HOTUBA YA RAIS
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA
KILELE CHA MAADHIMISHO YA PILI YA KITAIFA YA WIKI YA ELIMU TANZANIA UWANJA WA
JAMHURI, DODOMA - TAREHE 15 MEI, 2015
Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb), Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi;
Mheshimiwa Hawa
Ghasia (Mb), Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
Waheshimiwa
Manaibu Waziri;
Mheshimiwa Chiku Galawa; Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Mheshimiwa Magreth Sitta (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Huduma za Jamii;
Waheshimiwa
Wabunge;
Balozi Ombeni
Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi;
Makatibu Wakuu
na Naibu Makatibu Wakuu;
Washirika wa
Maendeleo;
Wadau wa
Maendeleo ya Elimu;
Viongozi wa
Serikali na Mashirika ya Dini;
Walimu na Wanafunzi;
Ndugu
Wanahabari;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na
Mabwana.
Shukrani
Ninayo furaha
kubwa ya kuungana nanyi leo katika kuhitimisha maadhimisho haya ya pili ya
kitaifa ya wiki ya elimu. Nakushukuru wewe, Mheshimiwa Waziri na viongozi
wenzako wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kunipa heshima hii kubwa ya
kushiriki maadhimisho haya.
Pia,
nawashukuru na kuwapongeza kwa dhati viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa
na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Chiku Galawa kwa kukubali kuwa wenyeji wa maadhimisho
haya kwa mara ya pili mfululizo. Vile vile, napenda kuipongeza Kamati ya Maandalizi ya Kilele cha Maadhimisho ya Pili ya Kitaifa ya Wiki ya
Elimu Tanzania kwa kazi nzuri waliyofanya ya kufanikisha shughuli hii.
Kwenu wote nasema hongereni sana!
Kauli
Mbiu
Ndugu Waziri;
Ndugu wananchi;
Nimefurahishwa na
kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Elimu Bora ni Haki ya Kila Mtoto kwa Maendeleo ya Taifa”. Kauli
mbinu hii ni muafaka kabisa kwa kuwa kupata
elimu ni moja ya haki ya msingi ya mtoto. Tena lazima apate elimu iliyo bora.
Aidha kauli mbiu inaakisi kwa usahihi madhumuni na malengo ya Serikali katika
hatua inazochukua kuendeleza elimu nchini. Kuwapatia Watanzania elimu bora ndiyo
shabaha ya msingi ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka
2014 niliyoizindua mapema mwaka huu. Pia
ndiyo shabaha ya Sera zilizokuwepo kabla ya hii tangu uhuru mpaka sasa. Tulichokifanya katika awamu hii ni kutoa
msukumo mkubwa zaidi katika kuendeleza elimu.
Kama ilivyokuwa kauli mbiu yetu ya ari Mpya, Nguvu Mpya na Ari Mpya na
baadae ile ya Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa tumepata mafanikio ya kutia moyo ingawaje
bado tuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu.
Tuliamua kuanzisha maadhimisho ya Wiki ya Elimu nchini kwa malengo mawili.
Kwanza, kuelimisha Watanzania kuhusu jitihada
zinazoendelea kufanyika na hatua tunazopiga katika kuboresha elimu na kuongeza
fursa kwa watoto wetu na Watanzania kwa ujumla kupata elimu. Pili,
kutambua na kuwatunza waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za elimu.
Chanzo cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu
Ndugu Wananchi;
Katika kuboresha utendaji wa Serikali na kutekeleza mipango na
ahadi zake tulibuni Mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN).
Katika mpango huo Elimu ilikuwa miongoni mwa sekta sita za mwanzo, nyingine
zikiwa maji, kilimo, nishati, miundombinu na mapato ya serikali. Baadae tumeongeza mazingira ya uwekezaji na
afya.
Baada ya kufanya uchambuzi wa hali ilivyo na kutafuta ufumbuzi wa
changamoto zilizopo katika elimu ilikubaliwa mambo tisa kupewa kipaumbele. Mambo hayo ni:-
(i)
Upangaji wa shule kwa
ubora kwa matokeo ya mtihani kitaifa kuanzia shule iliyoongoza hadi ya mwisho.
(ii)
Uratibu wa utoaji wa tuzo
kwa shule zilizofanya vizuri,
(iii)
kuwa na kiongozi cha
usimamizi wa shule,
(iv)
Upimaji wa kitaifa wa
stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu,
(v)
Mafunzo kwa walimu kwa
stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu,
(vi)
Kujenga uwezo wa walimu na
wanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji,
(vii)
Ujenzi wa miundo mbinu
muhimu ya shule; madarasa,
(viii)
Utoaji ya ruzuku wa
uendeshaji wa shule na,
(ix)
Utoaji wa motisha kwa
walimu.
