STARS WALISHWA MIPANGO YA MABAO RUSTENBURG AMBAYO IKIKUBALI ITAKUWA BALAA COSAFA


Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij ameelekeza nguvu zake katika kuwafundisha wachezaji wa timu hiyo mipango ya kutengeneza nafasi na kufunga mabao.
Stars ipo Rustenburg, Afrika Kusini kwa ajili ya michuano ya nchi za Kusini mwa Afrika, COSAFA ambayo wao na Ghana wamealikwa kutia ‘nakshi’.
Na timu hiyo leo imeendelea na mazoezi yake kwa siku ya tatu tangu iwasili hapa, kwenye viwanja vya Michezo vya Rustenburg, katikati ya mji huu mdogo wa madini ya Platinum.
Nooij ambaye siku mbili zilizopita timu yake ilifanya mazoezi Uwanja Olimpia Park, ambako michuano ya COSAFA itafanyika, leo alikuwa akiwaelekeza wachezaji wake namna ya kusaka mabao.
Mshambuliaji Mrisho Ngassa akiunganisha krosi ya Juma Luizio (hayupo) pichani kufunga bao katika mazoezi ya Taifa Stars leo viwanja vya Michezo vya Rustenburg, Afrika Kusini

Alikuwa akiwaelekeza vijana wake namna ya kupanga shambulizi hadi kufika langoni kwa wapinzani na kufunga.
Na katika mfumo huo, wachezaji wa nne wote wa mbele walikuwa wanapishana nafasi, wakati mwingine wengine wakienda pembeni na kurudi katikati wakipishana.
Unaonekana kuwa mfumo mzuri wa kusuka nafasi za mabao, iwapo wachezaji watauelewa vizuri na kuweza kuufanyia kazi uwanjani.
Ni mfumo ambao mipira inayowapita washambuliaji, viungo wanatakiwa kuifuatilia kumalizia kwa mashuti makali.
Wote Mrisho Ngassa, John Bocco, Juma Luizo na Ibrahim Hajib walionyesha umahiri wa kufunga na kupiga krosi.
Viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mwinyi Kazimoto, Hassan Dilunga na Said Ndemla walikuwa makini katika kumalizia mipira inayowapita washambuliaji.
Kocha Msaidizi, Salum Mayanga alikuwa katika lango lingine akiinoa safu ya ulinzi dhidi ya mashambulizi ya aina tofauti, hususan ya kutokea pembeni kutokana na mipira ya kona na krosi.
Kipa Deo Munishi 'Dida' akiokoa krosi ya Ngassa (hayupo pichani) huku beki Shomary Kapombe akiwa tayari kumsaidia. Nyuma ni mshambuliaji Juna Luizio

Stars iliyopangwa Kundi A katika COSAFA, inatarajiwa kutupa kete yake ya kwanza Jumatatu Uwanja wa Olimpia dhidi ya Swaziland. 
Mbali na Swaziland, timu nyingine katika kundi la Taifa Stars ni Lesotho na Madagascar, wakati Kundi B lina timu za Shelisheli, Namibia, Zimbabwe na Mauritius.
Kila timu itakayoongoza kundi, itaungana na wenyeji Afrika Kusini, Botswana, Ghana, Malawi, Msumbuji na Zambia kwa ajili ya hatua ya Robo Fainali.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI