayolingana na Balozi. 
Kutokana na kuanza kutengwa fedha za maendeleo, Wizara imeweza kununua na kujenga majengo ya ubalozi ambayo pia ni vitega uchumi. Tumefanya hivyo New York, Washington DC na Paris.  Tunatarajia kujenga majengo ya namna hiyo Nairobi na Oman.  Pamoja na ununuzi, tumeendelea na ukarabati wa majengo mengi ya Balozi zetu katika kuboresha taswira ya nchi yetu nje.  Lengo letu ni siku nyingine tuachane na kupangisha majengo ya ofisi na kuishi katika Balozi zetu bali yawe mali yetu. Kwa kuwa ni vitega uchumi pia vitega uchumi na hivyo kutaziongezea Balozi mapato na uwezo wa kujiendesha bila kutegemea sana fedha kutoka nyumbani.
           
Vilevile, kuna haja kwa Wizara kujenga uwezo wa maafisa waliopo na watakaoajiriwa kupitia mafunzo na kupata uzoefu kwa kutenda. Ninachozungumzia hapa ni  kuwa na maafisa wenye uelewa mtambuka na uwezo wa kuchambua mambo na kushiriki ipasavyo kwenye majadiliano ya kimataifa. Wasiwe wasikilizaji tu bali wawe washiriki makini wanaofahamu maslahi ya nchi na kuyalinda.  Chuo cha Diplomasia kiendelezwe kwa ajili ya kuandaa wanadiplomasia wetu.  Pia tuwapeleke watumishi wetu kuongeza elimu katika vyuo mbalimbali duniani. Aidha, mnapaswa sana kupanua wigo wa ujuzi wa maafisa wetu.  Muwe na mchanganyiko wa taalama nje zaidi ya uhusiano wa kimataifa.  Mnahitaji wataalamu wa elimu ya fani za uchumi, biashara ya kimataifa, nishati na nyinginezo.
Mheshimiwa Waziri na viongozi wenzako;
Mabalozi;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nashiriki Mkutano huu kwa mara ya mwisho nikiwa Rais wa Nchi yetu. Hivyo, napenda kutumia nafasi hii kuwaaga rasmi. Naondoka nikiwa na kumbukumbu nzuri kwenu kwani tumefanikiwa mengi pamoja.  Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Bernard Membe kwa ushirikiano na msaada wako mkubwa na wenzako katika kunisaidia katika eneo langu hili kwa miaka tisa.  Naelewa ugumu na uzito wa jukumu lenyewe maana name niliwahi kuwa  Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10.  Nakupongeza kwa jinsi ulivyoongoza vizuri Wizara hii nyeti na mafanikio mliyoweza kupata. Hii ni Wizara ambayo haikuwahi kuninyima usingizi katika kipindi cha uongozi wangu. Naondoka nikiwa na faraja kuwa Diplomasia yetu iko katika hali nzuri.  Nina imani kuwa wanadiplomasia wetu watafanya Watanzania tuendelee kutembea kifua mbele.  Daima mkumbuke ule msemo wetu, “Better than yesterday, Less than Tomorrow” yaani tuhakikishe tunafanya vizuri kuliko jana, ingawaje ni pungufu kuliko kile tutakachofanya kesho.
Inawezekana, timiza wajibu wako.
Asanteni sana kwa kunisikiliza

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*