Kuhusu utoaji wa tuzo naipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kwa uamuzi wa busara kuwa tuzo hizo zitolewe kwenye kilele cha
Maadhimisho ya Wiki ya elimu.
Ndugu Wananchi;
Ni matazamio yetu kuwa utoaji wa tuzo hizi utakuwa kichocheo cha
kujenga ari, hamasa na tabia ya ushindani wa kitaaluma ndani ya mfumo wa Elimu.
Jambo hilo litasaidia kuinua ubora na ufanisi katika ngazi zote za elimu. Ushindani wa kitaaluma utasababisha kuongezeka
kwa ufanisi na uwajibikaji katika kufundisha na kujifunza na hatimaye kuendelea
kuboresha uelewa wa wanafunzi na kuwafanya wawe na matokeo mazuri.
Tuzo kwa Waliofanya Vizuri katika Mitihani ya Taifa ya
Mwaka 2014 na Uandishi wa Insha za Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
Ndugu wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa wale wote
waliopata Tuzo. Wahenga wamesema “mcheza
kwao hutunzwa”. Siku hii ya leo, jumla ya shule 20 na wanafunzi 20 waliofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya Taifa ya darasa
la saba na kidato cha nne mwaka 2014 wamepokea zawadi na tuzo. Nazipongeza sana
shule zetu hizi na wanafunzi wote hawa kwa ushindi waliopata. Aidha jumla ya
shule 3,090 yaani 2,166 za msingi na 924 za sekondari zilizopata ufaulu uliotukuka na nyingine kuongeza ufaulu
kwa kiwango cha juu zitapata tuzo na zawadi stahiki.
Mheshimiwa
Waziri;
Ndugu
wananchi;
Niruhusuni pia nitoe pongezi kwa vijana 13 walioitoa nchi yetu kimasomaso katika mashindano ya uandishi wa
insha yanayoendeshwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Umoja
wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Hongereni Sana.
Hali kadhalika, natoa pongezi maalum kwa wale vijana
watatu (3) waliopata ushindi kwa
kuandika insha bora na wengine watatu
(3) waliochora picha bora kuhusiana na kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka 2015.
Naomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
wakishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
kuongeza wigo wa mashindano ya kitaaluma kwa wanafunzi. Naamini kufanya hivyo
kutasaidia kuibua vipaji vya watoto wetu tangu wakiwa wadogo. Tusiishie hapo,
nawasihi walimu, wazazi, walezi na jamii nao wahakikishe kuwa vipaji hivi
vinaendelezwa.
Ndugu Wananchi;
Maadhimisho
haya yanatukumbusha sote juu ya wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika
shughuli za maendeleo ya shule na ufuatiliaji wa karibu wa shughuli zote
zinazofanyika shuleni kwa lengo la kumuwezesha kila mtoto kupata elimu bora. Ni
ukweli ulio wazi kwamba wajibu wa kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora
si wa Serikali pekee, bali pia ni wa wazazi na walezi wanaoishi na watoto na
jamii kwa ujumla. Daima tukumbuke kuwa watoto hawaishi Serikalini bali kwenye
familia na jamii hivyo wazazi, walezi na jamii ina nafasi maalum katika maendeleo
ya mtoto kwa upande wa elimu na mambo mengine maishani.
Maendeleo
katika Sekta ya Elimu Nchini
Ndugu Wananchi;
Katika kipindi
cha miaka kumi iliyopita tumeweza kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu
nchini. Ninyi mliopo hapa ni wadau muhimu hivyo ni mashahidi wa mafanikio
tuliyoyapata ambayo ni matokeo ya kuongezeka kwa shule, idadi ya wanafunzi,
idadi ya walimu, vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Katika kipindi
hicho, Shule za msingi zimeongezeka kutoka shule 14,257 mwaka 2005 hadi kufikia shule 16,343 mwaka 2014. Hii imefanya idadi ya wanafunzi kuongezeka kutoka
milioni 7.54 hadi kufikia milioni 8.23. Kwa upande wa shule za sekondari,
idadi yake imeongezeka kutoka shule 1,745
mwaka 2005 hadi kufikia shule 4,576 mwaka
2014. Hali kadhalika, idadi ya wanafunzi wa shule za sekondari imeongezeka
kutoka wanafunzi 524,325 mwaka 2005 hadi
kufikia wanafunzi 1,804,056 mwaka
2014.
