TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi akiwa kwenye mazungumzo na Ujumbe ulioongozwa na Mhe. Bernard K. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania. Mawaziri wengine katika picha ni Mhe. Louise Mushikiwabo (kulia kwa Waziri Membe), Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na Mhe. Amina Mohamed (mwenye skafu nyekundu), Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Simu: 255-22-2114615, 211906-12 
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz
Tovuti : www.foreign.go.tz
Nukushi: 255-22-2116600
               


                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM,  
                                    Tanzania.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri Membe aongoza Mawaziri wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye mazungumzo nchini Burundi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Mhe. Bernard K. Membe jana aliongoza Jopo la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Burundi kwa lengo la kupata hali ya maendeleo ya kisiasa nchini humo.

Wakiwa nchini humo, mawaziri hao walikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi, viongozi na wawakilishi wa vyama arobaini na tano vya siasa vya upinzani nchini humo, ambapo walitoa salamu za Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Waziri Membe, kwenye mazungumzo yao na Rais Nkurunziza yaliyodumu takriban saa moja na nusu, mawaziri hao walifikisha mwaliko kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, kuhudhuria Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi ambao umepangwa kufanyika Dar es Salaam Mei 13, 2015.

Kwenye jopo hilo la mawaziri liliongozwa na Mhe. Bernard Membe wa Tanzania, walikuwepo pia Mhe. Balozi Amina Mohamed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya na Mhe. Louise Mushikiwabo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda aliwakilishwa na Rtd Brig. Matayo Kyaligonza Balozi wa Jamhuri ya Uganda nchini Burundi.

“Lengo kuu la mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es salaam ni kujadili hali ya amani wakati wa kuelekea kipindi cha uchaguzi nchini Burundi” Waziri Membe aliwaeleza waandishi wa habari waliokuwa wakimsikiliza baada ya mazungumzo hayo. 

Kwenye mazungumzo hayo ya Burundi Waziri Membe alimuomba Rais Nkurunziza na viongozi wa vyama vya siasa nchini humo kutoa maelezo, na maoni yao kwa jopo hilo kwa uwazi na kupendekeza namna ambavyo viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakavyoweza kuisadia Burundi.

Pande zote mbili zilizoshiriki kwenye mazungumzo hayo na jopo la mawaziri kwa nyakati tofauti walielezea kufurahishwa kwao na hatua ya Rais Kikwete kuitisha kikao hicho cha Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili suala la Burundi kwa wakati muafaka.
Hadi wakati mazungumzo hayo, wakimbizi wapatao ishirini na nane elfu wameikimbia nchi hiyo kwenda Rwanda na Tanzania ambapo wengi wao wameingia nchini Rwanda. 

“Hili ni janga la kibinadamu ambalo ni lazima jumuiya yetu chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete kulipatia ufumbuzi kwa haraka” alimalizia Waziri Membe. 

Kwenye safari hiyo, Waziri Membe aliongozana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (NUU) pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Leticia Mageni Nyerere (Mb.).

-Mwisho-.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI KWA UMMA,
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
07 MEI 2015

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*