Jumla ya walimu wote wa msingi na sekondari
idadi imeongezeka kutoka 153,767 mwaka
2005 hadi 301,960 mwaka 2015. Katika kipindi hicho, vyuo vya ufundi
vimeongezeka kutoka 184 mwaka 2005
hadi 744 mwaka 2015. Wanafunzi wa elimu ya ufundi nao wameongezeka
kutoka 40,059 mwaka 2005 hadi 145,511 mwaka 2015. Kwa upande wa elimu
ya juu, wanafunzi wa vyuo vikuu wameongezeka kutoka 40,719 mwaka 2005 hadi 200,986
mwaka 2014. Hii ni kutokana na kuongezeka kwa vyuo vikuu na vyuo vikuu
vishiriki vimeongezeka kutoka 26 mwaka
2005 hadi 52 mwaka 2015. Upanuzi huu mkubwa katika udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu
umewezekana kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi na
kuruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu vya binafsi navyo wapatiwe mikopo. Bajeti iliongezwa kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 345 mwaka 2015 na kunufaisha wanafunzi 98,000 mpaka sasa.
Ndugu Wananchi;
Mafanikio haya
ni matokeo ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa elimu katika bajeti ya serikali. Leo
hii bajeti ya sekta ya elimu ndiyo kubwa kuliko zote nchini ambayo sasa imefikia
shilingi trilioni 3.4 ikilinganishwa
na shilingi bilioni 669.5 mwaka 2005.
Tumefanya hivyo kwa kutambua kwamba kuwekeza kwenye elimu ni kuwekeza kwenye uhai
na maendeleo ya taifa na watu wake sasa na miaka mingi ijayo. Tusipowekeza
kwenye elimu, Watanzania hawataweza kutawala mazingira na raslimali zao na
kuzitumia kujiletea maendeleo. Taifa lisilowekeza katika elimu, halina nafasi
huko tuendako.
Ndugu wananchi;
Ukiacha sababu hizo, jambo lingine lililotufanya tuongeze sana
bejeti ya elimu ni ule ukweli kwamba, wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia
madarakani mwaka 2005 Tanzania ilikuwa nyuma kwa wanafunzi wa elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu
kuliko Kenya na Uganda. Lakini nchi yetu ndiyo kubwa kuliko nchi zote katika
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Takwimu
zilizopo zinaonesha kuwa mwaka 2005, Tanzania ilikuwa na wanafunzi wa shule za
sekondari 524,325 wakati Uganda
ilikuwa na wanafunzi 728,393 na
Kenya 925,341. Kwa upande wa vyuo
vikuu Tanzania ilikuwa na wanafunzi 40,719,
wakati Uganda ilikuwa na wanafunzi
124,313 na Kenya ilikuwa na wanafunzi 108,407.
Kwa kuwa nyuma ya wenzetu katika utoaji wa fursa ya elimu kwa
vijana wetu kulituweka pagumu katika kutoa ushindani katika soko la jumuiya ya
Afrika Mashariki. Wakati ule wazazi
wengi walilazimika kupeleka watoto wao kusoma Uganda na Kenya. Tukafanya uamuzi
wa makusudi kuongeza uwekezaji kwenye elimu ili fursa ya kupata elimu ya
msingi, sekondari na chuo kikuu ziongezeke hapa hapa nchini. Kwa upande wa elimu ya msingi tulijenga shule
mpya na kuongeza madarasa pale ilipohitajika.
Kwa upande wa sekondari tukaanzisha mkakati wa kujenga shule ya
sekondari kwa kila kata na kwa elimu ya juu tulihimiza wadau wengine kujenga
vyuo vikuu na serikali kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wote. Sisi tulionesha mfano kwa kujenga Chuo
Kikuucha Dodoma, Chuo cha Nelson Mandela na kuanzisha Chuo cha Mbeya na sasa
tunajenga Chuo Kikuu cha Kilimo Butiama.
Matokeo ya uamuzi huo na hatua hizo ni kuongezeka sana kwa shule
za sekondari na vyuo vikuu nchini. Kwa sababu hiyo ilipofikia mwaka 2013 hali
ilikuwa tofauti kabisa. Wanafunzi katika shule za sekondari Tanzania walifikia milioni 1,804,056 na vyuo vikuu 200,986. Wenzetu wa Kenya bado wanatuzidi
kwa kuwa na wanafunzi wa sekondari 2,104,300
na vyuo vikuu 324,600. Lakini,
tuliweza kuipita Uganda iliyokuwa na wanafunzi wa shule za sekondari 1,362,739 na wa vyuo vikuu 140,403. Leo tuko mahala ambapo
tunaweza kusema tunashindana kisawa
sawa na wenzetu.
Mafanikio hayo makubwa katika sekta ya elimu hayakutokana na nguvu
za Serikali peke yake. Haya ni mafanikio
yaliyotokana na mchango mkubwa wa wananchi na wadau wengine. Wananchi
walijitolea nguvu zao na chochote walichokuwa nacho kujenga shule za sekondari na
msingi nchini kote. Aidha, huwezi kutaja mafanikio haya bila ya kutambua
mchango mkubwa wa taasisi na mashirika ya dini na sekta binafsi ambao wamejenga
shule za msingi na sekondari
pamoja na vyuo vikuu.
Tunayo kila sababu ya kujipongeza na kujivunia matokeo haya na
matunda ya kazi yetu nzuri. Wakati huo huo tunaendelea kukumbushana umuhimu wa
kuendelea na kazi muhimu ya kuongeza ubora wa elimu waipatayo watoto wetu
katika ngazi zote.
Suala la kuongeza ufaulu katika mitihani ya darasa la saba na
kidato cha nne ni miongoni mwa malengo makuu ya Mkakati wa Matokeo Makubwa
sasa. Kwa mujibu wa BRN malengo ya ufaulu kwa kidato cha nne umetakiwa uwe asilimia 60 mwaka 2013 na asilimia 80 mwaka 2014. Kiwango cha ufaulu kwa kidato cha nne hivi sasa ni asilimia 69.7. Kwa upande wa darasa la
saba, malengo yalikuwa kufikia asilimia
60 mwaka 2013 na asilimia 80 mwaka 2014 mpaka sasa tumefikia asilimia 56.9.
Kwa jumla ufaulu umekuwa unaongezeka lakini bado hatujafika pale
tunapopataka. Ufaulu wa wanafunzi ni
kielelezo cha ubora wa elimu wanayopata.
Hivyo basi, tunayo kazi kubwa ya kufanya kuinua ubora wa elimu
ncini. Katika BRN kuongeza ubora wa
elimu lilikuwa agenda mama na yote tunayofanya shabaha yake ni hiyo. Tunaendelea na utekelezaji wake na sina shaka
kwamba tukifanikiwa kutekeleza kwa ukamilifu elimu nchini siyo tu itamfikia
kila anayeistahili bali itakuwa ya ubora wa hali ya juu. Hakuna lisilowelezekana, kinachotakiwa ni
kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia
fursa hii pia, kuzipongeza Halmashauri zote na mikoa yote kwa kuitikia wito
wangu wa kujenga maabara katika shule zetu za sekondari ambazo hazina. Aidha,
nawashukuru wazazi, walezi na wadau kwa kujitolea kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa maabara. Wasivunjwe moyo na wale wachache
wanaojaribu kutukatisha tamaa. Kwa viongozi wa mikoa, Wilaya na Halmashauri, nakumbusha
kwa mara ya mwisho kuwa ujenzi wa maabara zilizokuwa hazijakamilishwa uwe
umekamilika ifikapo Juni 30, 2015.
Nimeona nirudie hili kuweka msisitizo.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Hapana shaka
kuwa tuko katika njia sahihi katika azma yetu ya kuleta mapinduzi katika sekta
ya elimu, na kuwaandaa vijana wetu kukabiliana na changamoto za maisha za
kujiletea maendeleo yao, ya jamii wanayoishi na nchi yao. Kila mmoja na atimize
wajibu wake ipasavyo. Mafanikio ya kuleta mapinduzi ya elimu yanategemea
mkusanyiko wa jitihada za wanafunzi, wazazi walezi, walimu, wamiliki wa shule
na vyuo ikiwemo serikali. Kila mmoja akilima
mraba wake vizuri katika shamba hili kubwa, matunda yake na neema zake ni
faraja kwetu. Tukifanya kinyume chake madhara yake ni hasara kwetu sote. Hivyo basi, kila mtu atambue wajibu wake katika kuhakikisha elimu inapatikana kwa watoto wetu
wote na ni wa ubora ya hali ya juu. Njia
nzuri ya kutimiza wajibu wako ni kuanza na shule ya msingi na sekondari iliyoko
katika eneo lako na kata yako maana hakuna eneo wlala kata isiyo na shule hizo na hakuna Mtanzania
asiyeishi katika kata.
Kila mmoja wetu
na ajiulize, amechangia nini katika kuboresha shule ya eneo na kata yake?
Amechangia nini katika kusimamia na kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya
kitaaluma ya mtoto aliyeko kwenye kaya yake? Elimu bora inawezekana na inaanza
na wewe. Timiza wajibu wako.
Mungu ibariki Tanzania!
Ahsanteni Sana kwa Kunisikiliza
Comments